Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi kote nchini
kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa, badala ya kutaka kupata faida
kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za miradi ya ujenzi wanayopata kutoka serikalini.
Dkt. Magufuli amesema
hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano wa bodi
ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016 unaofanyika kwa siku mbili katika
ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli amesema
serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania pale
inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini amewataka kujirekebisha kwa
kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo
serikali itaridhika.
“Nawatolea mfano, idara
ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya, kwenye bajeti
wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu yanaonesha kila jengo lisizidi
shilingi milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka
jengo moja lijengwwe kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400, sasa nakuuliza
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo
huo utapasua moyo.
“Hata kama utakuwa na
upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa mimi niwaombe ndugu zangu
wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi wazalendo
ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi” Amesema Rais Magufuli
Pamoja na hilo, Rais
Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa serikali
pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake amewataka kutoa taarifa kwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili watendaji hao wakamatwe na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Mimi niwaombe
wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa,
atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa huna
hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa
hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa”
Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli
ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili waweze kupata zabuni
katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini
ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya
Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.
“Sina uhakika kwamba
mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata ya
kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
“Nitasikitika sana
kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania, wenzetu
wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa
kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili,
tumejipanga kujenga reli ya kati (Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu
tunaanza na kilometa 100, lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya
China, tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor)
itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania
mmejipangaje? " ameuliza Rais Magufuli.
Mkutano huo pia
umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema Taasisi hiyo ipo tayari
kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa
sekta zenye rushwa kubwa na ametaka wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha
tatizo hilo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Mei, 2016.
|
No comments:
Post a Comment