Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis
Kigwangalla akitoa tamko kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa
kipindupindu katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani)
ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Pichani chini kushoto ni Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Afya (Kaimu Mkurugenzi),
Michael John.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dkt. Hamis Kigwangalla ametoa tamko kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa
wa kipindupindu ulioanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es
Salaam na kusambaa kwa kasi katika Mikoa mingine 21 ya Tanzania Bara
ambayo ni Pwani, Morogoro, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita,
Mara, Manyara, Arusha, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa,
Kagera, Katavi, Mbeya na Mwanza na Simiyu.
Tangu
ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 12,810 wameugua Kipindupindu, na kati
yao jumla ya watu 202 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na
asilimia 1.6 ya waliougua.
Katika kipindi cha wiki iliyoanza tarehe 28
Desemba 2015 hadi tarehe 3 Januari 2016, kumekuwa na jumla ya wagonjwa
walioripotiwa 590 na vifo 6, ambayo ni asilimia 0.01 ya wagonjwa wote.
Mkoa wa Mara (Musoma Mjini) ndio ulikuwa unaongoza kwa kasi ya
maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu ukifuatiwa na Singida (Iramba),
Morogoro (Morogoro Vijijini) na Manyara (Simanjiro).
Takwimu
zinaonyesha kuwa licha ya kuwa na nafuu katika wiki ya nyuma, wiki hii
kasi ya maambukizi inaonesha kupanda tena kwenye mikoa ya Mwanza na
Arusha. Katika mkoa wa Arusha, maambukizi yamepanda kutoka wagonjwa
wapya 60 hadi 111 kwa wiki.
Katika mkoa wa Mwanza, kasi ya maambukizi
imepanda kutoka wagonjwa wapya 45 hadi 66 kwa wiki.
Kasi
ya maambukizi ya Kipindupindu katika wiki iliyopita imepungua kwa kiasi
kikubwa katika mikoa ya Mbeya na Tanga. Aidha, mikoa ya Dar-es-Salaam
na Lindi haijaripoti mgonjwa yeyote mpya wa Kipindupindu katika wiki
iliyopita.
Tunawapongeza kwa hatua hii kutokana na juhudi zinazofanywa
na wadau ambao kwa pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa
karibu zaidi.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana
na Sekta nyingine husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea
kukabiliana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali.
Kikosi kazi maalum
chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kinakamilisha mpango
unaoshirikisha Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na
Watoto , TAMISEMI, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, DAWASCO, DAWASA,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Sekretariat ya
Mkoa wa Dar-es-Salaam, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mikakati ya
kupambana na ugonjwa huu inakuwa jumuishi na ya haraka.
Bado
Wizara inaendelea kusisitiza kuwa, ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo
vinavyotokana na ugonjwa huu, wananchi wanasisitizwa kunywa maji yaliyo
safi na salama, kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira
yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi
yanayotiririka:- kabla na baada ya kula, baada ya kutoka
chooni,Baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia
mgonjwa Aidha,
ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia vyoo wakati wote na
kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani.
Wizara ilishapiga marufuku kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula
barabarani katika mazingira yasiyo safi na salama.
Hivyo, Mamlaka za
Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji ambao ni Waganga Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya, ziendelee kutoa taarifa kuhusu
utekelezaji wa jambo hili.
Wizara
inapeleka tena timu za wataalm katika mikoa iliyoathirika zaidi na
kipindupindu ambayo ni Simiyu, Mara, Morogoro, Manyara, Singida, Arusha
na Mwanza. Timu hizi zitaungana na timu za mkoa wa wilaya kusaidia
kudhibiti ugonjwa huu.
Hitimisho
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea
kukumbusha kuwa, mikoa ambayo bado haijaathirika ichukue hatua za
tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu.
Mwakilishi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini, Dk Rufaro Chatora (kulia)
akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo
pichani) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano makao makuu ya wizara
hiyo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Afya (walioketi) na waandishi wa habari katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment