RC Kagera Aagiza Watumishi Wawili Kusimamishwa Kazi Na Watano Kuchunguzwa kwa Ubadhilifu wa Fedha za Serikali – Biharamulo. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, August 17, 2018

RC Kagera Aagiza Watumishi Wawili Kusimamishwa Kazi Na Watano Kuchunguzwa kwa Ubadhilifu wa Fedha za Serikali – Biharamulo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Pichani.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aiagiza Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kuwasimamisha kazi mara moja watumishi wawili kupisha uchunguzi na wengine watano kuchunguzwa juu ya upotevu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 690 zilizokusanywa katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani na fedha hizo hazikuwasilishwa Benki kwenye akaunti ya Halmashauri kama kanuni, taratibu na sheria za fedha zinavyoelekeza.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa maagizo hayo leo Agosti 17, 2018 katika kikao Maalum cha Kamati Fedha, Uongozi na Mipango ambacho kililenga kupokea taarifa ya uchunguzi wa awali na ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato ya ndani iliyoundwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera CP Diwani Athuman baada ya kupata taarifa kutoka katika vyanzo vyake vya ndani juu ya upotevu wa fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.
Watumishi walioagizwa kusimamishwa kupisha uchunguzi na ikithibitika wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ni Bw. Salanga Mahendeka (Mhasibu wa Mapato) ambaye alibainika kuwa na hoja ya mashaka ya fedha zaidi ya shilingi milioni 276 ikiwa ni pamoja na: Kutosimamia utaratibu wa mapato ya fedha yaliyoondolewa katika mfumo wa mapato bila idhini ya Afisa Masuuli, Kusababisha madeni ya wakusanyaji kutotambuliwa kwa kutofanya usuluhishi wa miamala ya mapato katika mashine za kukusanyia mapato, Kukusanya fedha bila kuziwasilisha benki.

Mtumishi wa pili aliyeagizwa Mamlaka ya Nidhamu kumsimamisha kazi ili kupisha TAKUKURU kufanya uchunguzi juu yake ni Bw. Emmanuel Maleo (Afisa Ushirika) ambaye alibainika kuchukua fedha taslimu kwa wafanyabiashara kwa nyakati tofauti mwezi Februari hadi Machi, 2018 bila kuziwasilisha Benki na kushindwa kuhitimisha mchakato wa kuwapatia leseni wafanyabiashara hadi Mei, 2018.

Aidha, Watumishi wengine watano walioagizwa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na Mamlaka zao za Nidhamu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu endapo itathibitika tuhuma zao ni za kweli ni pamoja na: Bw. Alexander Bashaula (Mweka Hazina) ambaye ni mkuu wa idara ya fedha ambaye alifanya uzembe katika kuwasimamia ipasavyo watumishi walioko chini yake kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu pia na kushindwa kumsahuri ipasavyo Afisa Masuuli kuhusu masuala ya fedha.

Pili ni Bi Beatrice P. Garusya (Afisa Biashara) ambaye hakutoa leseni za biashara kwa wafanyabiashara waliolipia na kusababisha malalmiko yasiyo ya lazima kwa wafanyabiashara hao .

Tatu ni Bw. Rogers H. Simkoko (Afisa Tehama) aliyefanya miamala ya kihasibu badala ya kufanya kazi yake ya ufundi kwenye mfumo wa kukusanya mapato na kukiuka taratibu kwa kutoa haki kwa Afisa mmoja kukamilisha miamala peke yake.

Wengine ni Bi Saphina Malimba (Mtunza Fedha) ambaye hakuwasilisha benki kiasi cha shilingi milioni 32, 098,800/= alizokusanya kwa kutumia mashine ya kukusanya mapato. 

Mwisho ni Bi Specioza Mikole (Mhasibu) aliyekuwa Mhasibu na kuhamishiwa TARURA na aliondoka na mashine ya kukusanyia mapato bila kuikabidhi ambayo ilikuwa na madeni makubwa ya fedha na fedha alizokuwa amekusanya zinatiliwa mashaka matumizi yake pia haijulikani kama fedha hizo ziliwasilishwa benki.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kumrejesha Mtumishi huyo na kumtaka akabidhi mashine hiyo ifikapo saa 10:00 jioni Agosti 17, 2018 ili usuluhishi ufanyike na endapo kuna deni atakiwe kulipa mara moja pia alimwagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kufuatilia na kuchukua hatua pia hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti aliagiza wakusanyaji 59 wa mapato ya ndani kwa kutumia mashine za kielektroniki waliokuwa hawajawasilisha mapato benki ya jumla ya shilingi milioni 427,130,100/= hadi ufuatiliaji unafanyika ifikapo Jumatatu Agosti 20, 2018 wawe wamewasilisha mashine zao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili zifanyiwe usuluhishi chini ya usimami wa Katibu Tawala Mkoa na kiasi kitakachothibitika kudaiwa kipelekwe benki mara moja. 

Pia Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wenye madeni hayo iwachukulie hatua za kinidhamu.

Aidha, vibanda 25 vya Soko la Kabindi vilivyobainishwa kwenye taarifa ya uchunguzi kuwa havikuwa na mikataba ya kukodishwa Mkuu wa Mkoa Gaguti aliagiza Halmashauri kuandaa mikataba hiyo mara moja kulingana na bei ya soko ya kukodi vibanda vya biashara kulingana na na mazingira vilipo pia viboreshwe kwa kuwekewa umeme ili kiwe chanzo cha mapato cha Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.

Maamuzi hayo yalifikiwa na Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya Katibu Tawala Msaidizi Serikali za Mitaa Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera Bw. David Lyamboko Kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wa awali uliofanyika chini ya uongozi wake baada ya Katibu Tawala Mkoa kuunda Kamati hiyo na kuipa adidu za rejea ili kufanya uchunguzi na Kamati hiyo ilianza kazi yake Mei 28, 2018 na kuikamilisha kazi hiyo Juni 18, 2018.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa kagera CP Diwan Athuman katika kikao hicho maalum aliwakumbusha wviongozi na Wakuu wa Idara ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kujitathimini na kujitafakari kama wanamsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Maguli kufanikisha adhima ya kuwahudumia wananchi kwa uadilifu.

Pia aliwaasa watumishi popote walipo katika Halmashauri za Wilaya kujitafakari kwa dhati juu ya utendajikazi wao, kuwa na mtazamo wa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano nini wanakilenga katika kutekeleza majukumu yao, na tatu ni kushirikiana kuwa na upendo pia na kuwa wakweli.

 Aidha, kila mtumishi alitakiwa kujitafakari kulinagana na Kaulimbiu ya Mkoa wa Kagera Isemayo Kagera Kazi, Amani na Maendeleo na ajipime kama anatimiza wajibu kulingana na kaulimbiu hiyo.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad