Asiilimia
2.7 ya wafungwa na mahabusu waliopimwa virusi vya Ukimwi (VVU) kwa mwaka
2016/17 wamegundulika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.
Matokeo hayo
yamebainika baada ya Jeshi la Magereza kuwapima Ukimwi wafungwa na mahabusu
34,793. Kati yao, wanawake ni 1,451 na wanaume ni 33,342.
Akiwasilisha
Bungeni mjini Dodoma February 7, 2018 taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ukimwi, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasmin Bunga, alisema wafungwa
waliokutwa na maambukizi ni 953 (asilimia 2.7), akibainisha kuwa wanaume ni 818
na wanawake 135.
Alisema
kamati yake pia ilielezwa kuwa jeshi hilo katika mwaka 2015/16 waliwapima
wafungwa na mahabusu 8,287 na kati yao, waliokutwa na maambukizi ya Ukimwi ni
376, sawa na asilimia 4.5.
"Kamati
ilipokea taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya VVU magerezani pamoja na
upatikanaji wa kinga na tiba ya magonjwa nyemelezi," alisema na kufafanua
zaidi:
"Katika
mahojiano hayo, kamati ilielezwa kuwa Jeshi la Magereza lina jukumu la
kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama ilivyo
kwenye jamii nyingine."
Vilevile,
alieleza kuwa kamati yake ilielezwa uwapo wa msongamano wa wafungwa na mahabusu
unaoathiri huduma bora kwa wafungwa, akibainisha kuwa kwa sasa kuna wafungwa na
mahabusu 39,312 wakati uwezo wa magereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu
29,552.
Kutokana na
hiyo, Bunga alisema kamati yake inashauri serikali itumie adhabu mbadala kwa
makosa madogo kwa kuwa kufanya hivyo kutapunguza msongamano, gharama kwa
serikali na uwezekano wa kuambukizana magonjwa ya homa ya ini, Ukimwi na kifua
kikuu.
Alisema
kamati yake pia ilitaka kutolewa elimu ya mara kwa mara ili wafungwa na
mahabusu wapate uelewa namna ya kupambana na janga la Ukimwi pamoja na wapatiwe
chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa hatari ya ini.
"Shughuli
zozote zinazohusu dawa za kulevya na Ukimwi magerezani, uongozi wa magereza
uwahusishe waratibu wa Ukimwi na dawa za kulevya wa mikoa na wilaya ili
kubadilishana uzoefu na elimu," alisema.
Kiongozi
huyo wa kamati pia alisema wamebaini kuna upungufu wa dawa aina ya Septrine
ambazo ni muhimu kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Kutokana na
changamoto hiyo, alisema kamati yake inaishauri serikali kuhakikisha dawa hizo
zinazotumika kupambana na magonjwa nyemelezi, zinapatikana kwa wingi na
ziingizwe katika orodha ya dawa za ARVs ambazo wanapewa WAVIU ili kufubaza
makali ya VVU na kuepusha magonjwa nyemelezi.
Bunga pia
alisema kamati yake imebaini kampeni za mwitikio wa masuala yanayohusiana na VVU
na Ukimwi ni kama zimekufa na hivyo watu sasa wanafanya ngono zembe bila hofu.
Alisema
ukimya huu umesababisha watu kujisahau na hivyo kufanya ngono zembe, hali
ambayo inaweza kuleta mfumuko mkubwa wa maambukizi mapya ya VVU.
"Kamati
inashauri serikali kuwa na mikakati kuhakikisha kamati za kudhibiti Ukimwi
katika kila ngazi zinafanya kazi ipasavyo," alisema.
No comments:
Post a Comment