Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
kimewasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa
sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja.
Jana,May 28,2016, lilitolewa tangazo chuoni hapo
likiwataka wanafunzi hao kuondoka kati ya jana hadi leo saa 12 jioni.
Tangazo
hilo lilieleza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa
stashahada hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na wataelezwa
mustakabali wao “mapema iwezekanavyo”.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa
Idrisa Kikula alipotakiwa kufafanua suala hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala
hilo lipo lakini akaelekeza apigiwe simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice
Baltazal kwa maelezo zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema
kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na wametakiwa
kulitekeleza.
Kuhusu lini na nini hatima ya
wanafunzi hao, alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko
kwa wanafunzi hao juu ya namna walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao
kwa ghafla na kutakiwa kuondoka.
Kozi ya stashahada ya ualimu wa
sayansi, ilianzishwa maalumu kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la
kuziba pengo la walimu wa sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na sifa za kujiunga na
kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo
ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa
na Serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo
Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika hawakuwa na sifa za
kudahiliwa.
|
No comments:
Post a Comment