Wabunge wa
upinzani wameendelea kususia kwa siku ya tatu mfululizo vikao vya Bunge
vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson tangu walipotangaza hatua hiyo
Jumatatu wiki hii kwa kutokuwa na imani naye.
Tangu
Jumanne wiki hii wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi
huyo kwa madai kuwa anaminya demokrasia.
Siku hiyo
wabunge hao waliingia bungeni kama kawaida na Dk Tulia alipomaliza tu kusoma
dua ya kuliombea Bunge, walitoka hadi kipindi hicho kilipomalizika na naibu
spika kumwachia mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuongoza, ndipo wote
waliporudi ukumbini na kuendelea na shu ghuli zao kama kawaida.
Juzi,June 01,
2016,Wabunge hao wote kama kawaida waliingia bungeni asubuhi na alipoingia Dk
Tulia kuongoza kikao hicho, walisimama na kusikiliza dua ya kuliombea Bunge,
kisha walitoka na kuwaacha wabunge wa CCM wakiendelea na Bunge.
Siku nzima
ya juzi,June 01, 2016, ambayo Dk Tulia aliendesha kikao cha asubuhi na jioni,
wabunge hao hawakuhudhuria na ilipofika wakati wa kusoma hotuba ya msemaji wa
kambi ya upinzani kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde aliingia
ukumbini akitokea nje na kuomba hotuba yake iingie kwenye kumbukumbu rasmi za
Bunge kama ilivyo. Kisha akasema: “Sitaisoma hapa kwa kuwa
haturidhishwi na mwenendo wa Naibu Spika wa kutuendesha kama watoto.”
Wabunge hao
wa upinzani walitoa sababu sita kwanini wanataka Dk Tulia aondolewe madarakani
kwa Azimio la Bunge.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Simanjiro,
James Millya alizitaja sababu hizo kuwa ni kwanza Dk Tulia ameweka maslahi ya
chama chake cha siasa mbele kuliko maslahi ya Bunge, kinyume na Kanuni ya 8(b)
ya Bunge.
“Pili, Mei 6 alitumia vibaya madaraka ya
kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka Ibara ya
12(2) ya Katiba. Muongozo huo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa wabunge
wanawake,” alisema.
Ya tatu ni
kitendo cha Dk Tulia kuvunja Kanuni ya 64(1) (f) na (g) zinazokataza mbunge
kutumia lugha ya matusi kwa mbunge mwingine ambapo alinukuliwa akisema “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege
wako humu ndani.”
Alisema ya
nne ni Mei 30 kiongozi huyo aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya
Katiba na kutumia vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge kumzuia
Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza
majukumu yake ya kikatiba ya kusimamia na kuishauri Serikali.
“Sababu ya tano ni kuwa Mei 26, mwaka huu Dk
Ackson akiongoza kikao cha Bunge bila ridhaa ya upinzani alishiriki kufuta
sehemu ya hotuba ya msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia kinyume cha kanuni ya 99(9) ya Bunge bila kushirikisha kamati yoyote
ya Bunge,” alisema.
Sababu ya
sita, Millya alisema kuwa ni kitendo cha Dk Ackson kukataa taarifa ya maoni
tofauti, iliyowasilishwa na wabunge wanne wa upinzani.
|
No comments:
Post a Comment