|
Watu wawili Rugonzibwa Mujunangoma na
Theophillo Bwakea wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini
Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya rushwa baada ya kupokea mgao wa Sh.
Milioni 485.1 kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow walizohamishiwa na James
Rugemalira.
Katika kesi
ya kwanza, aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Vizazi na Vifo (Rita)
Mujunangoma ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Sheria Wizara Ardhi, Nyumba
Maendeleo ya Makazi, alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,
Emmilius Mchauru.
Upande wa
Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Leonard Swai akisaidiana na Max Ari, ulidaiwa kuwa Februari
5, mwaka 2014 katika benki ya Mkombozi iliyopo Ilala jijini, mshtakiwa akiwa
Mkuu wa Sheria wa wizara hiyo, alipokea rushwa.
Ilidaiwa
kuwa mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh. Milioni 323.4 kama zawadi kupitia akaunti
yake namba 00120102062001 kutoka kwa Mshauri binafsi wa kimataifa na Mkurugenzi
wa zamani wa IPTL,James Rugemalira baada ya kuwa mjumbe katika menejimenti ya
Rita wakati wa machakato wa kuipitisha IPTL kuiuzia Tanesco umeme.
Ilidaiwa
kuwa mshtakiwa alipokea zawadi hiyo kama ofisa wa muda wa kushughulikia masuala
ya IPTL. Mshtakiwa alikana mashitaka yake.
Swai alidai
kuwa upande wa Jamhuri hauna pingamizi la dhamana na kwamba mahakama ijielekeze
katika hati ya mashitaka fedha anazodaiwa kuchota mshtakiwa.
Hakimu
Mchauru alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kujidhamini kwa Sh.
Milioni 160 taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha.
Pia
wadhamini wawili wanaofanyakazi serikalini watakaosaini hati ya dhamana ya Sh.
Milioni 10 na mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam, bila kibali cha mahakama.
Mshtakiwa
alitimiza baadh ya masharti ya dhamana ambapo hakimu alisema mahakama imempa
dhamana ya muda hadi Januari 16, mwaka huu hati za mali zake zitakapohakikiwa.
Katika kesi
ya pili, aliyekuwa mjumbe wa kitengo cha kuidhinisha Tanesco kununua umeme wa
IPTL, Wizara ya Nishati na Madini, Injinia Bwakea kwa sasa mtumishi wa Wakala
wa Umeme Vijijini(REA), alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Frank
Moshi.
Swai alidai
kuwa Februari 12, mwaka 2014 mshtakiwa akiwa Injia Mkuu wa REA, alipokea rushwa
ya Sh. Milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901 ya Tegeta Escrow kama
zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Rugemalira.
Ilidaiwa
kuwa mshtakiwa alipokea zawadi hiyo baada ya kuwa mjumbe aliyeandaa sera
zinazohusu sekta binafsi kuzalisha na kuuza umeme kwa Tanesco.
Mshtakiwa
alikana mashitaka yake. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi la
dhamana na kwamba upelelezi umekamilika.
Hakimu Moshi
alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili kutoka serikalini au wanaofanyakazi
katika taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 20
kila mmoja. Pia alisema mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam, bila
kibali cha mahakama.
Mshtakiwa
alitimiza masharti ya dhamana na kesi yake itatajwa Januari 26, mwaka
huu.
Leo Januari
14,2015, kuanzia saa 2:00 asubuhi katika viunga vya mahakama ya Kisutu,
watumishi na watu mbalimbali waliingia katika eneo hilo huku kukiwa na
minong’ono kwamba wanaotuhumiwa ufisadi wa Escrow watafikishwa mahakamani hapo.
Pia
waandishi wa habari waligawanyika katika makundi tofauti huku wakijadili na
kutafatuta wadau wao kujua kuhusu ujio wa watuhumiwa hao.
Mapema jana Januari
13,2015,saa 5:42 asubuhi vigogo hao walitinga mahakamani hapo na kwenda
kusomewa mashitaka yao yanayowakabili.
|
No comments:
Post a Comment