Mwenyekiti
wa Bodi ya Ushauri ya TEMESA Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri,
akipanda ngazi kukagua ujenzi wa kivuko kipya cha MV. MWANZA, nyuma yake ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transaport Boat Yard Ltd
(inayojenga kivuko hicho) Salehe Songoro, akifuatiwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Ufundi na Umeme( TEMESA) Dkt. Mussa Iddi Mgwatu.
|
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme( TEMESA) Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (wa kwanza
kulia) akiongea na waandishi wa habari baada ya ukaguzi wa kivuko kipya cha MV.
MWANZA kulia kwake mwenye miwani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TEMESA
Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi Mabula Mashauri.
Na.
Theresia Mwami - TEMESA
Serikali
kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), imeahidi kukamilika kwa ujenzi
kivuko kipya cha Kigongo Busisi (MV. MWANZA) unaofanywa kampuni ya kizalendo ya
Songoro Marine Transport Boatyard ifikapo mwezi Juni 2018.
Kivuko hicho
kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 250, ambazo ni sawa na kubeba magari 36
na abiria 1,000 kwa wakati mmoja.
Akizungumza
na waandishi wa habari, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa kivuko hicho, uliofanywa
na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TEMESA mapema Jana May 16,2018,
Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Iddi Mgwatu alisema ujenzi huo unagharimu
jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 8.9 na ulianza rasmi tarehe 28/08/2017
na kwamba tayari umekamilika kwa asilimia 95.
“Namuagiza
Mkandarasi kuhakikisha kuwa ujenzi wa kivuko hiki unakamilika kwa aslimia 100
ifikapo mwezi Juni,2018 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba ili kuweza kuboresha
zaidi huduma ya uvushaji abiria na mizigo yao katika eneo Kigongo – Busisi”,
aliongeza Dkt. Mgwatu.
Aliongeza
kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha MV. MWANZA kutafanya eneo la Kigongo
Busisi kuboresha zaidi huduma za uvushaji kwani kwa sasa tayari kuna Kivuko cha
MV. Misungwi ambacho pia kina tani 250, MV. Sengerema tani 170 na MV. Sabasaba
tani 85.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya TEMESA Brigedia Jenerali Mstaafu Mhandisi
Mabula Mashauri alisema kuwa, serikali inalengo la kuboresha hali ya maisha ya
wananchi, kwa kuwawekea miundombinu salama ya vivuko, ili kuhakikisha wanapata
huduma bora na salama wakati wote.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo
kutatoa nafasi ya ukarabati mkubwa wa vivuko vingine vinavyotoa huduma kati ya
Kigongo na Busisi kufanyika kwa awamu.
Aidha alitumia nafasi hiyo pia
kuwapongeza TEMESA kwa kazi nzuri ya usimamizi wa ujenzi wa kivuko hicho, kwa
kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mkataba wa ujenzi
wake.
Nae
Mkurugenzi Kampuni ya Songoro Marine Transaport Boat Yard Ltd, Major Songoro,
aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini kampuni hiyo na kuahidi kuimaliza
kazi hiyo kwa haraka na ustadi mkubwa.
|
No comments:
Post a Comment