Mabosi wa Halmashauri za Monduli, Karagwe, Biharamulo kikaangoni Upotevu wa milioni 171.8 za Miradi ya Maji - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, April 19, 2018

Mabosi wa Halmashauri za Monduli, Karagwe, Biharamulo kikaangoni Upotevu wa milioni 171.8 za Miradi ya Maji

Maji ni uhai.
 
Ni uhai kwasababu  yanabeba dhana nzima ya mwanadamu yeyote kuishi na kufanya shughuli zingine za maendeleo. Pia maji ni uhai kwasababu yanagusa sekta zote za uzalishaji, popote utakapokwenda utahitaji maji. 

Hiyo ndiyo thamani ya maji.

Ni dhahiri kuwa jambo lolote linalofanyika kwa nia ya kuvuruga au kuhalibu mfumo wa upatikanaji wa maji safi na salama, linalenga kuuawa uhai wa binadamu. Kuanzia kwenye uhalibifu wa mazingira, vyanzo vya maji, ukosefu wa rasilimali fedha na watu kutekeleza miradi ya maji hadi kukosekana kwa utashi wa kisiasa kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika.

Katika makala hii tunajadili matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo katika baadhi ya halmashauri za wilaya nchini ambazo zimetumia vibaya fedha na kuwahatarishia uhai wakazi wa maeneo yao.

Halmashauri hizo ni Monduli, Karagwe na Biharamulo ambazo  zimekiuka makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maji na kusababisha milioni 171.8 kutumika kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa.

Halmashauri hizo 3 katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2017 zilikuwa zinatekeleza miradi ya maji chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP). 

Fedha za mfuko wa WSDP hutolewa na nchi wahisani au mashirika ya kimataifa kuhakikisha wananchi hasa maeneo ya vijijini wanapata maji safi na salama.

Wahisani hao wanaongozwa na dhamira kuu; maji ni uhai na binadamu popote alipo ni lazima aypate ili aweze kuishi. 

Lakini wapo baadhi ya watendaji katika halmshauri hizo kwa kujua au kutokujua wanahujumu miradi inayofadhiliwa na wahisani hao.
Tabia hiyo inatajwa kuwa kikwazo kwa wafadhili kuendelea kuwasaidia wananchi kupata maji kwasababu kukosekana kwa utashi wa kisiasa  kwa baadhi ya watendaji ambao kwa namna moja ama nyingine wanatumia tatizo la maji kama mtaji wa kujinufaisha kisiasa na kupata nafasi za uongozi Serikalini.

Kulingana na Mkataba wa makubaliano (MoU) wa uanzishaji wa Mfuko wa WSDP aya ya 9.2.2 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013 inaeleza kuwa, “Serikali imekubali kusamehe kodi zote zilizowekwa moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja kwenye matumizi yote yanayostahili ya bidhaa, kazi na huduma za kifedha chini ya WSDP”.

Lakini halmashauri za  wilaya za Monduli mkoani Arusha; Karagwe na Biharamulo mkoani Kagera zilikiuka kifungo hicho na kutoza kodi yenye thamani sh. Milioni 171.8 kwenye miradi minne ya maji iliyofadhiliwa na mfuko wa WSDP ambayo haikupaswa kukatwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 2017 inaeleza kuwa katika halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilibainika mikataba miwili ambayo ilitozwa kodi yenye thamani ya sh. Milioni 87.7 kutoka kwenye miradi ya maji ambayo haikustahili kulipa kodi katika wilaya hiyo.

Nimebaini mikataba miwili, Na. LGA/004/2016/17/RWSSP/W/14 na Na. LGA/004/2016/17/RWSSP/W/10 katika Halmashauri ya Wilaya Monduli Mkoani Arusha, ambapo kiasi cha VAT (ongezeko la thamani) Sh. 87,765,679 kililipwa kwa ajili ya miradi ya maji iliyosamehewa kodi”, imeeleza ripoti hiyo ambayo ilitolewa na CAG, Prof. Mussa Assad wiki iliyopita.

Halmashauri za Karagwe na Biharamulo nazo zilifuata mkondo ule ule wa Monduli kwa kutoza kodi ya sh. Milioni 84.035 kwenye miradi miwili ya maji iliyokuwa ikitekelezwa na mfuko wa WSDP katika wilaya zao.

Taarifa ya CAG inafafanua kuwa “Nimebaini pia mikataba miwili katika Halmashauri za Wilaya Karagwe na Biharamulo yenye namba LGA/033/W/2016/17/W/NT/07 na LGA/032/2016-2017/HQ/WSDP/W/76 LOT 03 ambapo kodi ya ongezeko la thamani (VAT) yenye thamani ya Sh. 84,035,685 ilijumuishwa katika gharama ya miradi ya maji iliyosamehewa kodi.

Kwa vyovyote vile katika miradi hiyo mitatu kuna harufu ya ufisadi, kama miradi hiyo haikutakiwa kulipa kodi fedha hizo zimeenda wapi?. 

Na kama serikali ilipokea hizo fedha ilitumia vigezo gani kwasababu masharti ya mkataba ambao Serikali ilisaini hayaruhusu kodi ijumuishwe kwenye gharama za mradi wa maji.

Kiasi cha milioni 171.8 kukatwa kodi huenda kimewakosesha wananchi katika maeneo mengine kupata huduma ya maji. 

Kwa mafano fedha hiyo ingetumika vizuri ingeweza kujenga miradi mingine ya kusambaza maji katika halmashauri hizo na kuwapunguzia wananchi tatizo la upatikanaji wa maji.

Nini kifanyike…

CAG katika ripoti yake ameonyesha kusikitika na mwenendo  huo wa baadhi ya watendaji wa halmashauri kutozingatia maadili ya kazi zao. 

Amebainisha kuwa tabia hiyo ikiendelea inaweza kuwakatisha tamaa wafadhili kuendelea kutoa fedha za misaada.

Kwa maoni yangu, malipo ya VAT kwa miradi iliyosamehewa kodi yanapunguza uwezo wa Halmashauri kugharamia miradi mingine. Aidha, kutofuata MoU kunakatisha tamaa nia za wafadhili kuendelea kutoa ruzuku katika miradi mingine.”, amesema CAG, Prof. Assad katika ripoti yake.

Kwa kutambua kuwa fedha zilizopotea ni nyingi, Makatibu Tawala wa halmashauri za wilaya hizo 3 wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kitendo chao cha kukwamisha upatikanaji wa huduma muhimu ya maji kwa wananchi.

Napendekeza kwamba, katika siku zijazo Uongozi wa Halmashauri ufuate mkataba wa makubaliano uliosainiwa. Aidha, Afisa Masuuli achukuliwe hatua kwa ulipaji wa VAT katika miradi iliyosamehewa kodi,” ameshauri CAG, Prof. Assad.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad