Jeshi la Polisi Nchini linawashikilia
watuhumiwa 14 kufuatia tukio la mauaji ya watu watatu lililotokea katika
msikiti wa Rahman eneo la Ibanda relini mkaoni Mwanza, Mei 18 mwaka huu,2016.
Akiongea na waandishi wa habari Jana,May
24, 2016, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidizi Advera Bulimba,
alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine unaendelea katika maeneo
mbalimbali nchini.
Hivyo amewaomba wananchi kutoa
ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo ili kufanikisha kuwakamata wale wote
wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
“Nitoe
wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya usalama katika kufichua
wahalifu kwa kuwa ni watu tunaoishi nao, hivyo hakuna budi kutoa taarifa zao
ili usalama na mali zetu uendelee kuimarika”, aliongeza Kamishna Msaidizi
Bulimba.
Hata hivyo, alieleza kuwa hali ya
usalama nchini iko shwari na kuwatoa hofu wananchi kwamba jeshi hilo
limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwepo.
“Niwaombe
wananchi kuondoa hofu juu ya hali ya usalama na wasiwasi na watoe ushirikiano
kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu
wanakamatwa haraka”, alisema Kamishna Msaidizi Bulimba.
Aliongeza kuwa uchunguzi zaidi wa
matukio ya uhalifu nchini unaendelea ikiwemo matukio ya mkoani Tanga, Dar es
Salaam na mikoa mingine ili kubaini na kuwakamata wahusika na kufikishwa katika
vyombo vya sheria.
Hivi karibuni kumeripotia matukio mbalimbali
ya uvunjifu wa amani katika mikoa mbalimbali
ikiwemo mauaji ya watu watatu waliouawa wakiwa msikitini jijini Mwanza.
|
No comments:
Post a Comment