4. Mwenye uadilifu usio na shaka
Mgombea bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa kuwa na uadilifu uliotukuka, usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana kuwa, awe ni mtu ambaye uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa Taifa zima. Awe na rekodi za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina maana kuwa, wananchi wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka haraka wasimame na kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”. Marais wengi walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na Marekani kwa kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa hii.
Hatari ya sifa hii
Kigezo hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo uelewa wa wananchi vijijini na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu nao huweza kuchafuliwa ndani ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si ajabu mgombea akawa hata na uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili kimchafue mwenzake, sifa za mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope. Vyama vya upinzani vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha uadilifu wa mgombea wake unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na propaganda za CCM.
5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua
uchumi
Moja ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania ni usimamizi wa uchumi. Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa kutekeleza mipango yetu kwa sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila dakika na ambao hauna dira. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu ambaye akisimama na kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote wanamwelewa, kwamba “naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa umaskini wa nchi”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango kabambe ya uchumi lakini yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa umaskini, lakini pia ni pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi. Katika nchi maskini, wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi ili kuwahakikishia wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza kutekelezeka kwa wakati
6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa
Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa mtu wa kipekee ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano dhidi ya rushwa, ndogo na kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba anapiga vita rushwa, bali anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu ambaye yuko mbali kabisa na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani watatafuta mgombea wa namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule wa CCM, kwamba ukiwaweka pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme “…naam huyu wa upinzani anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”
Hatari ya sifa hii
Ikiwa upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika mapambano ya rushwa lakini ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya mipango ya upinzani inapaswa kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya ya usimamizi wa mapambano dhidi ya rushwa na hata kueleza watu watakaokuwa na sifa za kufanya kazi na mifumo hiyo.
7. Asiyependa kulipiza visasi na
atakayefuata sheria
Jambo hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka upinzani anapaswa kuwa na sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa kutokuwa na tabia ya kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa ya sheria katika utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya kisheria ambayo ni lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate, mfano, wizi wa pesa za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi upo, lazima watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala kupotea”. Lakini kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo yalikuwa yanatendwa na uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na zisizo na maana, hayana haja ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.
Hatari ya sifa hii
Wananchi wengi huhofia masuala ya usalama iwapo vyama vipya vitaingia madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo hupoteza usalama ni “kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani vinawajibika kuwa na mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya nyuma ya kiutendaji, ila atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa makusudi na kwa kutofuata sheria.
8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi
Tangu tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika kwa kuwa na mifumo mibovu na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni janga kubwa. Rais bora ajaye kutoka upinzani ana kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi katika kila eneo ili mifumo ifanye kazi kwa mbio na kwa tija kubwa zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka ya 1990 na bado wako gerezani bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari Kilombero na huko bei ya sukari ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni matatizo makubwa ya kimfumo. Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuja kubadilisha kabisa mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa bahati nzuri, upinzani unaweza kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo havikuwahi kuongoza Serikali na vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.
Hatari ya sifa hii
9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba
Suala la katiba mpya ni ajenda muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe kuwa na busara za kutosha na msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba na hasa mchakato wa Katiba Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na misimamo ya wananchi katika suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama katiba itapitishwa au la na hatuelewi kama wananchi wanaikubali au wanaikataa. Nani atatuvusha na kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo mgombea bora wa urais kutoka upinzani.
Hatari za sifa hii
Msimamo wowote ule wa mgombea urais wa upinzani katika jambo hili unaweza kuwa na athari chanya au hasi kulingana na namna wananchi wanavyolitazama suala la katiba. Kama mgombea huyu atakuwa na msimamo katika kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi, jambo hili peke yake litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa kinyume chake, litakuwa na athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama athari yenyewe ni chanya au hasi.
10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa
Moja ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni kuliwakilisha Taifa katika masuala ya kimataifa. Rais bora kutoka upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya masuala ya kimataifa, si kuishi Ulaya na Marekani, lakini kuwe na ushahidi wa kutosha kuwa amewahi kushiriki katika baadhi ya shughuli muhimu za kimataifa na kwamba huenda hata kimataifa yeye ni mtu bora. Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea mwenye sifa hii pia, ni jukumu la upinzani pia kuwa na mtu ambaye amejipanga vyema kimataifa na mambo aliyoyasimamia kimataifa pia yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali, yanaweza kuwa ya kijamii, ya kitaasisi au ya kitaaluma.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za kuisaidia CCM, kwamba ndicho chama pekee chenye watu waliofanya kazi za kimataifa na wataifanya Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea ambaye tayari wananchi wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na shaka ili kusiwe na tabu ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura juu ya eneo hili.
HITIMISHO
Andiko hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote muhimu za kiongozi bora kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha Taifa. Nimechokoza mjadala wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya kuongoza Serikali si nyepesi, inataka kujipanga kila idara na kuwathibitishia wapigakura kuwa mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura huwa ni kutafuta namna gani watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati nzuri vyama vya upinzani katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya kupigiwa mfano inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji na utendaji kazi bora. Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759. Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.
Pata
Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori
inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
Monday, June 22, 2015
UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:-Sifa 10 za mgombea urais bora wa upinzani 2015.
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment