Imeelezwa
kuwa uhaba wa walimu na mlundikano wa wanafunzi katika madarasa ya awali
ni kikwazo kwa Tanzania kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030
yanayohimiza utolewaji wa elimu bora na yenye usawa.
Uchambuzi
wa takwimu uliofanywa na FikraPevu kuhusu elimu ya awali umebaini kuwa
miaka miwili mfufulizo tangu mwaka 2016, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika
madarasa ya awali umekuwa sio wa kuridhisha.
Hali hiyo
imesababishwa na upungufu wa walimu katika madarasa ya awali ambapo mzigo wa
walimu kufundisha watoto wengi umeongezeka, jambo linalotishia mstakabali wa
elimu ya watoto wanaoandaliwa kuingia katika shule za msingi.
Kwa mujibu
taarifa ya mapendekezo ya bajeti ya elimu ya Shirika la HakiElimu (2018)
yaliyotolewa hivi karibuni yanaonesha kuwa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa
mwaka 2017 ulikuwa mwalimu 1 kwa wanafunzi 159 (1:159) ukilinganisha na uwiano
wa mwaka 2016 ambapo ulikuwa 1:135.
Hiyo ni sawa
na kusema wanafunzi katika madarasa ya awali waliongezeka zaidi kwa mwaka 2017
lakini idadi ya walimu haikuongezeka au ilipungua kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo utekelezaji wa sera elimu bila malipo.
Kimsingi
mzigo wa walimu kufundisha umeongezeka ukilinganisha na mwaka 2016. Kwa
mfano kama darasa la moja la awali lilikuwa na wanafunzi 135 ina maana mwaka
uliofuata (2017) waliongezeka wanafunzi wengine 29.
Mtaala wa
Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 na vigezo vya Wizara ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), unapendekeza uwiano sahihi katika madarasa ya
awali ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 (1:25).
Ukilinganisha
na uwiano uliopo katika madarasa mbalimbali ya awali nchini, bado haukidhi
matakwa ya TAMISEMI na uwezekano wa wanafunzi kukosa maarifa ya msingi
kuwaandaa kuingia elimu ya msingi ni mkubwa.
|
Zinaeleza
zaidi kuwa uwiano wa mwalimu (kwa walimu wenye sifa) kwa wanafunzi
kwa mwaka huo ulikuwa 1:131 ambapo ni mara 5 zaidi ya uwiano unaotakiwa wa
1:25.
Maoni ya
Wadau.
Mkurugenzi
Mtendaji wa shirika la HakiElimu, Dk. John Kallage wakati akitoa mapendekezo ya
shirika kuhusu bajeti ya elimu ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 alisema serikali
inapaswa kuweka kipaombele katika utatuzi wa matatizo sugu katika sekta ya
elimu ikiwemo suala la ajira za walimu katika madarasa ya awali.
“Kutenga na
kuongeza bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na hasa
fedha zinazokwenda TAMISEMI kwa ajili ya elimu msingi. Kutenga bajeti yenye
uhalisia wa kutatua changamoto sugu na muda mrefu za miundombinu
mashuleni na kuweka kipaumbele katika suala la ajira za walimu,” alisema
Dk. Kallage.
Serikali
imeshauriwa kuanzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa madarasa ya awali
kama ilivyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuboresha ustawi wa elimu ya
watoto nchini.
Kwa upande
wake, Mwandishi wa Vitabu na Mwanaharakati wa masuala ya Watoto, Richard Mabala
amesema licha ya kuongeza idadi ya walimu katika madarasa ya awali, wanafunzi
wapewe ulinzi na elimu bora itakayowakomboa fikra na maisha yao.
“Mimi
naamini suala kubwa elimu bure, pili ulinzi kwasababu mimi kama mzazi nikijua
shuleni wasichana wanatongozwa, wanatishiwa kubakwa na njiani hakuna ulinzi.
Kwahiyo kuwe na ulinzi wa kutosha kuhakikisha watoto wako salama,” amesema.
Msimamo
wa Serikali.
Serikali
kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako imesema
inaendelea na jitihada za kuboresha elimu ya awali kwa kujenga madarasa,
kuajiri walimu na kuhakikisha vifaa vya kujifunzia na kufundishia vinakuwepo
mashuleni.
Akisoma
bajeti ya elimu jana, Prof. Ndalichako alisema, “Katika kusimamia Elimu ya
Msingi na Sekondari, katika mwaka 2018/19 Wizara itatekeleza yafuatayo:
itaandaa Mwongozo wa Kitaifa wa uendeshaji wa Elimu ya Awali unaozingatia
viwango.
Lengo la Mwongozo huo ni kufafanua viwango vya Elimu ya Awali kwani
kwa sasa kuna mifumo mingi ambayo inahitaji uratibu wa karibu kwa ajili ya
kuwawezesha wanafunzi hao kusoma katika mazingira tulivu na salama yenye
kusaidia kuinua ubora wa elimu na mafunzo.”
|
No comments:
Post a Comment