Kinana
ambaye amekuwa Meneja wa Kampeni za mgombea urais wa CCM tangu mwaka 1995
ulipoanza uchaguzi wa vyama vingi, alisema kwamba baada ya kutumikia chama
katika nyadhifa za juu kwa robo karne sasa, ameamua kupumzika ili kuwaachia
vijana waendelee kukijenga chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika.
“Nimekuwa Mjumbe wa NEC kwa miaka 25, bila
shaka muda huu unatosha, kwani wanaCCM wamenipa heshima ya kuwa katika vikao
vya juu vya chama kwa robo karne. Sasa ni wakati wa kung’atuka, nimetoa mchango
kwa kadri nilivyoweza katika vikao mbalimbali na katika shughuli nyingi,”
alisema.
Alisema
anaamini kuachana kwake na siasa hakutakuwa na madhara kwa chama chake, kwani
CCM ina hazina kubwa ya viongozi ambao wana sifa na wanaweza kuongoza chama
hicho kuelekea Uchaguzi wa 2015.
“Uongozi ni kupokezana vijiti. Wako wanaCCM
wazuri, walio na uwezo mkubwa na sifa za kutosha kuongoza. Nawashukuru wanaCCM
na viongozi kwa heshima waliyonipa wakati wote huu,” alisema Kinana ambaye
alikuwa Meneja wa Kampeni wa Rais Benjamin Mkapa kwa vipindi viwili na Rais
Jakaya Kikwete kwa vipindi viwili vya uchaguzi.
Kinana
alisema anajivunia kufanya kazi na marais wote wa Tanzania kuanzia Mwalimu
Julius Nyerere hadi Rais Kikwete kwa uadilifu mkubwa na kuheshimiana.
”Ushauri wangu katika vikao umekuwa ukiheshimika
sana. Nimekuwa nikiheshimiwa na uongozi wote wa CCM na hata wapinzani nao
tunaheshimiana. Nimesimamia kampeni za kistaarabu na ambazo zimeleta ushindi
mkubwa kwa CCM tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi,” alisema.
Kinana
ambaye pia alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA),
ameshauri vijana ndani ya CCM watangulize masilahi ya taifa mbele na wasikilize
wananchi. Ni muhimu washikamane, wabuni mikakati ya kusaidia kukuza uchumi kwa
haraka zaidi na kuendeleza umoja na undugu wetu,” alisema.
|
Abdulrahaman
Kinana anang’atuka ni baada ya kuwa mjumbe NEC,Kamati kuu kwa miaka 25.
|
Ushauri wa
viongozi wapya CCM Kinana alishauri viongozi wapya ambao wanatarajiwa
kuchaguliwa ndani ya chama chake, iwapo wataona upungufu wake wausahihishe. “Ni
matumaini yangu kuwa watakaopata uongozi wataona upungufu na watasahihisha
makosa yangu,” alisema. Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015, Kinana aliwaasa viongozi
wasiwaze nani anafaa kuwa mgombea urais bali washughulikie kero za wananchi.
“Bado tuna kazi kubwa ya kutekeleza Ilani.
Tusiwasumbue Watanzania kuwa ni nani anafaa kuwa Rais bali tushughulikie
matatizo yao. Kwa sasa ajenda ya CCM ni kutekeleza ahadi zetu katika sekta zote
siyo kutafuta nani atakuwa Rais 2015," alisema na kuongeza:
"Hata
wapinzani wawaeleze Watanzania yale ambao wamedhamiria kutekeleza. Kueleza
upungufu wa CCM ni mtaji mdogo kwa wapinzani, ajenda kubwa ni watafanya nini?
Hapa bado wana kazi kubwa. Wanapoona upungufu wasisite kutusema,” Kinana ambaye
ana shahada ya uzamili katika utawala na masuala ya sera kutoka Chuo Kikuu cha
Harvad nchini Marekani, alisema anatarajia kufundisha na kusoma Shahada ya
Uzamivu (PhD) katika moja ya vyuo vikuu vya hapa nchini.
“Baada ya kustaafu kuna mambo mawili ambayo
natarajia kufanya. La kwanza ni kuona kama naweza kufundisha. Pili kusoma
katika mojawapo ya vyuo vikuu vyetu,” alisema.
Mbali na nyadhifa zilizotajwa huko juu, Kinana
ametumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa muda mrefu na kupanda cheo
hadi kufikia Kanali. Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Arusha
Mjini.
Nape alisema
Kinana ni miongoni mwa wanasiasa waadilifu wa CCM ambao wamekitumikia chama kwa
muda mrefu na kwa uaminifu wa hali ya juu. Ni kweli hajagombea, lakini
kutokugombea kwake hakujafungwa milango kwa CCM kumtumia au kutumia uzoefu wake
pale watakapomhitaji.
Alisema "Kwa mfano Mwenyekiti wa CCM ana
nafasi alizopewa kikatiba kuteua wajumbe wa NEC, huwezi kujua anaweza akamwona
anafaa na akamteua,"
Chanzo:
www.mwananchi.co.tz





No comments:
Post a Comment