Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuzifuta wizara
15 kati ya zilizopo sasa na kubaki na baraza dogo litakalokuwa na wachapakazi
makini ili kutimiza dhamira yake ya kubana matumizi na kuinua maisha ya
Watanzania.
Kadhalika,
inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta mabadiliko ya kweli wakati
akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na ushindi wa asilimia 58.46 dhidi
ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, sasa yuko mbioni kutangaza
baraza lake la mawaziri litakalokuwa na wizara 15, idadi inayofanana kwa kiasi
kikubwa na ile ya Baraza la Mawaziri la miaka ya 1980 lililoundwa na Rais wa
Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Serikali ya
awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, 2015 ikiwa na Wizara 30.
Kadhalika, alipoingia kwa
mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye
mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Kufikia leo,
Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015, tayari ameshamteua Mbunge wa
Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa serikali yake ya awamu ya tano na
Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge la 11.
Chanzo
kimoja cha uhakika kimedokeza jana kuwa hivi sasa, tayari Rais Magufuli kwa
kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa
kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba, kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza
wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo hicho
kilidai kuwa Dk. Magufuli ambaye amejichimbia mjini Dodoma tangu mwishoni mwa
wiki iliyopita, anatarajiwa kutangaza baraza lake dogo la mawaziri wakati
wowote kuanzia leo.
“Halitakuwa
sawa na hili alilomaliza nalo Rais Kikwete… na wala halitakuwa na watu wengi
kama lile aliloingia nalo kwa mara ya kwanza Rais Kikwete mwaka 2005. Ni baraza
dogo tu na wizara kadhaa hazitakuwapo,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu
wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mawaziri wanakuwa
wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa ibara ya 54, mawaziri
huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
“Kuna mambo
madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo Mheshimiwa Rais atalitangaza Baraza
la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo. Kimsingi mkakati wake ni kuwa na baraza
dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo hicho.
Aidha,
ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo zitakuwa mpya na
kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu ya nne wana nafasi ndogo
ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa kiasi
fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la Serikali ya Mwalimu Nyerere
miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo la kubana matumizi ya
serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi usiku na mchana ili kutimiza
lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea maisha bora Watanzania,” chanzo
kiliongeza.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alikuwa na serikali yenye
wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya Mipango; Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya
Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii.
Wizara
nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni; Wizara ya Afya; Wizara ya
Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria;
Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment