Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi aliyewahi
kuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mpwapwa Mkoani Dodoma
Bw. Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa familia
yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda.
Watu hao wamefariki dunia baada
ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na Lori jana tarehe 17 Septemba, 2017 majira ya saa 4:00 Usiku katika barabara ya
Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea Tanzania.
“Nimepokea taarifa ya vifo
hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya
watu, nampa pole Ndg. Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa pole wanafamilia,
ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi.
“Nawaombea marehemu wote
wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata matibabu huko
nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka
wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika
kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu
waliowategemea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Septemba, 2017
|
No comments:
Post a Comment