Kidato cha tano majanga , Shule za serikali zakosa wanafunzi 10,000. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, July 11, 2013

Kidato cha tano majanga , Shule za serikali zakosa wanafunzi 10,000.



Matokeo mabaya waliyoyapata wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 yamesababisha shule za sekondari za serikali kukosa wanafunzi 10,000 waliopaswa kuanza masomo Julai 29, mwaka huu.





Kutokana na upungufu huo serikali imeamua kusitisha usajili wa shule za sekondari za serikali na imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuboresha shule zilizopo kwa kuhakikisha zinakuwa na miundombinu bora kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.



Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ndiye aliyetangaza upungufu huo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi.




Mwaka jana tulisajili shule mbili za kidato cha tano na sita, ambazo ni Miono iliyopo Bagamoyo na Tandahimba ya Mtwara… tumekubaliana mwaka huu hatutaongeza shule nyingine, tuboreshe zilizopo kwanza,” alisema Mulugo.



Mulugo alisema kutokana na uchache huo wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na kidato cha tano, hasa wa masomo ya Sayansi ya Jamii, serikali imeamua kutoongeza idadi ya shule za sekondari kama inavyofanya kila mara kulingana na idadi ya wanafunzi wenye sifa za kujiunga na shule husika.



Mulugo alisema watahiniwa 34,213 kati ya 431,650 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na watakaokwenda kwenye shule 207 zilizopo hapa nchini.



Mulugo alisema idadi ya waliofaulu inajumuisha wanaokwenda kwenye vyuo vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.



Kwa mujibu wa Mulugo, watahiniwa binafsi 193 walifaulu na kati yao watahiniwa 76 waliokuwa na sifa za kwenda kidato cha tano hawakuchaguliwa, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo umri zaidi ya miaka 25 huku mmoja wao akiwa si raia.



Waliochaguliwa ni 34,213, kati yao wanaokwenda kidato cha tano ni 33,683 na ufundi ni 530, ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 8.9 ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa mwaka 2012.



Kati ya hao wanaokwenda sekondari wasichana ni 10,300 na wavulana ni 23,383, hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 2,824, sawa na asilimia 9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012,” alisema Mulugo.



Kuhusu ufaulu wa masomo ya sayansi, naibu waziri huyo alisema wavulana wameongezeka, ambapo kati ya 23,383 waliochukua masomo ya sayansi ni 13,708 sawa na asilimia 58.62 wakati waliobaki walichaguliwa kwenye msomo ya sayansi ya jamii.




Waziri Shukuru Kawambwa.
Mulugo alisema kati ya wasichana 10,300 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wasichana 5,038 sawa na asilimia 48.91 walichaguliwa kwenye masomo ya sayansi huku 5,262 sawa na asilimia 51.09 wakipelekwa kwenye masomo ya sayansi ya jamii.



Kwa upande wa vyuo vya ufundi, Mulugo alisema waliofaulu ni 530, kati yao wavulana ni 416 na wasichana ni 114, na kusema idadi ya wasichana imeongezeka kutoka 47 mwaka jana, sawa na asilimia 142.55.



Akifafanua zaidi, alisema kuanzia mwaka huu wamerejesha utaratibu wa wanafunzi wanaoingia kidato cha tano wataanza masomo wiki ya tatu ya Julai, badala ya Aprili kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita.



Chanzo:Tanzania Daima.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad