![]() |
Simba SC |
Wekundu wa Msimbazi Simba SC
imezidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia
ushindi wa mabao 4-1 ilioupata leo
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya timu ya JKT Oljoro ya Arusha ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili
baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa
kadi nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa
na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles
Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1,
mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika
za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
Kiemba alifunga bao la kwanza
akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na
krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa
kulia.
Nonga naye alifunga bao lake
baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma
Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
Kipindi cha pili katika Dakika ya
83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru
penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango
huyo.
Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza
mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa
rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini
akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha
pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu,
ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
Matokeo na ratiba Jumapili
Oktoba 7
Mgambo Shooting 1 v 0 Polisi Morogoro (Uwanja wa Mkwakwani,Tanga)
Toto Africans 2 v 1 JKT Ruvu
(Uwanja wa Kirumba, Mwanza)
Tanzania Prisons 0 v 0 Mtibwa
Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya)
Jumatatu Oktoba 8
Kagera Sugar v Yanga (Uwanja wa
Kaitaba, Bukoba)
No comments:
Post a Comment