Aidha baada ya kuhukumiwa kulipa faini Sh1 milioni
au kwenda jela mwaka mmoja hapo June 17, 2015 kwa kosa la shambulio la kawaida
dhidi ya aliyekuwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu uliopita wa 2010,
Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwania tena
ubunge katika jimbo hilo.
Mbowe
aliyeepuka kwenda jela kwa kulipa faini hiyo june 17,2015, alitangaza uamuzi
huo june 18,2015 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la stendi
ya zamani mji mdogo wa Bomang’ombe, Kilimanjaro.
Mwenyekiti
huyo alifikia hatua hiyo baada ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo
kumshinikiza agombee ubunge na kumchangia Sh800,000 za kuchukua fomu ambayo
ndani ya Chadema hugharimu Sh250,000.
“Nashukuru
kwa walioanzisha wazo hili lakini zaidi ninawashukuru waliojitolea kunichangia
fedha. Nimekubali nitagombea ubunge katika uchaguzi ujao,” alitangaza Mbowe na
kufanya uwanja kulipuka kwa shangwe.
Mbowe
aliyeambata na wabunge kadhaa akiwamo Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini,
alijinasibu kuibuka na ushindi wa kishindo yeye na chama chake katika uchaguzi
ujao kuanzia jimbo la Hai na katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kama sheria
ingekuwa inaruhusu ningefurahi iwapo CCM ingesimamisha wagombea zaidi ya 10
katika Jimbo la Hai ili wapambane na mimi kwa sababu mgombea mmoja pekee siyo
saizi yangu,” alijinasibu Mbowe.
Hukumu dhidi
yake
Akizungumzia
hukumu iliyomtia hatiani na kuhukumiwa faini au kifungo, Mbowe ambaye pia ni
Kiongozi wa Upinzani Bungeni alisema alikusudia kwenda jela kuwakilisha
mamilioni ya Watanzania wanaosota huko “kwa kesi na hukumu za kipuuzi”.
“Kama kesi
ya mtu mwenye dhamana ya uwakilishi wa wananchi kwa nafasi ya ubunge inaweza
kuendeshwa kwa zaidi ya miaka minne na hukumu kutolewa katika mazingira
tatanishi kama ilivyokuwa kwangu, Watanzania wa kawaida wanateseka kiasi gani?”
alihoji
Mbowe.
Alidai kuwa
baada ya kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja au faini ya Sh1,000,000, Hakimu
Denis Mpelembwa amepandishwa cheo kuwa hakimu mkazi na kuhamishiwa mkoani
Kagera, siku moja tu baada ya hukumu.
“Kilichokuwa
kinatafutwa ni namna ya kumzuia Mbowe asigombee ubunge Hai kwa sababu CCM
wanajua nguvu yangu. Wamekosea sana kwa sababu hukumu ile hainizuii kugombea.
Nitagombea na nitashinda kwa kishindo,”-“Ninao
wanasheria mahiri ambao baada ya kupitia hukumu yangu kwa harakaharaka,
wamenihakikishia kwamba adhabu ile hainizuii kugombea na wanaendelea na
taratibu nyingine za kisheria kuiomba Mahakama Kuu kuitangaza kuwa batili,”
alisema.
Wabunge
wanena
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, wabunge waliohudhuria mkutano huo, Pauline Gekul, Grace
Kiwelu, Rose Kamili na Joseph Selasini waliwaomba wakazi wa Hai kuhakikisha
Mbowe anarejea tena bungeni kutokana na uwezo wake wa kiuongozi.
“Ili
tufanikishe lengo la kumrejesha Mbowe bungeni na wagombea wengine wa Chadema,
mnatakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na
kujitokeza kupiga na kulinda kura Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Gekul.
Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment