Baadhi ya
wasichana na wanawake wadogo watakaofikiwa na mradi katika Picha ya pamoja
wakati wa uzinduzi wilayani Kahama mkoani Shinyang'a.
|
Afisa Tawala
wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila akikata utepe kuashiria uzinduzi wa
mradi wa Dreams Innovation Challenge wilayani humo.
Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la IDLO kimezindua
mradi wa Kuwajengea Uwezo wa Kisheria Wasichana na Wanawake Wadogo mkoani
Shinyanga ili Kuweza Kuiwajibisha Jamii Kutoa Huduma Bora za Afya ya UKIMWI.
Katika
uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Septemba 14 katika manispaa ya Shinyanga na
Septemba 15,2017 katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, makundi lengwa ya mradi huo
ikiwemo wasichana na wanawake wadogo, wazazi, viongozi wa serikali na Jamii kwa
ujumla yameonyesha kuvutiwa na malengo na matokeo tarajiwa ya mradi huo.
Akizungumza
kwa Niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakati wa kuzindua mradi huo Afisa
Tawala wilaya ya Shinyanga Bw. Charles Maugila amesema ujio wa mradi huo katika
Manispaa ya Shinyanga ni wa kufurahiwa kwani mkoa wa Shinyanga kwa ujumla
unakabiliwa na changamoto kubwa ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa
kijinsia na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hususani kwa wasichana na wanawake
wadogo.
“Kumekuwa na miradi mingi inayolenga kukabiliana na ukatili wa kijinsia
na UKIMWI lakini mradi huu ni wa kipekee kwa vile unalenga kuwajengea uwezo wa
kisheria wasichana na wanawake wadogo ambao ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa
kijinsia na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
waweze kuwajibisha jamii kwa kudai huduma bora za afya ya UKIMWI”
Alisema Maugila.
Kwa niaba ya
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bw. Anthony Ndanya
ameitaka Jamii ya Kahama kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika
utekelezaji wa mradi huo ili kuweza kufikia malengo ya mradi huo na kupata
matoke tarajiwa.
Akizungumza
kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Mkurugenzi wa
Fedha na Utawala, Bw. Ezekiel Massanja alisema “kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za
Binadamu Tanzania 2016, ukatili wa kijinsia ukijumuisha ukatili wa majumbani,
ukatili wa kingono, mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na vitendo vingine
vya kikatili kwa watoto na wanawake vimezidi kuongezeka maradufu mbali na
kuwepo kwa sheria zinazolinda kundi hilo. Moja ya matokeo ya changamoto za ukatili
kwa wanawake ni kuambukizwa virusi vya UKIMWI”.
“Sambamba na
ongezeko la vitendo vya kikatili, Jamii inakosa uwezo wa kuwawajibisha
watekelezaji wa vitendo vya kikatili na kushindwa kukabilianan na madhara ya
ukatili wa kijinsia kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria na namna ya kudai
upatikanaji wa huduma bora za afya” – Aliongeza Massanja.
Mradi huu ni
moja ya miradi mingi ya Dreams Innovation Challenge inayotekelezwa nchini.
Mradi umejikita kuwajengea uwezo wasichana wa
miaka 15 hadi 24 na jamii kwa ujumla juu ya masula ya kisheria, afya na ukatili
wa kijinsia.
Mradi unalenga kuwapa uwezo wasichana kuiwajibisha jamii pale haki
zao za msingi zinapokosekana hasa kwenye masuala ya afya ya UKIMWI.
Lengo kuu la
mradi ni kuimarisha uwezo wa jamii kuboresha huduma za afya ya UKIMWI kwa
wasichana na wanawake wadogo kupitia mbinu ya uwezeshaji kisheria na
uwajibikaji kijamii.
Mradi
unalenga kufikia jumla ya wasichana 1000 wenye umri kati ya miaka 15 – 24.
Wasichana 500 Shinyanga na 500 wilayani Kahama.
Wanufaika wengine ni pamoja na
wanaume ambao ni wapenzi wa wasichana hao, wazazi, watoto, vyombo vya sheria,
wahudumu afya pamoja na jamii yote kwa ujumla.
|
No comments:
Post a Comment