Mbunge wa
Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefunguka na kudai amerudi nchini akiwa na unyenyekevu
mkubwa zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri alioonyeshwa na Mbunge Tundu Lissu
pindi alipokwenda kumjulia hali katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Zitto
ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa facebook asubuhi ya leo na kusema japo
Lissu ameumizwa sana lakini hakuacha kumuonyesha ucheshi licha ya kuwa na
maumivu makali aliyokuwa nayo katika mwili wake.
"Siku
mbili hizi nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa mawazo sana, nimerudi
nchini nikiwa kwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao
ndugu yangu amenionesha licha ya kuwa kwenye maumivu makali. Siyo mara nyingi
hapa nchini kusikia tukiongelea ujasiri lakini namfikiria lissu na vile
nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi, najua hivyo ndivyo alivyo",
ameandika Zitto.
Pamoja na
hayo, Zitto ameendelea kwa kusema "waliomshambulia wamemuumiza kweli na
bado wakati tuliokuwa naye amenionesha shukrani, ari na pia ucheshi. Huo ni
ujasiri, alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu siyo kitu rahisi kwa mtu
yeyote kutafakari. Kufikiria hali ile kungeniacha niumie moyo kama asingesema
maneno haya kwangu kuwa 'tumeshinda. Tumeshashinda", amesisitiza
Zitto.
Mbunge Tundu
Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa
Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa kwenda jijini Nairobi
Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata, ambapo mpaka
sasa yuko huko kwa matibabu.
|
No comments:
Post a Comment