Simba yatangaza kikosi cha mauaji 2012/13 - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, August 16, 2012

Simba yatangaza kikosi cha mauaji 2012/13


Ochieng kulia na Akuffo kushoto 
Hapo  jana zoezi la kuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara na timu za vijana ukifikia tamati, mabingwa wa ligi hiyo Simba, wamefunga usajili wao kwa kuwasajili wachezaji wawili wa kimataifa Mghana Danniel Akuffo na Mkenya Pascal Ochieng.


Aidha, Simba inatarajia kupokea mchezaji wa kimataifa kutoka nchini Mali  Abdul Azizi ambaye ataletwa na wakala wa wachezaji Vaier St. Claire na Simba itaangalia jinsi gani itamfanyia mchezaji huyo kwani zoezi limeshafungwa.


Simba ambayo jana iliwatambulisha wachezaji hao wapya kwa waandishi wa habari, imewasilisha pia majina ya Emmanuel Okwi, Mussa Mudde na Felix Mumba Sunzu hivyo kufikisha wachezaji watano wa kimataifa wanaohitajika kusajiliwa kwa mujibu wa kanuni.


Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kwamba, wamemsajili Akuffo kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya wakala wake kuwaeleza kuwa nyota huyo yupo katika mpango wa kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa mwakani.


Alisema wachezaji hao wanatarajiwa kushuka dimbani na kikosi cha Simba kitakachokwaana na AFC Leopards keshokutwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, pia watakuwapo katika mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Azam FC itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Alisema mbali na hao, katika usajili wao wamewasilisha majina ya wachezaji wake Kelvin Yondan aliyesajiliwa Yanga na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ waliomsajili kutoka Azam na kusema kuwa suala lao litamalizwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Mashabiki wa Simba
Yondan ambaye alizua utata baada ya kumwaga wino kuichezea Yanga, huku Simba ikidai kuwa bado ina mkataba naye, jina lake pia limeorodheshwa na watani zao hao katika usajili wa wachezaji watakaoichezea timu hiyo katika msimu wa 20012/13.


Wachezaji wengine waliojumuishwa kwenye usajili wa Simba ni pamoja na Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Nassoro Said Cholo, Amir Maftah, Juma Nyoso, Uhuru Seleman, Haruna Moshi ‘Boban’, Paul Ngalema na Abdallah Juma.


Wengine ni Hamad Waziri Mwinyimani, Salum Kinje, Mrisho Ngassa, Haruna Shamte, Jonas Mkude, Edward Christopher, Shomary Kapombe, Haruni A. Chanongo, Omary Seseme, Hassan Kondo na Kiggi Makasi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad