RIPOTI MAALUM TANZANIA :-Ununuaji kansa wapamba moto ,Bei huanzia Sh.750 hadi 7,000, Kijiko cha mkorogo Sh. 1,000. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, January 26, 2015

RIPOTI MAALUM TANZANIA :-Ununuaji kansa wapamba moto ,Bei huanzia Sh.750 hadi 7,000, Kijiko cha mkorogo Sh. 1,000.


Kasi ya wananchi kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kansa imeendelea kupamba moto jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini licha ya jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa kila uchao katika kudhibiti hali hiyo, imefahamika.

Wananchi hao, hasa kina mama na wasanii wa fani mbalimbali wakiwamo wa filamu, muziki wa dansi na bongofleva, wamekuwa vinara wa kununua vipodozi vyenye viambata vya sumu na kujipaka mwilini kwa nia ya kujiongezea urembo na utanashati lakini bila kujua kuwa wanajiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kansa, hasa ya ngozi na ini.  

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kuanzia wiki iliyopita umebaini kuwa watu wanaojiweka katika hatari hiyo hununua vipodozi hivyo kwa kati ya Sh. 750 hadi Sh. 7,000 kwa chupa kutegemeana na ujazo na pia aina ya kipodozi na chapa yake (brand) huku mkorogo wenye mchanganyiko wa vipodozi hivyo, maarufu kama 'manjano' au 'kijiko special' ukiuzwa kwa Sh. 1,000 kwa kipimo cha kijiko kimoja kikubwa cha chai.

Kadhalika, imebainika kuwapo kwa utitiri wa vipodozi vyenye sumu katika maduka na masoko mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kwingineko nchini huku wauzaji na wateja wao wakionekana kupuuza au kutofahamu lolote juu ya ukweli kwamba bidhaa hizo zinahatarisha afya yao na vilevile wanajiweka katika hatari ya kukumbana na mkono wa dola kwani kuuza au kutumia bidhaa hizo kunakiuka sheria za nchi.

Katika maeneo kama ya masoko ya Tandika, Buguruni, Manzese, Magomeni, eneo la Mbagala Rangi Tatu na kwingineko nchini, vipodozi hivyo huuzwa bila kificho na baadhi huuzwa kwa kuwekwa kwenye viroba na kupangwa ardhini huku vikipigiwa debe na wauzaji kama ilivyo kwa biashara ya nguo za mitumba.

Katika tovuti yao (http://www.tfda.or.tz) na pia kupitia kampeni mbalimbali za kuelimisha umma, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imekuwa ikivitaja viambata vyenye sumu kwenye vipodozi kuwa ni pamoja ni Bithionol, Hexachlorophene, Mercury, Vinyl chloride, Zirconium, Halogenated salicylanilides (di-, tri- metabromsalan and tetrachlorosalicynilide), Chloroquinone, Steroids, Chloroform, Chlofluorocarbon na Methyelene chloride.

Aidha, TFDA imetaja vipodozi zaidi ya 100 vyenye viambata vyenye sumu. Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya vipodozi hivyo ndivyo vilivyojaa sokoni na kwenye baadhi ya maduka, vikiwamo vya Mekako, Rico, Princess Cream, Butone Cream, Extra Clear Cream, Viva Super Lemon Cream, Ultra Skin Tone Cream. 

Vingine ni Clere Extra, Top Lemon, Diproson, sabuni aina ya Jaribu, Riki, Amira na pia cream kama Movate, Demovate na Oranvate.

HATARI ILIYOPO.

Vipodozi hivi vyenye viambata vya sumu husababisha pia ngozi kuharibika na kuifanya kuwa nyepesi, hivyo kusababisha miale hatari ya jua (UV-B) kupenya kirahisi kwenye ngozi na kusababisha kansa.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Kuzuia Udhibiti wa Kansa katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, Dk. Maguhwa Stephano, ameiambia NIPASHE kuwa vipodozi vyenye viambata vya sumu vina madhara makubwa na wananchi wanapaswa kujua kuwa kuvitumia ni kujihatarishia uhai kwani magonjwa ya kansa ni ya hatari na kutibu kwake huligharimu taifa fedha nyingi.

Kwa mujibu wa Dk. Maguhwa, gharama za kuwatibu wagonjwa wa kansa ni kubwa na hivyo serikali hufanya kazi ya ziada ya kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika kila mwaka ili kuwatibu wananchi wake; rasilimali ambayo pengine inaweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo ikiwa wananchi watajiepusha kutumia vipodozi hatari wanavyovinunua kwa fedha kidogo lakini wakijiweka katika hatari kubwa kiafya.

Anasema tiba kubwa wanazotoa kwa wagonjwa wa kansa huwa ni za aina tatu, ambazo ni kwa kutumia mionzi, drip na pia kwa dawa maalum (chemotherapy). Na matibabu yote hayo huhitaji gharama kwa kila mgonjwa. 

"Kwa kawaida, gharama ya kipimo cha wagonjwa wa kansa (Biops) ni Sh. 50,000 hadi 80,000 kulingana na mahala anakokwenda mgonjwa. 

Gharama nyingine ni mionzi huwa kati ya Sh. 800,000 hadi 1,200,000. Katika hali ya kawaida, wastani wa gharama za kuwatibu wagonjwa wa kansa ya ngozi kwa mwaka huwa ni zaidi ya 2,000,000. Isipokuwa, lazima ifahamike kuwa gharama kuwa juu au chini hutegemeana na stage ya ugonjwa wenyewe na mahala ulipo katika mwili,” anasema.

  
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu takriban milioni 3 hupata kansa kila mwaka, huku milioni moja kati yao wakiwa ni watu wanaopata saratani ya ngozi.

TFDA WANENA.

Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudencia Simwanza anasema vipodozi vya sumu ni janga kubwa linalopaswa kudhibitiwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya mamlaka yao na wadau wengine, hasa wananchi wenyewe.

Anasema tafiti mbalimbali zimethibitisha kuwa watumiaji wa vipodozi vyenye sumu wanajiweka katika hatari kubwa ya kupata maradhi ya kansa na pia athari nyingine nyingi za kiafya.

Anataja madhara mengine mbali na kansa ya ngozi kuwa ni kansa ya ini, kina mama wajawazito kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo, shinikizo la damu na pia uwezekano wa kina mama kuota ndevu pindi wanapotumia vipodozi vyenye sumu kwa muda mrefu.

Kuhusiana na udhibiti, Simwanza anasema kuwa mamlaka yao hujitahidi kufanya ukaguzi wa kustukiza kila mara kwenye maduka na maeneo mengine yauzayo vipodozi, kushirikiana na mamlaka nyingine kama jeshi la polisi katika kufanya ukaguzi maeneo ya mpakani mwa nchi na pia kufanya kampeni mbalimbali za kuelimisha umma.

Anaongeza kuwa kasi ya uingizaji wa vipodozi vyenye sumu nchini ni kubwa lakini wameendelea kufanya jitihada za kutosha za kudhibiti. Hadi kufikia sasa, wamekuwa wakikamata na kuteketeza wastani wa tani 54 za vipodozi vyenye viambata hivyo kila mwaka, thamani yake ikiwa ni takriban Sh. milioni 354.

Anasema Sheria ya Chakula, Dawa  na Vipodozi ya mwaka 2014 inawapa mamlaka ya kukamata na kuteketeza vipodozi vyenye viambata vya sumu.-"Sheria inapiga marufuku viambato vyenye sumu na vipodozi vyenye viambato viletavyo madhara... ni katika vifungu 87(i) na 90," anasema Simwanza.

Hata hivyo, anasema kuna changamoto kadhaa za kisheria kwani kadri inavyoonekana sasa, adhabu kwa wahusika zinaonekana zimepitwa na wakati na kwamba hazitishi wahalifu kiasi cha kutosha.  "Watuhumiwa wanaokutwa na vipodozi visivyofaa hunyang'anywa vipodozi hivyo na hulipia gharama ya kuviteketeza. Sambamba na hilo, wengine hufikishwa mahakamani. Kesi 10 zilifikishwa mahakamani."

Anasema matumizi ya vipodozi visivyofaa yatakoma mara moja pindi jamii ikibadilika na kwamba,  TFDA inaamini kwa kuendelea kutoa elimu, lengo hilo litatimizwa kwani kidogokidogo jamii itakuwa ikibadilijka.

KWINGINEKO AFRIKA.

Katika makala kuhusiana na vipodozi vyenye vimabata vya sumu iliyochapishwa na mtandao wa BBC Januari 1, 2013, ilielezwa kuwa matumizi ya vipodozi hivyo ni janga kubwa barani Afrika. Kwa mfano, madaktari wa ngazi katika hospitali moja jijini Dakar, Senegal walikaririwa wakisema kuwa hupokea takriban kina mama 200 kila wiki wanaokuwa wameathiriwa vibaya ngozi zao baada ya kutumia vipodozi vyenye sumu kwa nia ya kubadili rangi za ngozi zao.

Mtandao wa voices in bioethics unakariri taarifa za utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoonyesha kuwa nchi za Mali, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Togo ndizo zinazoongoza kwa matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu barani Afrika. Katika utafiti huo, inaelezwa kuwa wanawake ndiyo vinara kwani kila uchao, asilimia 77 ya wanawake wa Nigeria hutumia vipodozi hivyo, wakifuatiwa na Togo (59), Afrika Kusini (35), Senegal (27) na Mali (25).


Chanzo:- NIPASHE

UNGANANASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad