Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja
Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu azindua
Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi
Mkoani Kagera ili kuondokana na uvuvi haramu na madhara yake
yanayosababisha kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria na kupelekea kudhoofisha uchumi wa Mkoa na
Mwananchi mmoja mmoja wanaojishughulisha na shghuli za uvuvi.
Mpango Mkakati huo umezinduliwa leo
Agosti 24, 2016 na Mkuu wa Mkoa katika Mwalo wa Malehe Kituo cha Kanyigo
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambapo aliteketeza nyavu haramu zilizokamatwa
katika doria mbalimbali kupitia kituo hicho zenye thamani ya shilingi milioni
205, 510,000/-
Kabla ya kuzindua Mpango Mkakati huo Mhe. Kijuu alikitembelea
Kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Vicfish ili kujionea uzalishaji wa
kiwanda hicho ambapo Meneja wa Kiwanda Bw.Nurdin Salum Juma alitoa
taarifa kuwa uwezo wa kiwanda hicho ni kuzalisha tani 60 kwa siku lakini
kutokana na madhara ya uvuvi haramu kiwanda hicho kinazalisha tani 6 hadi 8 kwa
siku sababu ukosefu wa samaki.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi Ofisi ya
Usimamizi Raslimali za Uvuvi Mkoa wa Kagera Bw. Gabriel Mageni alimweleza Mkuu
wa Mkoa kuwa kuanzia kipindi cha mwaka
2012 hadi sasa Agosti 2016 ofisi yake imefanikiwa kufanya doria na kukamata
zana za uvuvi haramu katika Vituo vya Kanyigo, Bukoba na Halmashauri ya Wilaya
ya Bukoba kama ifuatavyo:-
Makokoro ya Sangara 192 yenye thamani
ya shilingi milioni 96,000,000/-,
Timba 3,319 zenye thamani ya shilingi milioni
232, 330,000/-,
Nyavu za Makila 2,410 zenye thamani ya shilingi milioni 24, 100,000/-,
Nyavu za dagaa chini ya
(milimita 88) 25 zenye thamani yashilingi milioni 17,500,000/-
na Kokoro ndogo
za vyambo 16 zenye thamani ya shilingi milioni 3,200,000/-, Jumla kuu ni
shilingi milioni 373,130,000/-.
Aidha, Bw. Mageni alimweleza Mkuu wa
Mkoa kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika ofisi yake ni kuachiwa suala la
uvuvi haramu wao peke yao kama Maafisa Uvuvi badala ya Taasisi zote za Serikali
na binafsi na Wananchi kupambana na
uvuvi haramu, Pili ni kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Vitongoji,
Vijiji na Kata hasa watendaji na Wenyeviti wanaozunguka katika Ziwa Victoria.
Akiwahutubia wananchi na wavuvi
katika Mwalo wa Malehe Mhe. Kijuu aliwaeleza kuwa Mkakati aliouzindua utakuwa
shirikishi hasa viongozi na wanachi ili kukomesha uvuvi haramu katika Ziwa
Victoria, aidha, alitoa rai kuwa kiongozi au Mtendaji yeyote atakayegundulika
kuhusika au kukutotoa ushirikiano katika suala la uvuvi haramu atashghulikiwa
ipasavyo kisheria.
Aidha, aliwataka wananchi wote
wanaojihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja ili kuruhusu samaki kuzaliana
na kuvuliwa kwa utaratibu ulio mzuri.
Katika hatua nyingine aliwahamasisha
wavuvi kujihusisha na miradi ya ufugaji samaki katika mabwawa kuliko kutegemea
Ziwa la Victoria peke yake.
Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali
za Uvuvi Mkoani Kagera unalenga kuzuia
uvuvi haramu katika Maziwa yanayopatikana katika Mkoa kwa kuendesha doria za
mara kwa mara na endelevu, kuhamasisha wavuvi kukopa na kuwekeza katika uvuvi
wa kisasa, na kutunza mazingira na mazalia ya samaki ili kuongeza wingi na
upatikanaji wa samaki hasa katika Ziwa Victoiria.
Mpango huo utawahusisha wadau
mbalimbali vikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wananchi, Wavuv,i Wenye
Viwanda na Viongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali hasa kuanzia katika
ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Kata ili kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa
mara moja katika Mkoa wa Kagera.
|
No comments:
Post a Comment