Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba Akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya Kukitembelea Kiwanda cha AMIAMZA.
Changamoto Kubwa Sita Alizozitatua Dkt. Tizeba Kuhusu Mfumo Mpya Utakaotumika Kununua Kahawa ya Wakulima Msimu wa Mwaka Huu 2018.
Kwanza; Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera namna ya kupata fedha ya kukusanyia Kahawa za Wakulima na kuzipeleka mnadani kwenye soko la dunia. Waziri akijibu changamoto hiyo Dkt. Tizeba alisema kuwa tayari Serikali inavisimamia vyama vya KCU 1990 LTD, KDCU LTD na NGARA FARMERS kupata fedha kwa ajili ya malipo ya awali ya wakulima na mwanzoni mwa Mwezi Mei 2018 Vyama vyote vitakuwa na fedha ya kutosha kukusanyia kahawa ya wakulima.
Pili; Namna gani viwanda vyote vya binafsi na vya Vyama vya Ushirika vitakoboa kahawa. Katika Kikao hicho cha wadau iliamuliwa kuwa Vyama vya Ushirika vilivyoruhusiwa kukusanya kahawa ya wakulima vitoe tenda katika viwanda vilivyopo maeneo husika vikoboe kahawa ili kuiwahisha mnadani. Aidha, viwanda vitavyotumika kukoboa kahawa hiyo ni vile ambavyo vina viwango na si vile vinavyokata kahawa na mwisho kuonekana haina ubora.
Tatu; Dhana ya Vyama vya Ushirika kununua kahawa ya Wakulima. Pamoja na Waziri Dkt. Tizeba kulitolea ufafanuzi jambo hilo lakini pia Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania Bw. Tito Haule alitoa ufafanuzi kuwa Vyama vya Ushirika havitakiwi kufanya biashara kwa wananchama wake bali jukumu lake ni kukusanya kahawa kwa wakulima na kuzipeleka mnadani katika soko la dunia ili mkulima apate bei iliyo nzuri.
Nne; Bei elekezi iliyotangazwa na Chama Kikuu cha Ushirika Kagera Co operative Union 1990 LTD (KDCU 1990 LTD) katika mkutano wake Mkuu kwa wakulima. Waziri Dkt. Tizeba alifafanua kuwa chama hicho hakikutakiwa kutangaza bei elekezi kwasababu hakitanunua kahawa ya wakulima bali jukumu lake ni kukusanya kahawa ya wakulima. Aidha, wakulima watalipwa fedha ya awali ambayo itakuwa kidogo ili mara baada ya kahawa kupata bei halisi mkulima alipwe fedha nyingi na kumnufaisha.
Tano; Namna bora ya kudhibiti utorashaji wa kahawa maarufu ‘Obutura’. Kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Deodatus Kinawilo alikikumbusha kikao kuwa Mkuu wa Mkoa tayari alishatoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kuhakikisha hakuna kahawa inauzwa kwa njia za Magendo au Obutura.
Agizo, Katika hatua nyingine mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wadau kutoka Wilaya ya Karagwe kuhusu baadhi ya vyama ambavyo vilisajiliwa na vinavyoendesha ununuzi wa kahawa holela Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba alimuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania kuvifutia usajili vyama hivyo mara moja tangu tarehe 26.04.2018 Vyama hivyo ni Nguvumali, Nkwenda Amcoss na Mavuno na kuagiza kuwa viache mara moja kujishughulisha na masuala ya kununua kahawa.
Sita; Gharama za uendedeshaji wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera. Katika Mkoa wa Kagera wakulima walikuwa hawapati malipo ya pili takribani miaka mitano iliyopita kutokana na Vyama vya Ushirika kuwa na gharama kubwa za uendeshaji jambo ambalo lilipelekea Serikali kuanzisha mfumo mpya wa Vyama hivyo kukusanya kahawa za wakuli na si kununua kwasababu fedha ya wakulima ilikuwa inaenda kwenye gharama za uedeshaji wa Vyama.
|
Waziri wa Kilimo Dkt. Tizeba Akiongea na Wadau wa Kahawa Mkoa wa Kagera Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Katika kulishughulikia suala hilo Dkt. Tizeba alimagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania kuhakikisha analeta mara moja wataalamu wa hesabu kuzikagua gharama za uendeshaji wa Vyama hivyo na kuhakikisha zinakuwa gharama halisi na ndogo ili zisimuumize mkulima kwa kukatwa fedha yake ili msimu ukianza kila kitu kiwe katika mpangilio mzuri.
Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo Dkt. Tizeba alikitembelea kiwanda cha Kahawa cha AMIAMZA kilichopo Kibuye Manispaa ya Bukoba na kuongea na mmiliki wa Kiwanda hicho Bw. Amir Amza ambaye alimuomba Waziri Dkt. Tizeba kuona uwezekano wa kuondoa Ushuru wa Halmashauri (Cess) ili kahawa ya kiwanda hicho iweze kushindana katika soko la dunia.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo Waziri alisema kuwa Serikali inaishi kwa kutegemea kodi kujenga miundombinu kama barabara kwahiyo kodi hizo haziwezi kufutwa isipokuwa Serikali ilipunguza kiwango cha cha Kodi hiyo ya Halmashauri kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.
|
No comments:
Post a Comment