Agizo la
Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu katika
utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo zitatakiwa
kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Muda mfupi
baada ya kuapishwa na kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya mkuu wa nchi, Rais
alifuta safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali na viongozi ili kuokoa
fedha zinazotumika kwa ajili hiyo na kuagiza shughuli hizo zifanywe na
mabalozi.
Rais alisema
safari hizo zitadhibitiwa na Ikulu ambayo itatoa kibali kwa safari maalumu,
ikiwa ni pamoja na kuweka masharti ambayo mtumishi anayetakiwa kusafiri
atatakiwa kuyatimiza kabla ya kupewa kibali.
Lakini
utekelezaji wa agizo hilo unakabiliwa na vikwazo vingi, hasa vikubwa vitano
ambavyo ni uchache wa balozi za Tanzania nje ya nchi, ukomo wa madaraka ya
mabalozi, wigo wa ufahamu wa mambo ya kitaalamu na ukosekana kwa mazungumzo
endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili tofauti kwenye mikutano
miwili tofauti.
Idadi ndogo
ya balozi.
Takwimu za
Umoja wa Mataifa (UN), zinaonyesha kuwa hadi sasa chombo hicho kina wanachama
193 ambao nchi zinazaweza kuwa na uhusiano nazo wa kidiplomasia, kwa mujibu wa
makubaliano ya wanachama wa umoja huo.
Kwa mujibu wa wakosoaji, uchache huo
utasababisha mabalozi hao kusafiri sehemu mbalimbali duniani kushiriki kwenye
shughuli ambazo viongozi wa umma walitakiwa kwenda, hali ambayo itasababisha
safari kuwapo kama kawaida isipokuwa wanaosafiri ndiyo watakaobadilika.
“Ni kweli
kwamba idadi ya watu wanaosafiri itapungua, lakini ile dhana ya safari itabakia
vilevile,” alisema mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka jina lake litajwe.
“Kwa mfano,
mkutano wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Malta, Balozi wa Tanzania nchini
Uingereza ndiye atatakiwa kwenda. Kwa hiyo ni safari pia.”
Bara zima la
Amerika Kusini lina ofisi moja tu ya ubalozi iliyoko Brasilia, Brazil, wakati
bara la Amerika Kaskazini lina balozi tatu, mbili zikiwa Marekani--Umoja wa
Mataifa jijini New York na Washington--, huku Ulaya yenye nchi 50 ikiwa na
balozi nane, wakati Asia, Arabuni pamoja na Australia kuna ofisi nane za
ubalozi.
Bara la
Afrika lenye nchi 52, ndiko kuna balozi nyingi zaidi, kukiwa na ofisi 14.
Ugumu katika
utekelezaji unaosababishwa na idadi ndogo ya mabalozi pia ulidokezwa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata
Mulamula mapema mwezi huu.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye alikuwa akijibu maswali
kuhusu vikwazo vitano vya utekelezaji wa agizo hilo la Rais, alisema suala hilo
linaweza kujibiwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Lakini
msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga alisema atumiwe ujumbe wa barua pepe ili
ajibu suala hilo.
Ukomo wa
madaraka ya mabalozi.
Suala
jingine linalozungumziwa ni ukomo wa mabalozi katika mamlaka yao, hasa pale
wanapotakiwa kumuwakilishi Rais wakati hawabebi madaraka hayo ya mkuu wa nchi.
Mara nyingi wakuu wa nchi huona umuhimu zaidi
wa kuwa na mazungumzo baina yao kuliko na mabalozi inapotokea wamekutana kwenye
mikutano ya mikubwa kama ya Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, Sadc na
mingine inayoweka maazimio muhimu kuhusu masuala kama ya mazingira, afya, na ya
kibiashara.
Lakini
Balozi Sefue alisema Rais atakuwa akihudhuria mikutano michache na hivyo uamuzi
huo hautaathiri nchi.
“Ni mikutano
michache sana ambayo wanahudhuria wakuu wa nchi,” alisema Balozi Sefue. “Pale
ambapo tutajiridhisha kuwa ubalozi hauwezi kutuwakilisha vizuri, basi
tutaruhusu mtu atoke hapa nyumbani. Hiyo itakuwa ni baada ya kujua ni nani
atakayekwenda na atakwenda kufanya nini,” alisema Balozi Sefue.
Kwa uzoefu
wake, alisema hata viongozi watakaopewa ruhusa hawatakuwa na misafara mirefu
kama ilivyokuwa awali kwa kuwa wapo baadhi yao ambao wanakuwa hawafanyi
chochote huko waendako.
“Nilipokuwa
Washington niliwahi kushuhudia. Kuna msafara ulikuja, mkubwa sana na kwa
kipindi chote walichokaa pale, wapo baadhi hawakupata nafasi ya kufanya
chochote. Hili nalo ni miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika vibali
vitakavyokuwa vinatolewa kwa wale watakaokidhi masharti,” alisisitiza.
