Baadhi
ya askari wa JKT na JWTZ katika sherehe hizo Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam leo(Julai
10,2013) katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT).
|
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE
KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA JESHI LA KUJENGA TAIFA
UWANJA WA UHURU, 10 JULAI, 2013, DAR ES SALAAM
Mheshimi
wa Shamsi Vuai Nahodha (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa;
Mheshimiwa
Gril Haskel, Balozi wa Israel;
Meja
Jenerali Raphael Muhuga,Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa,
Makamanda,
Wapiganaji na Vijana;
Wageni
Waalikwa;
Ndugu
Wananchi;
Mabibi
na Mabwana;
Pongezi.
Nakushukuru
sana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha
na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Raphael Muhuga kwa
kunishirikisha kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhai wa Jeshi la
Kujenga Taifa.
Nawapongeza sana kwa
maandalizi mazuri ya sherehe hizi ambazo hakika zimefana sana. Gwaride lilikuwa zuri na tumeburudika vya
kutosha kutoka vikundi vya ngoma, ngonjera na nyimbo.
Kwa
niaba yangu, ya Serikali na ya Watanzania wote nawapongeza kwa dhati Maafisa
Wakuu, Maafisa Wadogo, wapiganaji na vijana wa JKT popote pale walipo kwa
kusherehekea Jubilei ya Dhahabu ya uhai wa JKT.
Mnastahili kuwa na furaha na kusherehekea kama tulivyoshuhudia sote.
Historia ya JKT.
Ndugu
Wananchi;
Miaka 50 iliyopita, tarehe kama ya leo, yaani tarehe 10 Julai,
1963 Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa rasmi.
Huu ulikuwa ni utekelezaji wa Azimio la Kikao cha Baraza la Mawaziri
kilichofanyika tarehe 19 Aprili, 1963 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika. Wazo
la kuanzishwa kwa JKT lilitokana na mapendekezo ya busara ya Mkutano Mkuu wa
Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika
African National Union (TANU Youth League), uliofanyika mkoani Tabora mwaka
1958. Wazo hili lilitolewa na Katibu
Mkuu wa TANU Youth League wakati ule Ndugu Joseph Nyerere ambaye sasa ni
marehemu.
Lengo kuu la kutaka kuundwa
kwa JKT lilikuwa ni kuwandaa vijana kuwa raia wema, wawe na moyo wa uzalendo,
na wawe tayari kulitumikia taifa lao kwa nguvu na uwezo wao wote.
Ndugu
Wananchi;
Jeshi la
Kujenga Taifa lilianza na Vijana 11
kutoka Wilaya 11 nchini. Hao ndio walikuwa wa kwanza kupata mafunzo
katika Kambi ya JKT Mgulani, Jijini Dar es Salaam. Vijana hao walikuwa ni Makatibu wa Umoja wa
Vijana wa TANU na wengine walimu.
Niruhusuni niwatambue watu hao kuwa ni Bi Zainabu Kiango, Bw. Sebastian
Chale, Bw. Peter Lwegarulira, Bw. Rupho Kamba, Bw. Hashim Ngaliwason, Bw. John
Ndimugangwo, Bw. Said Desai, Bw. Dismas Msilu (Brigedia Mstaafu), Bw. Athumani
Msonge (Brigedia Jenerali Mstaafu), Bw. Reginald Mitande na Bw. Eslei
Mwakyambiki.
Kati ya hao 11, walio
hai ni Bi Zainabu Kiango na Brig. Jenerali Dismass Msillu ambao wapo nasi siku
ya leo. Waliosalia wameshatangulia mbele
ya haki. Mwenyezi Mungu awarehemu. Kundi la pili liliwajumuisha Bi. M. Mhando,
Bw. E. Simkone, Bw. Mwanimlele (Asst Master) Bw. AA Moyo (Asst Master) ambao
walijiunga na kupata mafunzo ya uongozi.
Sheria Iliyoanzisha JKT
Ndugu
Wananchi;
Mwaka 1964, Bunge lilitunga Sheria ya Kuanzisha JKT iliyoupa nguvu
ya kisheria uamuzi wa mwaka 1963 wa Baraza la Mawaziri wa kuanzishwa kwa Jeshi
hilo. Kwa mujibu wa Sheria ile, kujiunga
na JKT ilikuwa jambo la kujitolea kwa mapenzi ya mtu. Lakini mwaka 1966, Sheria
hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuanzisha utaratibu wa kujiunga na JKT kwa
mujibu wa Sheria.
Utaratibu huu uliwahusu vijana waliohitimu vyuo vikuu, vyuo vya
elimu ya juu, kidato cha sita na waliomaliza kidato cha nne ambao wamepata
mafunzo kwenye vyuo vya taaluma mbalimbali kama vile ualimu, uganga, uuguzi na
kadhalika. Mkurugenzi wa JKT
aliwezeshwa kisheria kuwaita vijana hao kujiunga na JKT. Mwezi Julai 1967, kikundi cha kwanza cha
vijana wasomi 64 kilijiunga na JKT
katika Operesheni Azimio.
Katika
kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa,
viongozi na wasomi wengine waliohitimu zamani waliamua kujiunga na mafunzo ya
JKT. Mwezi Januari, 1968, kwa mfano,
aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Rashid Kawawa, aliyekuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Aboud Jumbe, aliyekuwa Spika
wa Bunge Chifu Adam Sapi Mkwawa pamoja na baadhi ya Wabunge na viongozi
mbalimbali wa Chama na Serikali walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa.
Wote walikuwa katika kambi ya
Ruvu ambapo walipatiwa mafunzo ya uongozi.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka 1975 JKT iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania na hivyo kuwa sehemu kamili ya JWTZ.
Kuanzia wakati ule, Maafisa na Askari wa JKT wakawa ni wa JWTZ na
kutambulika kwa vyeo vya JWTZ.
Jeshi la
Kujenga Taifa liliendelea na majukumu yake ya kutoa mafunzo kwa vijana wa
kujitolea na wa mujibu wa sheria. Hata
hivyo, mambo mawili ya msingi yalisisitizwa au kuongezwa katika majukumu ya
JKT.
Kwanza kwamba, kuwa Divisheni ya
Uzalishaji ya JWTZ yenye dhamana ya kulipatia Jeshi mahitaji yake ya chakula,
mavazi na mengineyo. Pili, kwamba JKT
ndipo mahali pa kutolea mafunzo ya awali ya kijeshi na kwamba JWTZ itaajiri
kutokana na wanaohitimu JKT.
Katika dhamira ya kutimiza wajibu wa kwanza kwa ufanisi, mwaka
1982 Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) liliundwa. Shabaha kuu ilikuwa ni kuwa na chombo
madhubuti cha kupanga, kusimamia, kuratibu na kutekeleza majukumu ya uzalishaji
mali na kiuchumi katika JKT kazi ambayo shirika linaendelea kuifanya hadi sasa.
Kusitishwa kwa Mafunzo ya
JKT
Ndugu
Wananchi
Tunapoangalia
nyuma, katika historia ya miaka 50 ya kuzaliwa na uhai wa JKT tunaona wazi kuwa
yamepatikana mafanikio makubwa. Tena ni
mafanikio ya kutia moyo na kujivunia.
Ninaposema hivyo, napenda nisieleweke vibaya kuwa sitambui ukweli kwamba
kulikuwepo vipindi vigumu vyenye changamoto za namna mbalimbali.
Zilikuwepo changamoto kubwa na ndogo na
zilizokuwa ngumu na nyepesi kuzipatia ufumbuzi.
Aidha, natambua kuwa bado zipo changamoto kadhaa tunazoendelea
kukabiliana nazo. Jambo la msingi na la
faraja ni kwamba pamoja na changamoto hii tumefanikiwa sana.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
upande wa mafunzo kwa vijana, kwa mfano, zaidi ya vijana 305,625 wamepitia JKT na kupatiwa mafunzo ya kijeshi na ya stadi
mbalimbali za maisha katika fani na nyanja mbalimbali. Tangu mwaka 1963 mpaka sasa yameshapita
makundi (kwa jina maarufu Operesheni) 102.
Bahati
mbaya kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyoikabili nchi yetu kuanzia nusu ya
pili ya miaka ya 1970 na kuwa mbaya zaidi miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990,
hali ya utoaji wa mafunzo kwa vijana katika JKT iliathirika sana. Upatikanaji wa huduma na mahitaji kwa ajili
ya mafunzo na kuendesha kambi na JKT kwa jumla ukawa mgumu.
Pengine
ni vyema nikaeleza kuwa kupanda sana kwa bei ya mafuta duniani, kuanguka kwa
bei za mazao yetu tunayouza nje na gharama kubwa ya vita dhidi ya Idi Amin wa
Uganda ndivyo vilivyosababisha uchumi wa nchi yetu kutetereka. Hali hii ilipunguza sana uwezo wa Serikali
kutimiza majukumu yake ya msingi katika sekta, karibu zote nchini.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
sababu hiyo, kwa upande wa JKT mwaka 1993, Serikali ililazimika kusimamisha
mafunzo kwa vijana wa kujitolea na mwaka 1994 ilifanyika hivyo kwa vijana wa
mujibu wa Sheria. Kwa kweli baada ya
mwaka 1994 shughuli za msingi za JKT zilidorora sana na kubakiza za kulinda
kambi na zile Shirika la Uchumi (SUMAJKT).
Hata hizo nazo hazikuwa zinafanyika kwa kiwango kikubwa wala hazikuwa
kwa ufanisi mkubwa kwa sababu ya kutokupata fedha za kutosha kutoka
Serikalini. Fedha za uendeshaji wa
shughuli zake zilikuwa kidogo.
Ndugu
Wananchi;
Kuifufua
JKT ilikuwa ni moja ya mambo niliyoyapa kipaumbele cha juu nilichojiwekea
katika mipango ya kazi baada ya kupewa heshima kubwa ya kuliongoza taifa letu
Desemba 21, 2005. Mtakumbuka kuwa katika
hotuba yangu ya kuzindua Bunge tarehe 30 Desemba, 2005, nilipozungumzia kufanya
kila tuwezalo kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana, nilikuwa
nazungumzia kufufua na kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na kuwepo kwa
shule za kitaifa hasa za sekondari.
Ni
ukweli ulio wazi kwamba JKT imefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa utaifa
na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia Jeshi hilo.
Hapa ni mahali ambapo vijana wa rangi zote,
makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi
kama ndugu wa nchi moja. Hakuna chombo
chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo.
Kwangu mimi na wenzangu katika Serikali
ninayoiongoza kufufua mafunzo ya vijana wa kujitolea na mujibu wa sheria
lilikuwa suala kubwa na muhimu sana kulitekeleza.
Ndugu
Wananchi;
Bahati
nzuri sikuwa peke yangu mwenye fikira na matamanio hayo.
Watu wengi ndani ya Serikali, nje ya Serikali
na miongoni mwa raia na Bungeni walikuwa wanaunga mkono mawazo hayo. Sababu kubwa ni kuwa athari za kusimamishwa
mafunzo ya JKT ziliwagusa wengi na ndiyo maana kumekuwepo na madai ya kutaka
mafunzo yarudishwe.
Kule
Bungeni kauli yangu kuhusu JKT iligeuka kuwa deni kubwa kwangu na kwa
Serikali. Madai ya kutaka Serikali
irejeshe mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yalikuwa yanajitokeza mara kwa
mara na mwangi wake ulikuwa unaongezeka ukali kila mwaka.
Nafurahi kwamba hatimaye tarehe 26 Machi,
2013 tulifanikiwa kutimiza dhamira na ahadi yetu nilipozindua kuanza upya kwa
mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu. Kundi
la kwanza limemaliza mafunzo yake na la pili limeshafika katika makambi na
tayari wameanza mafunzo.
Kama
ilivyokuwa mwaka 1964 JKT ilipoanza, na mwaka 1968 baada ya mafunzo ya mujibu
wa Sheria kuanzishwa, viongozi wa kitaifa waliongoza kwa mfano; safari hii
Wabunge wetu alionesha. Mwaka huu
Wabunge 22 wamefanya na kumaliza
mafunzo ya uongozi. Baadhi yao wako nasi
siku ya leo. Niruhusuni nirudie kutoa
pongezi zangu za dhati kwao kwa kuwa viongozi wa mfano.
Ndugu
Wananchi;
Taarifa
nilizonazo ni kuwa wamefanya na kumaliza mafunzo yao vizuri. Walikuwa na nidhamu nzuri, utii na moyo wa
kujituma. Wamemaliza wakiwa ni askari
wakakamavu na wenye mtazamo mpya na bora zaidi kuhusu masuala ya utaifa,
uzalendo na mustakabali wa taifa letu na watu wake.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
upande wa shughuli za kiuchumi zinazofanywa na JKT tuliazimia kuwa, tutafanya
kila tuwezalo kuimarisha SUMAJKT.
Tumefanya mambo kadhaa kwa ajili hiyo na tumekuwa tunapata mafanikio
ingawaje bado tunayo safari ndefu ya kulijenga shirika hili mpaka liwe bora kwa
shughuli lizifanyazo. Naamini tutafika
pale tunapopatarajia.
Tuliamua
kutoa upendeleo maalum kwa JKT kwa kutoa shughuli na miradi kadhaa ya Serikali
waitekeleze wao.
Kwa mfano, ujenzi wa
nyumba na majengo kadhaa ya Serikali pamoja na ujenzi wa barabara, mabwawa ya
maji na miradi ya kilimo cha umwagiliaji na kadhalika. Tumewapa JKT kazi ya kuzalisha mbegu bora kwa
wakulima. Vile vile, Serikali imechukua
mkopo wa dola za Marekani milioni 40
kutoka Serikali ya India uliotumika kununua matrekta 1,846 kutoka Serikali ya India na kuipa SUMAJKT kuuza kwa wakulima
kama biashara yao.
Hivi
sasa mchakato unaandaliwa wa kupata mkopo mwingine wa dola za Marekani milioni 92 kwa ajili hiyo. Tumefanya yote hayo kwa
makusudi mazima ya kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kuwa na shirika
lililoimara na linalotekeleza kwa ufanisi majukumu yake. Halikadhalika itawezesha JKT kudumisha sifa
yake nzuri katika kilimo, ufugaji, uvuvi na ujenzi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu, Wakuu wa JKT kumi,
waliotangulia pamoja na Meja Jenerali Muhuga aliyepo sasa. Tunawapongeza kwa utumishi wao uliotukuka na
moyo wao wa upendo kwa nchi yetu na watu wake.
Mafanikio haya tunayojivunia leo yametokana na juhudi kubwa za viongozi
hawa wakishirikiana na maafisa, askari na wafanyakazi raia katika kubuni na
kusimamia utekelezaji wa shughuli za JKT.
Mimi
na Watanzania wenzangu wote hatuna neno lingine zuri la kuwaonesha upendo wetu
na shukrani zetu zaidi ya kusema asanteni sana.
Tunatambua na kuthamini mchango wenu.
Tutauenzi daima.
Changamoto na Dira
Mheshimiwa
Waziri;
Pamoja
na mafanikio ya kutia moyo, naelewa kuwa bado safari iliyo mbele yetu ni ndefu
na imejawa na changamoto nyingi ambazo hatuna budi kuzipatia majawabu.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na
uhaba wa makazi ya maafisa na askari, upungufu wa wataalamu katika miradi
mbalimbali, upungufu wa vitendea kazi na vyombo vya usafiri. Baadhi ya makambi hayana miundombinu mizuri
ya kutoa kwa uhakika huduma muhimu kama vile maji, umeme na kadhalika.
Napenda
kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na JKT katika kutafuta njia
mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo. Tutaendelea kuongeza bajeti ya JKT kila mwaka
na kuidhamini SUMAJKT ipate mikopo ya kutekeleza miradi yake na shughuli
zake. Tutaendelea kutoa upendeleo kwa
Jeshi na JKT katika kutekeleza baadhi ya miradi ya Serikali.
Hata hivyo, nawaomba mzingatie ubora wa kazi
muifanyayo ili kulinda heshima ya JKT na
kutulinda sisi tunaoamua kuwapa upendeleo.
Ndugu
Wananchi;
Tunafanya
haya kwa dhamira moja kubwa ya kutaka kulifufua Jeshi la Kujenga Taifa na
kulifikisha mahali panapostahili na kuwa chombo madhubuti cha kutumainiwa na
taifa.
Nataka JKT liwe Jeshi la kisasa
zaidi, linaloenda na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya
juu. Tunapenda mafunzo yanayotolewa kwa
vijana wanaojiunga na JKT yaendeshwe vizuri.
Tunataka JKT itoe wazalendo wa kweli, wanaothamini utaifa, umoja na
mshikamano wa Watanzania. Vijana
wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea.
Tunataka JKT izalishe askari walio hodari na
wanaoweza kulinda nchi yao kwa ujasiri mkubwa.
Aidha, wanapoajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama na kwingineko,
idhihirishe wazi kuwa vijana waliopitia JKT ni bora. Ni watu walioiva, wa kuaminika na
kutumainiwa.
Hali
kadhalika, kwa wale wanaorudi uraiani kufanya shughuli nyingine wawe ni watu
waliokamilika na wenye uwezo wa kusimama wenyewe na kuendesha maisha yao. Kinachotakiwa ni kuwepo kwa utaratibu mzuri
kuwasaidia wanaojiajiri waweze kuanzisha shughuli za kuwaingizia mapato kwa
kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata.
Namna ya kuwawezesha vijana wanaomaliza JKT waanze maisha ya kujitegemea
ni jambo ambalo hatuna budi kulitafakari.
Lakini leteni mapendekezo yenu tuone namna ya kuyatekeleza.
Ndugu
Wananchi;
Mpaka
sasa bado JKT haijafanikiwa ipasavyo kuwa divisheni ya uzalishaji ya JWTZ kama
ilivyotarajiwa. Bado haizalishi chakula
cha kutosheleza mahitaji ya JWTZ. Aidha,
bado hawajaweza kutosheleza mahitaji mengine ya JWTZ kama vile mavazi na
kadhalika.
Sasa wakati umefika wa
kujipanga vizuri kutekeleza jukumu hilo.
JKT itumie sherehe hizi kufunga nadhiri ya kupanga na kuanza safari ya
dhati ya kufanya hivyo. Lakini,
wasiishie hapo tu, JKT iweke nia ya kuzalisha ziada ya kuuza nchini na hata nje
ya nchi. Inawezekana, jipangeni vizuri
ili mtimize wajibu wenu.
Rai kwa Makamanda wa JKT
Ndugu
Mkuu wa JKT, Makamanda, Maafisa na Askari;
Ni
jambo linalotia faraja kubwa kwamba sote tunatambua kuwa katika miaka 50
iliyopita Jeshi la Kujenga Taifa limepata mafanikio ya kutia moyo ingawaje
safari ilikuwa na vikwazo mbalimbali.
Hata huko mbele muendako hatutegemei kuwa mambo yatakuwa rahisi,
changamoto mbalimbali zitaendelea kujitokeza.
Hivyo basi, kinachohitajika ni kuendelea kuwa wabunifu kufanya kazi ya
ziada, tena kwa bidii zaidi, maarifa na moyo wa kujituma na kujitolea. Hizi ni sifa ambazo mnazo, hivyo naomba
muendelee kuzidumisha na kuziendeleza.
Endeleeni
kuwa chuo mahiri cha kuwafunda vijana wetu wawe na moyo wa utaifa, uzalendo,
kujituma na kupenda kufanya kazi. Wawe
raia wema na wawe tayari kutoa mchango stahiki katika kujenga taifa lao. JKT inategemewa kuendelea kuwa kitovu cha
shughuli za uzalishaji mali, mafunzo ya stadi za kazi na ujasiriamali kwa
vijana wetu. Endeleeni kuimarisha JKT.
Nawaomba
mtimize wajibu wenu huo kwa ukamilifu.
Msituangushe. Nawaomba endeleeni
kuwa na moyo wa kuchapa kazi, muwe
makini na waaminifu katika utendaji wenu wa kazi za kila siku.
Tafadhali zingatieni sana viapo vyenu vya
utumishi jeshini kwa kila ngazi ya uongozi.
Muwe na nidhamu siku zote kama mwanajeshi anavyotakiwa kuwa. Mkifanya hivyo, nina imani kuwa katika miaka
michache ijayo JKT itapiga hatua kubwa ya maendeleo. Taifa litanufaika sana.
Shukrani kwa Israel
Ndugu
Wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitatambua na kuwashukuru marafiki zetu wa Israel. Nchi ya Israel ndiyo iliyotupatia wakufunzi
wa kwanza waliotusaidia katika kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, walitoa mafunzo kwa viongozi wetu
kadhaa waasisi wa JKT nchini Israel.
Serikali ya Israel imewakilishwa hapa leo na Balozi wake nchini
Mheshimiwa Gril Haskel. Naomba Balozi
atufikishie salamu zetu nyingi za shukrani kwa Rais Shimon Peres, Waziri Mkuu
Benjamin Netanyahu na watu wote wa Israel kwa mchango wao muhimu walioutoa
katika kuanzisha na kujenga Jeshi la Kujenga Taifa. Hatasahau kamwe.
Mwisho
Ndugu
Wananchi;
Mwisho,
nawashukuru, kwa mara nyingine tena, Mheshimiwa Waziri Shamsi Nahodha na Meja
Jenerali Muhuga kwa kunialika.
Nawashukuru wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa vyama vya
siasa kwa kuja kwa wingi kushiriki katika sherehe za siku ya leo.
Na, kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi
wote waliotembelea maonesho ya shughuli zinazofanywa na JKT. Mmejionea wenyewe na kusikia faida za
kuwepo kwa JKT. Basi tuendelee kuliunga
mkono Jeshi letu, lipate mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment