Pichani ni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Mcheche Masaju.
Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri
ya Tanzania unatarajia kuanza kesho Januari 27,2015 mjini Dodoma hadi Februari
7, mwaka huu.
Mkutano huo
utaambatana na kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Mcheche Masaju, baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni baada
ya kujiuzulu kwa Jaji Frederick Werema kutokana na kuhusishwa na kashfa ya
uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
Benki Kuu Tanzania (BoT).
Katika
mkutano huo, Wabunge watajadili miswada mitatu ya serikali ambayo ni pamoja na
wa sheria ya usimamizi wa kodi wa mwaka 2014, ambao utapigiwa kura tu, wa
sheria ya takwimu wa mwaka 2013 ambao utasomwa kwa mara ya tatu na ule wa
marekebisho ya sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2014.
Pamoja na
miswada hiyo, Bunge pia litajadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali zilizowasilishwa katika mkutano wa 15 wa Bunge kuhusu hesabu
zilizokaguliwa za serikali Kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma kwa
mwaka 2012/2013 na serikali kutakiwa kuzitolea majibu kwa baadhi ya hoja.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa
Kimataifa kutoka Ofisi Ndogo za Bunge, katika mkutano huo, kamati za
Bunge pia zitapewa nafasi ya kuwasilisha taarifa za mwaka ikiwamo Kamati Teule
ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera zinazohusu ardhi,
kilimo, mifugo, maji na uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi
ya ardhi.
Vilevile
maswali ya kawaida 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa, maswali 15 kwa siku
na 10 kwa Alhamisi.
Mkutano wa
19 wa Bunge unatarajia kufanyika katikati ya Machi hadi mwanzoni mwa
Aprili huku ule wa 20 wa Bunge la Bajeti mwanzoni Mei hadi Juni 30,
mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment