Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeendelea kushika dola licha ya upinzani mkali kutoka vyama
vingine vya siasa hasa vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Maadhimisho
ya miaka 39 ya kuzaliwa kwake, yanaandika historia nyingine ya chama hicho
tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977.
Chini ya
Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere chama hicho ambacho ni cha pili kwa
ukubwa barani Afrika kikitanguliwa na ANC cha Afrika Kusini, kinajivunia mambo
mengi yaliyokifanya kudumu mpaka sasa wakati vyama vikongwe vya nchi nyingine
kama Zambia (UNIP), Kenya (Kanu) na Malawi vikiwa vimeshaondolewa madarakani.
Nape ataja
siri ya mafanikio.
Katibu wa
NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema mfumo wa chama hicho
kujiimarisha kimtandao kuanzia ngazi ya shina kwa maana ya balozi wa nyumba
kumi mpaka taifa umekifanya kiendelee kuwa kimbilio la wananchi wengi hadi
kufikia kupata wanachama zaidi ya milioni sita, kutoka wanachama wachache
waliokuwapo miaka iliyopita.
“Chama chetu
kimeendelea kuwa na sura ya kitaifa, kalenda inayojulikana ambayo imekuwa
ikiruhusu chaguzi kila baada ya miaka mitano na kuifanya Tanzania kuwa nchi
inayofuata misingi ya kidemokrasia,” anasema.
Yapo baadhi
ya mambo ambayo chama hicho kinajivunia kwa miaka 39 tangu kizaliwe.
Kuendelea
kushika dola.
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Patrick Myovela anasema mafanikio ya chama hicho
ni pamoja na ushindi kwenye chaguzi mbalimbali zilizowawezesha kuendelea
kushika dola.
“Tumepata
ushindi uliotuwezesha kushika dola katika chaguzi kuu zilizofanyika zaidi ya
mara sita. Tumeishi kwenye shabaha ya chama chetu ile inayotaka kuendelea kuwa
madarakani, tukiunda na kusimamia Serikali,” anasema.
Myovela
ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, CCM bado inaaminiwa
na Watanzania wengi ndiyo maana wameendelea kukipa kura na kukiwezesha kuunda
Serikali. Hiyo imetokana na imani ya wananchi juu ya chama hicho.
Nape anasema
mara zote CCM imekuwa ikichagua mgombea urais atakayeweza kushika bendera ya
chama hicho kwa umakini zaidi kwa kuzingatia matakwa ya wananchi kwa wakati
husika.
Uongozi wa
kupokezana.
Kati ya vitu
ambavyo vimeiletea sifa kubwa Tanzania ni pamoja na kuwa na uongozi wa
kupokezana madaraka.
Wakati nchi
nyingine ikiwamo Uganda, Burundi na Zimbabwe zikivurugana kutokana na vyama
vinavyotawala kushindwa kuenzi dhana ya kupokezana, tayari Tanzania imeshapitia
awamu tano za uongozi na kila awamu ikiongozwa na rais tofauti.
“Baada ya
kuongoza miaka 23, Mwalimu Nyerere aliamua kung’atuka akimuachia Rais wa Awamu
ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye aliingia kwa kupigiwa kura licha ya kuwapo
kwa mfumo wa chama kimoja,”anasema Nape.
Anasema
uongozi huo wa nchi kupokezana ulimfanya
Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kushikilia usukani akimpokea Mwinyi hadi
mwaka 2005 alipomkabidhi Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mwaka jana
Rais John Magufuli.
Myovela
anasema ni dhahiri taswira nzuri ya uongozi wa nchi inatokana na uimara wa
chama kilichopo madarakani.
Demokrasia
ya vyama vingi.
Licha ya
kuwapo kwa mabadiliko ya kidemokrasia hususan mfumo wa vyama vingi ulioasisiwa
na CCM yenyewe mwaka 1992, chama hicho kimeendelea kushamiri huku kikishinda
chaguzi zote kuu na zile za mitaa.
Nape anasema
wakati CCM iliamua kuasisi mfumo huo, wananchi wengi walitamani kiendelee kuwa
peke yake.
“Kumbuka
kwamba wakati wa kura ya maoni ya kuendelea kuwa na mfumo wa chama kimoja au
kuwa na vyama vingi vya siasa, Watanzania wengi walipendekeza kuendelea kuwapo
kwa chama kimoja, lakini kutokana na demokrasia, CCM iliamua kuruhusu mfumo wa
vyama vingi kuanza nchini,” anasema.
