Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa
huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa Waasisi wa Taifa na
Mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea leo tarehe
02 Februari, 2018 saa 10:30 alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini
Dar es Salaam.
Mzee
Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya
kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam tarehe 22
Desemba, 2017.
Mhe. Rais
Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa
katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu
wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa
mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.
“Mzee
Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi
kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake
uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa
wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na
maarifa na kuwa na nidhamu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kufuatia
msiba huu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM,
ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na
moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Mwenyezi
Mungu ailaze roho ya Marehemu Kingunge Ngombale Mwiru mahali pema peponi,
Amina.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
02 Februari,
2018
No comments:
Post a Comment