Wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa katika ukumbi wa bunge wakati
wa mkutano wa nne(4) wa bunge la kumi na
moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana Mjini Dodoma.
Alitumia
fursa hiyo kuwaasa wabunge kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia busara, hekima,
ustahimilivu na umoja huku wakitakiwa kujenga hoja ushawishi na matumizi ya
lugha zenye staha wakati wa vikao vya Bunge ili kujiepusha na mihemko ndani ya
Bunge.
“Nawasihi
kusoma na kuelewa hoja zinazoletwa mbele yetu ili kuzifanyia maamuzi yaliyo
sahihi,” alisema Ndugai ambaye alikuwa akitibiwa India.
Alimshukuru
Mungu kwa uponyaji na kumuwezesha kurudi tena nyumbani na bungeni kuongoza
Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 ulioanza jana mjini hapa, uliohudhuriwa na
wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa wamesusa vikao vya Bunge la Bajeti Juni
mwaka huu.
Ndugai pia
alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufuatilia matibabu yake na afya yake kwa
ujumla, wabunge, viongozi wa dini, na wananchi kwa kumuombea wakati wote
alipokuwa akipitia mapito ya kuugua.
“Niwashukuru
wapigakura wangu wa Kongwa kwa kuniombea na hasa baada ya kupata taarifa za
kushtusha kuwa mbunge wenu sipo tena duniani, lakini nawashukuru kwa uvumilivu
wenu,” alisema mbunge huyo wa Kongwa mkoani hapa.
Wakati Spika
akishukuru na kurudi salama bungeni, wabunge wa upinzani (wa vyama vinavyounda
Ukawa) wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe wamerejea
bungeni na kuungana na wabunge wenzao kuendelea na shughuli za Bunge.
Akiendelea
kutoa taarifa ya Spika, Ndugai alimshukuru pia daktari kiongozi aliyemtaja kwa
jina moja la Dk Vijay kwa kuongoza matibabu yake aliyeshirikiana na mkewe, Dk
Fatma na kuongeza kuwa ni ukweli usiopingika wanawake wanaweza.
Aliwashukuru
viongozi wanaosimamia shughuli za Bunge kwa kuongoza vizuri Bunge la Bajeti la
siku 70 lililoanza Aprili 9 hadi Juni 30, mwaka huu. Alimpongeza Naibu Spika Dk
Tulia Ackson kwa kazi nzuri wakati hayupo na kwamba ni ya kupigiwa mfano.
Spika
aliwapongeza wenyeviti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Andrew Chenge na Najma
Murtaza Giga na kuwataka waendelee kumpa ushirikiano kama walivyoshirikiana
wakati hayupo.
Tofauti na
matarajio ya wengi, hali ya amani na utulivu ilitawala bungeni licha ya ujio wa
wabunge wa upinzani ambao walisusa Bunge kwa takribani mwezi mmoja hadi Juni
30, mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti lilipomaliza vikao vyake.
Mbali ya
Mbowe, wengine waliokuwepo ni pamoja na Godbless Lema, Mchungaji Peter Msigwa,
David Silinde, John Heche na wengineo. Katika hatua nyingine, Spika Ndugai
alisema katika Mkutano wa Tatu miswada mitano ilipitishwa na kwamba Rais John
Magufuli ameshaisaini na kupitishwa kuwa sheria.
Alizitaja
sheria hizo kuwa ni Sheria ya Fedha na Matumizi ya Mwaka 2016, Sheria ya Fedha
Namba 2 ya Mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya
2016, Sheria ya Marekebisho ya Pili Namba 4 ya 2016 na Sheria ya Marekebisho ya
Ununuzi wa Umma Namba Tano, 2016.
CHANZO: HABARI LEO.
|
Wednesday, September 07, 2016
Ndugai Awarejesha Bungeni Ukawa.... Atoa Somo .
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment