Baadhi ya maaskofu wakiwa kwenye mkutano huo.
MAASKOFU wa makanisa mbalimbali ya
Kipentekoste nchini wamesema wanatarajia kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi
Nchini, IGP Ernest Mangu ili kulimaliza sakata la Askofu Josephat Gwajima,
kwani kuliendeleza ni kuleta mpasuko wa kidini katika jamii.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana March 30, 2015,jijini Dar es Salaam, Katibu wa
Maaskofu hao, Askofu Dk. Damas Mukassa alisema hakuna sababu ya jambo hilo
kukuzwa, kwani mhusika amemsamehe Askofu Gwajima.
Dk. Mukassa
alisema ni vema Serikali na vyombo vya usalama vikatumia weledi katika
kushughulikia mambo ya kidini na viongozi, kwani yanaweza kusababisha chuki
baina yao.
Alisema
wamekaa na kutafakari kilichomkuta Askofu Gwajima, kwani kiuhalisia afya yake
ilikuwa salama, hivyo wamebaki na shaka, kama vyombo vya usalama si sehemu
salama kama zamani.
Kwa upande
wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Gwajima aliyelazwa katika
Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam amejitokeza hadharani na kusema kuwa,
hakuna njama ya yeye kutoroshwa na wachungaji wake na amekiri kuwa,
bastola iliyokutwa katika begi ni yake na anaimiliki kihalali.
Alisema
iwapo angekuwa na lengo la kutoroka nchini angeondokea Arusha, ambapo
alikuwepo, lakini aliamua kuitikia mwito wa jeshi la Polisi na kurejea Dar es
Salaam.
Askofu
Gwajima alisema baada ya wachungaji wake kupata taarifa ya kuwa,
amefariki ndipo walikwenda kumwona na kumpelekea silaha hiyo ili aweze
kujilinda.
"Kwa
kuwa, palikuwa na mpango huo nikawaambia wachungaji wangu waende nyumbani
kwangu na kuchukua begi lililokuwa chumbani, ambapo ndani yake palikuwa na
baadhi ya nguo na bastola ninayoimiliki kihalali, kwani humo ndani
kulikuwa na nyaraka zilizokuwa zikionesha umiliki na vitu vingine,"
alisema Gwajima.
Alisema
alishangaa kuona Askari wakiwavamia wachungaji wake na kuwafikisha
kituoni kwa kosa la kutaka kumtorosha, jambo ambalo si la kweli.
Gwajima
alisema walipofika hospitalini usiku, wachungaji wake walimfikishia begi na
kuliweka ndani ya chumba, lakini walitokea watu ambao walijitambulisha kuwa, ni
askari na kuomba mzigo ulioingizwa ndani na hapakuwa na ushindani akawapa.
Kuhusu
kuzimia kwake, alitoa taarifa ya kusumbuliwa na kichwa kwa muda mrefu bila ya
kusikilizwa ili apatiwe huduma, ambapo kilichotokea ndiyo hicho walichokiona.
Gwajima
alisema alikuwa akihojiwa na Kamanda wa Upelelezi wa Kanda (ZCO), ambapo
aliendelea kumhoji huku akimpa taarifa ya kuumwa kichwa, lakini hakumsikiliza,
hivyo mpaka anaanguka na kuzimia hakujua kilichoendelea hadi alipofikishwa
hospitalini.
Askofu
Gwajima alisema hana mgogoro wowote na Askofu mwenzake na anampenda,
kilichotokea alikuwa katika kazi yake ya kukemea aliyoyasema.
Kwa upande,
Dk. Willibrod Slaa, mara baada ya kumtembelea Askofu Gwajima hospitalini hapo,
alisema haingilii ugomvi wa Askofu Pengo na Gwajima, bali anachokipinga ni
upotoshaji unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya raia.
Dk. Slaa
alisema polisi waache maneno yao ya kusema mtu anajifanya anaumwa, kwani ni
kitendo ambacho kinaonesha kuwa, halithamini utu wa mtu.
Aidha,
alisema mambo anayofanyiwa Askofu Gwajima hata yeye aliwahi kufanyiwa akiwa
Arusha, baada ya umma kupotoshwa kuwa, alikamatwa na silaha kana kwamba yeye ni
jambazi.
“Nilikamatwa
na jeshi la polisi huko Arusha, ambapo kisheria unapokuwa na silaha
unaisalimisha, nilifanya hivyo na nikaambiwa nijisajili, lakini siku iliyofuata
taarifa ikatolewa kuwa, nimekamatwa na silaha, hivyo inaonesha jinsi gani jeshi
la polisi linavyofanya hila kwa raia," alisema.
Dk. Slaa
alisema mahakama ndiyo itakayotoa ukweli wa jambo hilo kama ilivyotokea katika
kesi ya ugaidi dhidi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakati
fulani.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba alisema kinachoonekana kwa
sasa ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambao unaendelea kufanywa kwa vyombo vya
usalama.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema anatarajia kufanya
mazungumzo na Askofu Gwajima kutokana na kauli yake ili kujua nini kilimsukuma
kutoa kauli hiyo.
Wakati
huohuo, Methusela Gwajima ambaye ni Mwanafamilia amekemea vikali kitendo cha
kutukanwa kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kwamba ni kinyume cha
sheria.
Alisema
kitendo hicho ni cha fedheha, ni kinyume cha sheria ya nchi na kwamba,
alitakiwa kumfuata na kumweleza na si kumtukana matusi makubwa na kumsababishia
aibu kubwa.
Aliongeza,
Gwajima abebe msalaba wake mwenyewe kwa kwenda kuomba msamaha, kwani aliamua
kumchafua kiongozi huyo wa kiroho, na kwamba itamsaidia kurudisha heshima ya
mwanzo aliyokuwa nayo.
Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment