Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka, wako
hatarini kufutiwa posho kama wataendelea kususa vikao vya Bunge kama
walivyotangaza.
Hali hiyo inatokana na hoja zaidi ya
mbili zilizowasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa njia ya Mwongozo huku moja
ikiwasilishwa na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, Dk Harrison
Mwakyembe, zikikusudia kutaka Bunge kufuta posho za wabunge hao.
Akizungumza jana bungeni baada ya
kuruhusiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Dk Mwakyembe akitumia ibara za
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na Kanuni za Kudumu za Bunge,
alitaka uongozi wa Bunge kutazama upya kama wabunge hao wanastahili kulipwa posho.
Dk Mwakyembe, kwanza alitumia Ibara
ya 26 ibara ndogo ya kwanza na ibara ndogo ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo aliinukuu; “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za
Jamhuri ya Muungano. Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na
sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za
nchi.”
Baada ya hapo alinukuu tena Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa
aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote
wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na
sifa za kazi wanayoifanya. Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya
haki.”
Kwa kuzingatia ibara hizo za Katiba,
alisema kwa kutumia nafasi yake ya raia wa Tanzania na Waziri mwenye dhamana ya
Katiba na Sheria, alihoji kama haki inatendeka, kulipa posho na stahiki wabunge
ambao hawakuingia bungeni wala hawakuwa katika shughuli inayotambuliwa na
Bunge, sawa na waliokuwa wakifanya kazi bungeni.
Alitaka Bunge lifafanue kwa
kuzingatia ibara hizo za katiba kama ni haki kulipa wabunge hao wa Ukawa,
wanaoingia bungeni na kusaini ili walipwe posho, kwa kubonyeza vitufe vya kielektroniki
na kuingia bungeni kwa sekunde chache na kutoka kwenda kupumzika.
Kuhusu wabunge waliosimamishwa kazi
na Bunge, Dk Mwakyembe alihoji kama Bunge linazingatia Kanuni ya 75, ama la.
Kanuni hiyo inasema: “Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika
Bunge na hataingia tena katika sehemu yoyote ya Ukumbi wa Bunge na maeneo ya
Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa, na atalipwa nusu mshahara na
nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”
Kabla ya Mwongozo wa Dk Mwakyembe, Juzi ,June 01,2016,usiku Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM) aliomba Mwongozo na
aliporuhusiwa alimtaka Naibu Spika aeleze kama kitendo cha wabunge hao wa
Upinzani kuingia na kukaa muda mfupi na kutoka bungeni, kinatofautiana na
tatizo la wafanyakazi hewa ambao wanapigwa vita na serikali.
“Kweli
Mheshimiwa Naibu Spika, serikali inawaona na wewe unawaona, hii si kuiibia
serikali? Au na sisi tuanze?” Alihoji Keissy.
Mbali na Keissy, Mbunge wa Geita
Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliomba Mwongozo jana,June 02,2016, na kumtaka Naibu Spika kuzingatia
Mwongozo wa Dk Mwakyembe na Keissy, akieleza kuwa kama si dharau kwa Bunge,
kumsimamisha mtu kazi, halafu anaruhusiwa kuitisha mikutano ya kibunge jimboni.
Alimtaka Naibu Spika ambaye ni
mwalimu wa sheria, akubali iletwe hoja ya kurekebisha Kanuni za Bunge ili
adhabu inayotolewa kwa mbunge, imdhibiti asifanye shughuli zozote ikiwemo
mikutano ya hadhara wakati wa adhabu.
Akipokea miongozo hiyo, Naibu Spika aliahidi
kutolea uamuzi baadaye baada ya kufanya mashauriano huku suala la adhabu
likirejeshwa kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wabunge wa Ukawa kuanzia mwanzoni mwa
wiki hii waliazimia kususa kuingia bungeni katika vipindi vyote vitakavyoongozwa
na Naibu Spika, kwa madai kuwa anawaongoza kibabe kama wanafunzi na kuwa hajui
uchungu wa kampeni katika majimbo.
Hata hivyo, juzi Dk Tulia
aliwataka Watanzania wasikubali kupotoshwa na Kambi Rasmi ya Upinzani,
iliyoamua kususa vikao anavyoviongoza, kwa kuwa kama wanaona amekosea, kuna
fursa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake.
Kwa upande wao, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni imewasilisha kwa Ofisi ya Spika wa Bunge kusudio la kumwondoa
madarakani Naibu Spika wanayemtuhumu kwa mambo sita ikiwemo upendeleo, ubabe na
kufanya kazi kwa maslahi ya Serikali, badala ya umma.
Kusudio hilo la maandishi lilipelekwa
katika ofisi hiyo jana na kupokelewa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah
kwa niaba ya Spika, Job Ndugai ambaye hakuwepo ofisini wakati huo.
Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya
(Chadema) ndiye aliyewasilisha kusudio hilo kwa niaba ya kambi hiyo ya upinzani
na kuzungumza na wanahabari kuhusu hatua hiyo, katika mkutano na vyombo vya
habari.BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
|
Friday, June 03, 2016
Home
SIASA
UPINZANI KUTOKA BUNGENI:-Waziri Mwakyembe ataka Mishahara na Posho zao Zifutwe....Keissy Awafananisha na Watumishi HEWA.
UPINZANI KUTOKA BUNGENI:-Waziri Mwakyembe ataka Mishahara na Posho zao Zifutwe....Keissy Awafananisha na Watumishi HEWA.
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment