Serikali ya Tanzania, imetangaza rasmi kuanza kwa
kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote
walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia .
Aidha, imewataka watumishi hao waanze
kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na mabadiliko
makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini
Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako
wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa
mwaka wa fedha 2016/2017.
Amesema Serikali ya awamu ya tano
imejipanga kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu nchini ili
kuhakikisha kuwa Elimu inayotolewa katika shule, vyuo na taasisi mbalimbali
inazalisha wahitimu wenye sifa na ubora kwa maslahi ya Taifa .
Amesema katika kulitimiza hilo
Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria watendaji wote
walioshiriki na wale wanaoendelea kushiriki kwa namna moja au nyingine kukwamisha
maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na wale waliohusika katika udahili wa
wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.
"Serikali
ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati kabisa kuboresha kiwango cha elimu yetu
kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, naomba niwahakikishie
kwamba pale panapohitajika kufanyika mabadiliko tutayafanya bila woga" Amesisitiza.
Amesema katika kutafuta ufumbuzi wa
changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini, serikali imejipanga kubadilisha
mfumo wa elimu ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko
hayo yatafanyika kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.
"
Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa elimu tumekubali kwamba tuna
changamoto, katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa kuanzia hivyo
tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono" Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Prof.Ndalichako Amesema lengo la
Serikali kupitia Wizara yake ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa hapa
nchini kwa kuendelea kutoa wahitimu bora wanaokidhi vigezo na viwango katika
soko la ajira.
Amesisitiza kuwa mkakati wa Serikali
ni kuanza kuwafuatilia wahitimu wote wasio na viwango ambao wako katika maeneo
mbalimbali ya ajira huku akisisitiza kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na
kiwanda kinahitaji malighafi nzuri ili kitoe bidhaa bora.
Ameeleza kuwa Serikali imejipanga
kikamilifu kuvikagua vyuo vyote vinavyotoa elimu ya juu kuona kama vinakidhi
sifa na vigezo vya kiutendaji ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale
wote wanaowadanganya wananchi na kuwapotezea muda vijana wanaowadahili
bila kuzingatia sifa.
"Wizara
yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta hii muhimu, tulichofanya Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo vingine"
Kuhusu ujenzi wa maabara amesema kuwa
Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa
vya maabara kwa shule zote 1536 ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya
maabara kote nchini.
Katika hatua nyingine , amesema kuwa
Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya
Maendeleo ya Jamii kote nchini ili majengo ya vyuo hivyo yaweze kutumika
kuanzishia vyuo vya Ufundi Stadi VETA katika wilaya na mikoa ili kuwapatia
stadi za kazi vijana waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wao baadhi ya Wabunge
waliopata nafasi ya kuchangia wakati wa Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo
wameiomba Serikali kuweka mkazo katika usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili
shule, Taasisi na vyuo vya Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya
Taifa.
Aidha, wameiomba Serikali kupitia
Bajeti hiyo itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi
wa shule, kuboresha maslahi na kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha
Mamlaka za Udhibiti wa Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
|
No comments:
Post a Comment