Kuanzia sasa wateule
wengi wa Rais John Magufuli ,Serikalini watakuwa vijana kwa kuwa amegundua wengi
hawapendi rushwa, amesema.
Aidha, Rais Magufuli
amesema anafahamu kwamba vijana hawapendwi lakini amegundua ndio wachapakazi
ambao watasaidia kulipeleka taifa katika maendeleo anayoyatamani.
Rais Magufuli alisema
hayo jana,May 26,2016 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa makandarasi wa mikoa ya Dar es
Salaam, Mbeya na Dodoma, jijini.
“Nimegundua vijana
wengi hawapendi rushwa, hivyo nitaongeza vijana kila nikiteua kwa kuwa
niliowaweka naona matunda ya kazi zao," alisema na kuongeza kuwa: “Najua
watu wanawachukia sana ila nitawaongeza.
“Palipo na vijana
nimeona mambo yanaenda na kuna mabadiliko. Wazee ndio tumelifikisha taifa hili
hapa. Hakuna asiyejua kuwa Tanzania ilichakaa kila mahala.”
Tangu aingie Ikulu
Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli amejipambanua kama mwenye kupiga vita
wizi, rushwa, ufisadi, ukwepaji kodi, uzembe na ukosefu wa maadili wa watumishi
wa umma.
Aidha, Rais Magufuli
alisema idadi ya watumishi hewa imefikia 10,292 huku vijana wengi wenye ujuzi
wanamaliza vyuo vikuu na kukosa ajira.
Alisema kama si tatizo la uwapo wa
watumishi hewa, ajira zipo kwa wingi.
“Nataka vijana ili
twende kwa kasi, ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo tunayoyatarajia,”
alisemna.
Rais pia alizungumzia
uamuzi wake wa juzi wa kuvunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kutengua
uteuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Awadhi Mawenya.
Rais Magufuli alisema
zaidi ya Sh. bilioni 87 zililipa mikopo hewa kwa wanafunzi 480 wenye daraja la
nne kidato cha nne, huku ikiaminika mikopo ni kwa ajili ya watoto wa masikini.
“Unashangaa
anayesimamia kitengo ni Profesa. Hapa ndiko nchi ilikofikia,” alisema.
Rais Magufuli alitoa
mfano mwingine wa Meli kubwa 65 za makontena zilizotia nanga katika Bandari ya
Dar es Salaam bila kuandikwa, ambazo alisema “hazijulikani zilielekea wapi na
hazikulipwa.”
Baada ya Rais Magufuli
kumaliza hotuba yake, alimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
(34) kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo.
Makonda alisema
alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia
barabara na kubaini zaidi ya Sh. bilioni 2.2 zilitumika kujenga barabara ambazo
mvua ikinyesha hazipitiki.
Alisema pia walibaini
barabara zilizokuwa zikarabatiwe kwa Sh. milioni 200, zilitengewa Sh. bilioni
moja kwa kila barabara na baadaye ziliombwa zaidi ya Sh. bilioni 5.9 na
zilikuwa katika mchakato wa kulipwa lakini alizizuia.
“Manispaa ya Kinondoni
ni tatizo kubwa...unakuta wananchi wanalia shida, wao wanalia kwa uongo kwa
kuwa wanajua kuna fedha wanapata kama hizo.
“Nashukuru Mfuko wa
Barabara umewanyima fedha na wameambiwa watengeneze barabara za awali hadi
zikamilike kwa kutumia mapato yao ya ndani,” alisema.
Mbali na nafasi kadhaa
za Wakuu wa Wilaya ambako habari za uhakika zinasema wengi watabadilishwa, Rais
Magufuli pia ana nafasi ya uteuzi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, baada ya
kuteungua uteuzi wa Charles Kitwanga kwa sababu ya ulevi, Ijumaa iliyopita.
Aidha, Rais Magufuli
hajateua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga tangu atengue uteuzi wa Anne Kilango
Malecela kwa kutoa taarifa ya uongo kuwa mkoa wake haukuwa na watumishi hewa
Aprili, mwaka huu.
Rais Magufuli pia
hajafikisha jumla ya Wabunge 10 anaoruhusiwa kuwateua kwa mujibu wa katiba,
hivyo kuweka uwezekano wa kuwapo kwa vijana wengi zaidi serikalini kwa mara ya
kwanza katika miaka 55 ya Uhuru.
|
No comments:
Post a Comment