Kuhusu
ukubwa wa ujumbe ambao kiongozi anaruhusiwa kuambatana nao aendapo nje ya nchi,
msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga amewahi kufafanua kuwa, kwa
mujibu wa itifaki, kila mmoja ana maelekezo yake.
“Msafara wa
Rais hauwezi kulingana na wa makamu wake, Waziri Mkuu au waziri wa kawaida
ambao pia hutofautiana na makatibu wakuu au wakuu wengine wa idara na vitengo
vya Serikali,” alisema Kasiga wakati akitoa ufafanuzi juu ya gharama za safari
za nje wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Uwakilishi
wa mamlaka ya Rais.
Mbali na
vikwazo hivyo, suala jingine ni mabalozi kubeba majukumu ya Rais kwenye
mikutano ya nje jambo ambalo wakosoaji wanasema litawawia vigumu hasa
watakapotakiwa kufanya uamuzi kwa madaraka ya mkuu wa nchi.
Lakini
Balozi Sefue alisema mabalozi watakaotumwa kwenye mikutano hiyo watabeba kofia
hiyo ya mkuu wa nchi na taarifa itakayotumwa nchini itakuwa na uzito
unaostahili hivyo suala hilo halitaathiri ushiriki wa nchi.
Mabalozi
kutokuwa na utaalamu.
Uwezo wa
mabalozi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kitaalamu pia ni moja ya mambo
yanayoonekana kuwa kikwazo kwa agizo la Rais Magufuli kuzuia safari za nje.
Lakini
Balozi Sefue alisema matukio yanayohusu masuala ya kitaalamu kama kilimo,
mazingira, afya, madini na mawasiliano ambayo yanahitaji watendaji waliobobea
kwenye fani hizo, yatawekewa utaratibu licha ya kuwa changamoto kwa mabalozi.
“Kila
ubalozi una wataalamu wa masuala mbalimbali ambao wanaweza kutoa mchango unaostahili
kwa lolote linaloweza kuhitajika,” alisema.
“Si rahisi
kukosa mtu mwenye uwezo wa kumsaidia balozi kutekeleza majukumu yake kiasi cha
kuhitaji mtu mwingine kutoka nyumbani. Lakini likijitokeza hilo, tutatuma
mwakilishi.”
Akizungumzia
suala hilo, Balozi Mulamula alisema mapema mwezi huu kuwa utekelezaji huo
utachukua muda kidogo kutokana na balozi nyingi kukosa fedha na watalaamu.
Suala la
fedha kwenye balozi za Tanzania limekuwa kilio kikubwa kila wakati wa Bunge la
Bajeti na mwaka huu suala hilo liliibuka kwenye hotuba ya kambi ya upinzani
iliyosema kiasi cha Sh30 bilioni ziloizotengwa kwa wizara hiyo hazikutosha
kuwawezesha mabalozi kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Suala la
weledi pia lilizungumzwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ya mwaka 2014/15
ikisema uteuzi holela wa mabalozi usiozingatia sifa, unalikosesha Taifa fursa
nyingi za kiuchumi kwa kuwa wengi hawana ufahamu wa fursa zilizoko kwenye nchi
wanazokwenda.
Lakini
mapema mwezi huu, Balozi Mulamula alisema suala hilo sasa litaangaliwa kwa
jicho la karibu zaidi, hasa uteuzi wa mabalozi.
Alisema
watatoa mwongozo ambao utawataka wawakilishi hao wasibweteke katika utendaji
wao kwa kuwa kuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kupima matokeo ya utendaji
wao kwa kila baada ya kipindi kitakachoelekezwa.
“Kwa sasa
tutakuwa tunawapima mabalozi wetu kwa malengo tuliyokubaliana nao ambayo
yanaweza kuwa ya mwaka au zaidi.
Tutakuwa
tunamuuliza balozi umeweza kuleta watalii au kuwahamasisha wawekezaji wangapi
nchini?” alisema.
“Hii ni kwa
sababu zamani tulikuwa tunakwenda kienyeji lakini kwa sasa hapa kazi tu.”
Mazungumzo
endelevu.
Kikwazo
kingine kinachoonekana kwenye utekelezaji wa agizo hilo ni kukosekana kwa
mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili tofauti
kwenye mikutano miwili tofauti.
“Mfano iwapo
kutakuwa na mkutano wa suala fulani la Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini
Kenya, kwa agizo hilo la Rais, atakayewakilisha ni balozi wa Tanzania nchini
Kenya,” alisema mkosoaji huyo na kuongeza:
“Iwapo suala
hilo litaendelezwa kwenye mkutano mwingine wa jumuiya nchini Uganda, ni dhahiri
atawakilisha balozi wa Tanzania nchini humo ambaye hakuwapo kwenye mkutano wa
Kenya. Kwa hiyo kutakuwa na upungufu.”
Balozi Sefue
hakutaka kufafanua kuhusu hoja hiyo na badala yake akaielekeza kwa Wizara ya
Mambo ya Nje, ambayo alisema ina nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia.
Source:-:Mwananchi.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment