|
Waziri wa Katiba na
Sheria wa Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe amesema jumla ya watuhumiwa 30 wa mauaji ya
vikongwe na wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, wamehukumiwa kunyongwa,
baada ya kupatikana na hatia ya mauaji hayo.
Dk Mwakyembe amesema
pia kuwa serikali itaendelea kutoa adhabu kali kwa watu watakaobainika
kuendelea kuhusika na mauaji ya watu hao ili kumaliza tatizo hilo, ambalo
limeipaka matope Tanzania kwa kuonekana sio kisiwa tena cha amani. Waziri huyo
alisema hayo mjini Shinyanga jana,Julai 11,2016 alipofanya ziara yake ya kikazi.
Alisema katika miaka ya
hivi karibuni tatizo la mauaji ya wenye ualbino na vikongwe yamepungua nchini
na kwamba watahakikisha wanayakomesha kwa kutoa adhabu kali kwa wauaji.
“Tatizo hili la mauaji
ya vikongwe na albino linatutia sana doa nchi yetu kimataifa ambayo imekuwa
ikisifika kwa amani na utulivu, hivyo natoa mwito kwa wananchi waachane na
mauaji ya watu hawa wasio na hatia pamoja na mahakama zifanye kazi kwa kutoa
hukumu za haraka kwa watu watakaohusika na mauaji hayo,” alisema Dk Mwakyembe.
Hata hivyo, Dk
Mwakyembe alisema serikali itaanza mikakati ya kujenga mahakama za mwanzo kwa
kila kata nchi nzima ili kuondoa misongamano za kesi mahakamani na kukarabati
majengo ya mahakama ambayo yamechakaa.
Aliwataka wakuu wa
wilaya, waunde kamati za maadili ya wilaya.
Akisoma taarifa ya
mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe.Zainabu Telack, alitaja changamoto ambazo
zinawakabili kuwa ni uchakavu wa majengo ya mahakama, uhaba wa mahakimu na
magereza ya Shinyanga na Kahama kuwa finyu na hivyo kusababisha mlundikano wa
wafungwa.
|
No comments:
Post a Comment