Mpaka sasa
Tanzania ina vyama vya siasa zaidi ya 20 vilivyosajiliwa, vingi vikiwa
vimefanikiwa kushiriki katika chaguzi mbalimbali.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Iringa, Enock Ugulumu ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Mkoa wa Iringa anasema kama kingeendelea kuwa na mgombea mmoja kila kinapoingia
madarakani, uhakika wa kuwapo mpaka leo usingekuwapo.
“Mfumo wa
kubadilishana uongozi ndiyo siri kubwa ya ushindi wa CCM, hatung’ang’anii
madaraka kwa sababu Katiba ya CCM imeruhusu demokrasia tangu ndani, mpaka nje
kwenye umma.
"Vinginevyo
Mwenyekiti wa CCM Taifa asingetaka kutoka kwa miaka yote, angebaki kuwa
yuleyule,” anasema.
Vipo vyama
ambavyo vimeshindwa kuzingatia mfumo wa kubadilishana madaraka kwa kuwa na
viongozi wale wale tangu kuanzishwa kwake.
Katiba Mpya.
Mchakato wa
upatikanaji wa Katiba Mpya unaonyesha namna ambavyo CCM ilivyofanikiwa kupokea
na kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yanayotolewa na wananchi kutoka katika
kada zote.
Nape anasema
CCM inajivunia kuwa na mchakato huo hata kama haujafikia mwisho.
Anasema uwepo
wa rasimu iliyopita kwenye Bunge la Katiba kunaifanya CCM ionekane inasikiliza
maoni ya Watanzania na kuyatumia inapowezekana.
“Ni chama
kilichodumu kwa muda mrefu, kinajivunia kuwa kisikivu na kutimiza mahitaji ya
Watanzania.” Anasema bila nia njema ya kukubali mchakato huo uwepo,
usingeanzishwa na kufikia hatua ya kura za maoni ilipo sasa.
Kulinda na
kudumisha amani nchini.
Nape anasema
katika tunu za taifa mbazo CCM inajivunia kuziendeleza tangu uhuru kuwa ni
kulinda na kudumisha amani.
Katika miaka
yote, CCM imekuwa ikiagiza na kusimamia kuhakikisha Serikali inalinda na
kudumisha misingi imara ya amani iliyoasisiwa na waanzilishi wa taifa.
Hata hivyo,
anasema CCM imeshiriki katika harakati za kutafuta ukombozi wa nchi majirani
ili kujihakikishia usalama ndani na nje
ya nchi
Uhuru, umoja
na mshikamano .
Myovela
anasema ni ukweli usiopingika kuwa umoja na mshikamano uliopo nchini unatokana
na usimamizi mzuri wa Serikali inayoundwa na chama hicho.
Anasema
kutokuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile ikiwamo udini, ukabila, rangi wala
ukanda unatokana na misingi mizuri iliyowekwa na chama hicho tangu kuundwa
kwake.
Nape anasema
kitendo cha kuwa na ilani za uchaguzi zinazogusa maisha ya watu wa kila kada,
kimeisaidia Serikali kutimiza wajibu wake.
“Kila mwaka
wa uchaguzi, CCM imekuwa ikiisimamia Serikali katika kutimiza majukumu yake
kupitia ilani ya uchaguzi. Ukisoma ilani zote utagundua CCM haikurupuki,
inafanya mambo yake kwa umakini mkubwa. Hili tunajivunia,” anasema Nape.
Anasema
msingi wa utawala bora lazima uendane na kile ambacho chama kingependa wananchi
wake wafanyiwe kwa kuiagiza Serikali kupitia ilani yake.
Anasema
viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa taarifa ya utekelezaji wao wa majukumu
kwa chama ili kipate nafasi ya kukosoa na kusonga mbele.
Utawala bora.
Nape anasema
Watanzania wameshuhudia uanzishwaji wa mikoa, wilaya, kata na vijiji vipya ili
kuwasogezea huduma karibu.
Maazimio.
Anasema kuna
maazimio mbalimbali likiwamo Azimio la Mtowisa lililotaka kila kaya
kujitosheleza kwa chakula na Azimio la Zanzibar lililofungua Demokrasia ya
ndani ya CCM, haya yote yamechangia katika mafanikio ya CCM.
Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari kwa WhatsApp+255789925630-/+255756830214.
|
No comments:
Post a Comment