Muonekano wa jengo hilo kutokea barabara ya Makongoro Jijini Arusha. |
Na Hamza
Temba - WMU
........................................................
JENGO la
kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro jijini Arusha ambalo
ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi juni mwaka huu litakuwa kivutio cha
kihistoria cha utoaji wa huduma za utalii hapa nchini.
Hayo
yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla muda
mfupi baada ya kukagua jengo hilo ambalo linasemekana kuwa refu kuliko majengo
yote jijini Arusha likiwa na jumla ya ghorofa 18.
Alisema
jengo hilo ambalo linatizamana na Round About ya AICC katikati ya jiji hilo,
limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja (One Stop Centre) cha shughuli zote za utoaji wa
huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa
ujumla.
Alisema
jengo hilo litatoa fursa kwa wadau mbalimbali wanaotoa huduma za utalii kuweka
ofisi zao ikiwemo mabenki, watoa huduma za usafiri, mashirika ya ndege,
mawakala wa safari za utalii na huduma, maduka ya bidhaa za utalii na mahoteli.
"Tutapamba
pia jengo hili na" live screen" (Mabango ya Video Mubashara) za
vivutio, hivyo wanyama wakiwa wanapita huko porini watakuwa wanaonekana
"LIVE" (Mubashara) kwenye jengo hili kupitia LED Screen ambazo
zitakuwa zimezunguka jengo hili" alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema
huduma nyingine zitakazotolewa katika Jengo hilo ni pamoja na zile za kuangalia
jiji la Arusha kupitia darubini, huduma za burudani ikiwemo kumbi za starehe na
migahawa.
Kwa upande
wake Mkandarasi wa Jengo hilo, Mhandisi Bismas Meela wa Kampuni ya
Inter-Consult limited alisema ujenzi wa jengo hilo ambalo ulianza mwezi
Novemba, 2013 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.
Alisema
jengo hilo ambalo lina uwezo wa kupaki magari 67 kwa wakati mmoja katika
ghorofa za chini linagharimu shilingi za Kitanzania bilioni 45.
|
Dk. Kigwangalla na msafara wake wakiangalia umbo la uso wa Simba uliotengengenezwa katika moja lango la kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo. Milango yote ya kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo itapambwa kwa taswira mbalimbali za wanyamapori. |
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu kuhusu jengo la kitega uchumi la mamlaka hiyo lililopo katikati ya Jiji la Arusha ambalo limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja cha shughuli zote za utoaji wa huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa ujumla. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. |
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mandhari ya Jiji la
Arusha akiwa juu ya Jengo la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Kutoka kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka hiyo, Asangye Bangu na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. |
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishuka kwenye ngazi maalum zinazotumia nishati ya umeme ndani ya Jengo hilo. Kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu na nyuma yake ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. |
No comments:
Post a Comment