Waziri Mkuu
wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa
amesema kuanzia Machi mosi, 2017 Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti
za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.
“Tumekaa
na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza Pombe waziweke katika ukubwa
unaokubalika. “Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za
msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia
tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”
Ametoa kauli
hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 16, 2017) wakati akizumgumza na maelfu ya
wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili
ya ziara yake mkoani Manyara.
Amesema
agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa
Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
“Tutawakamata
wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna mirungi,
cocaine na heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa
za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale waliolegealegea, kisha
tuwapime,” alisisitiza.
Akifafanua
suala la uwekezaji kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe ulioandikwa
kwenye mabango, Waziri Mkuu alisema katika eneo hilo zimetengwa ekari 500 kwa
ajili ya EPZA ili kujenga miundombinu mbalimbali.
“Hilo
eneo ni la uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka makubwa
(malls). Sote tunafahamu kuwa Tanzania hivi sasa inaweka msisitizo juu ya
ujenzi wa viwanda. Pale tunataka tuwe na viwanda vya nyama, vya kushona
nguo na kuchakata madini ya Tanzanite ili kjongeza thamani,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema kama
kuna mtu ana uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia katika eneo lile,
aende akaonane na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera lakini taarifa alizopewa
ni kwamba hakuna mtu ambaye hajalipwa.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One ili
wampatie taarifa juu ya malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo
kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko
hivi sasa.
“Nikimaliza
ziara ya mkoa huu, nataka tarehe 27 Februari, Wakuu wa hii kampuni waje ofisini
kwangu na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha na
wabunge wenu ili waje waseme kwa nini mzungu ni bora kuliko Mtanzania,”
alisema.
“Serikali
hii inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilmali zao. Haiwezekani
tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa mzungu kuliko mzawa,”
alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
IJUMAA,
FEBRUARI 17, 2017.
|
No comments:
Post a Comment