Rais Kikwete-Tanzania. |
SERIKALI ya
Tanzania imeipa onyo kali nchi ya Rwanda ikiitaka isijaribu kuota ndoto za
kuishambulia kijeshi, vinginevyo itajibu mapigo kwa nguvu zote na kuhakikisha
kuwa imeichakaza.
Kauli hiyo
ya kwanza nzito imetolewa jana(Julai10,2013) na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa
Kimataifa kufuatia taarifa ya matamshi makali yanayodaiwa kutolewa na Rais Paul
Kagame wa Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na kutishia kuishambulia
Tanzania.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa
Ally, alisema ingawa Serikali
ya Tanzania hadi sasa inajua haina ugomvi wowote na Rwanda, lakini amekiri
kuwapo kwa kile alichokiita ‘kupishana lugha’ kwa Rais Jakaya Kikwete na Paul
Kagame.
Mkumbwa
alikiri Serikali ya Tanzania kunasa matamshi yanayodaiwa kutolewa na Rais
Kagame katika moja ya hotuba zake aliyoitoa Juni 30,2013, nchini kwake wakati
akihutubia katika hafla moja ya vijana.
Kwa mujibu
wa hotuba hiyo, ambayo kwa wiki sasa imesambazwa katika baadhi ya mitandao ya
kijamii, Kagame anadaiwa kusikika akitoa matamshi ya vitisho dhidi ya Rais
Kikwete, kwamba anamsubiri katika wakati aujuao na kumchapa.
Rais Kagame-Rwanda. |
Baadhi ya
maneno yanayodaiwa Rais Kagame aliwaambia vijana waliokutana katika mkutano wao
uliojulikana kama ‘Youth Konnect’ na kufadhiliwa na mke wake, Janet Kagame,
yanasema: “Huyu mtu mliyemsikia akiwa upande wa Interahamwe na FDLR na
akashauri majadiliano….majadiliano?”
Aidha,
Kagame anadaiwa kusema kuwa hatakuwa tayari kujadili jambo hilo, isipokuwa
atamsubiri Rais Kikwete sehemu muafaka na ‘kumtandika’.
“Sitapoteza
muda wangu kumjibu Kikwete, inajulikana maana kuna mahali hataweza
kuvuka…haiwezekani,” alikaririwa akisema Rais Kagame, akilenga kumtisha Rais
Kikwete.
Mbali na
Kagame, baadhi ya viongozi kadhaa wa serikali ya Rwanda wamekuwa wakimshambulia
Rais Kikwete wakimpachika majina ya kejeli ya; “Rais mhurumia magaidi, wauaji
wa kimbari, mkorofi na mwenye dharau.”
Mkumbwa hata
hivyo alisema Serikali ya Tanzania haina sababu ya kuingia katika vita na
Rwanda, kwa sababu tu ya ushauri alioutoa Rais Kikwete wa kuitaka ikutane na
wapinzani wake wanaoishi ndani ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC), kujadiliana kuhusu amani ya nchi za Maziwa Makuu.
Alisema
msimamo wa Tanzania utabaki kuwa uleule wa kuitaka nchi hiyo ikubali kukaa meza
moja na wapinzani wake, ili kumaliza migogoro inayoendelea katika nchi hizo za
maziwa makuu, ambao unaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na SADC.
“Unajua
mgogoro wa DRC na Rwanda hauwezi kumalizika bila ya nchi hizo kukaa meza moja
na wapinzani wao ili kupata suluhu ya kudumu,” alisema Mkumbwa.
Aliwataka
Watanzania kuwa watulivu na kuendelea na kazi zao kama kawaida, kwani serikali
yao iko makini katika kulinda mipaka yake.
Chanzo cha Mzozo.
Msuguano
baina ya nchi hizi mbili ulianza siku chache tu baada ya kumalizika kwa kikao
cha viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, chini ya uenyekiti wa Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni.
Rais Kikwete
wakati akimtaarifu Rais Museveni kile walichokuwa wamekijadili katika kikao
hicho kwa vile aliketi kwa muda kwa kuwa alichelewa kuwasili, alisema ni vema
serikali za Rwanda na Uganda zifungue mlango wa mazungumzo na waasi wao na
akaanza kutaja majina ya vikundi vya uasi vya nchi hiyo vilivyopo nchini DRC.
Habari
zinasema kauli ya Rais Kikwete iliungwa mkono na Rais Museveni akisema: “Bila
mazungumzo hatutafika popote pale”.
Waziri Bernard Membe. |
Hata hivyo,
matamshi hayo yalijibiwa kwa ukali na serikali ya Rwanda, kiasi cha kumlazimu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutoa tamko
bungeni.
Kwa kauli
yake, Membe alisema serikali ilikuwa imeshangazwa na shutuma hizo za Rwanda
kwani halikuwa jambo baya kutoa ushauri uliolenga kuleta mapatano na kuepusha
umwagaji zaidi wa damu wa wananchi.
Akaongeza
kuwa, ilikuwa ni wajibu wa Serikali ya Rwanda kuupokea ama kuukataa, na wala si
kutoa maneno ya kejeli na vitisho.
Kauli ya Mbunge Zitto.
Mbunge Zitto Kabwe. |
Akizungumzia
kauli hiyo ya vitisho, mwanasiasa machachari hapa nchini na Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, alisema ushauri wa
Rais Kikwete kwa Rwanda ulikuwa wa busara mno na akashangaa kuona nchi hiyo
jirani ikitoa vitisho, kejeli, dharau na ukosefu wa adabu kwa Kikwete.
Katika moja
ya tamshi lake alilolitoa jana katika mitandano ya kijamii, Zitto ambaye ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) alisema Marekani wanaongea na waasi wa
kundi la Taliban, hivyo hakuna dhambi kwa Rwanda pia kufanya hivyo.
“Pia kama
hutaki ushauri si unakataa tu, sasa kuanza kurushiana maneno ya nini tena?
Hutaki ushauri basi. Maneno ya kila siku ya nini? Tangu Kikwete amesema kule
Addis, hajasema tena. Membe (waziri) akajibu Dodoma Tanzania haijasema tena.
Kigali inasema mambo haya kila siku kwa ajili ya nini ?.
“Taliban na
Al Qaeda si wale wale? Wale watoto waliozaliwa mwaka 1994 na wakimbizi wa
Kihutu waliopo Kongo nao ni wauaji? Tufikiri vizuri mambo haya.
Kuna
‘genociders’ wasakwe, wakamatwe wahukumiwe. Kuna watu wana haki kabisa ya kutaka
kushiriki kwenye siasa za Rwanda na wanazuiwa, wameshika silaha. Hawa lazima
wakae meza moja wakubaliane,” alisema Zitto.
Mwanasiasa
huyu alisema kwa sasa serikali za nchi hizo mbili zinatakiwa kuingia katika
vita ya kupambana na kuondoa umasikini wa watu wake na si vita ya mtutu wa
bunduki.
“Busara
itumike kwa viongozi ‘neutral’ kama Uhuru Kenyatta kuwaweka pamoja Kagame na
Kikwete wamalize tofauti zao. Haya maneno hayana maana yoyote,” alisema.
Alisema vita
haitamuumiza Rais Kagame wala Rais Kikwete na familia zao, bali itaumiza
wananchi wa kawaida wa mikoa ya Kagera na Kigoma na mikoa ya mpakani ya Rwanda.
“Vita
itaturudisha nyuma sana kwenye juhudi za maendeleo. Vita itazima harakati za
kujenga demokrasia nchini. Busara
itumike tu,” alisema Zitto.
Chanzo:Tanzania Daima.
KAGAME AJARIBU TUMSHIKISHE ADABU
ReplyDelete