|
Mashirika yanayotetea
haki za wanawake na usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa nafasi muhimu za
uongozi serikalini unaofanywa na Rais John Magufuli, hauzingatii hali halisi ya
uwakilishi wa kijinsia.
Akizungumza jana jijini
Dar es Salaam kwa niaba ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha ya kupiga kelele tangu uteuzi wa
Baraza la Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado hali inaonekana kuwa tete
kwa upande wa wanawake.
Alisema katika baraza
hilo, kati ya Mawaziri 19, wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia 21.1 ya
mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi wa baraza la Serikali ya Awamu ya Nne
ambalo lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na asilimia 33.3.
Alisema Manaibu Waziri
kati ya 16 waliopo, Wanawake ni watano sawa na asilimia 31.25.
“Ukiangalia upande wa
makatibu wakuu, walioteuliwa ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26 sawa na asilimia
89.7 huku wanawake wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7 ya mwaka 2014
hadi kufikia watatu sawa na asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi.
Alisema uteuzi wa
wanawake katika nafasi hizo umepungua kwa asilimia 10.
Katika nafasi ya Wakuu
wa Mikoa, Liundi alisema idadi ya Wanawake imeshuka zaidi, kati ya wakuu wa
mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni Wanaume sawa na asilimia 80 na Wanawake ni watano
sawa na asilimia mbili.
Kadhalika, alisema
idadi ya Wakuu wa Wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka
jana,2015 ambako Wanawake walikuwa asilimia 35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi
umepungua kwa asilimia saba.”
Liundi alisema mikoa
mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi Wanawake kwa nafasi ya
ukuu wa wilaya.
“Hii iko hata kwenye
nafasi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa halmashauri,
hatuoni idadi ya wanawake ikiongezeka na badala yake inashuka,” alisema.
Mwakilishi wa Taasisi
ya Women Fund Tanzania (WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati ya
mataifa duniani yaliyoridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na
kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu ikiwamo ushiriki katika ngazi
zote za uamuzi, lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka isukumwe na
asasi za kiraia jambo linaloleta ukakasi.
Alisema miongoni mwa
mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR: 1948),
Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake
(CEDAW: 1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo na
Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mwakilishi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Gladness Munuo alisema Tanzania
kupitia Dira ya Maendeleo ya 2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya
ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na jamii yenye maono ya kimaendeleo na
utamaduni wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.
|
No comments:
Post a Comment