Hatimaye,
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa
msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya
mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es
Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama
inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi,
haikubaliki na sio halali kikatiba.
“Hoja ya
kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo
na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama
tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.
Makamu huyo
wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane
vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini
hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama
baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.
Aidha,
Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali
Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar
kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.
Maalim Seif amesema
kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana
na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar
es Salaam.
Amesema kuwa
endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba
ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.
Ametaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi
na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake.
Mbali na
hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha
Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko
lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu
hiyo kikatiba.
Ameitaka ZEC
iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe
wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza
mshindi.
Maalim Seif
ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio
ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake
hawatakubali.
|
No comments:
Post a Comment