HALI YA SIASA ZANZIBAR:- Rais Kikwete ateta na Maalim Shariff Seif Hamad. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, November 05, 2015

HALI YA SIASA ZANZIBAR:- Rais Kikwete ateta na Maalim Shariff Seif Hamad.


Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Sharif Seif Hamad, kuhusu hali ya kisiasa visiwani humo walipokutana Ikulu jijini Dar es Salaam jana,November 04,2015. PICHA: IKULU.

Rais  Jakaya Kikwete, amekutana na  kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif  pia alikuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofanyika Oktoba 25,2015.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana,November 04,2015 jioni, ilieleza kuwa viongozi hao walikutana jana Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa viongozi hao wawili walikutana kwa takribani saa moja Ikulu, kuzungumzia hali ya kisiasa Zanzibar kufuatia ombi la Maalim Seif kutaka kukutana na kuzungumza na Rais Kikwete.

Viongozi hao wamekubaliana kuwa mashauriano yaendelee kufanyika baina ya pande zote zinazohusika na hali ya kisiasa Zanzibar,” taarifa hiyo ilieleza kwa kifupi.

Zanzibar inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Rais na uwakilishi wa Zanzibar, kwa maelezo kuwa ilibaini kuwapo kwa kasoro kadhaa kisiwani Pemba.

Uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu 2015 ulitangazwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jesha Salim Jecha, Oktoba 28, mwaka huu na kuibua mgogoro.

Katika tangazo la kufuta matokeo hayo, Jecha alisema uchaguzi huo utarudiwa, lakini Maalim Seif, viongozi na wafuasi wa CUF wanapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo na kusisitiza kwamba Maalim Seif anapaswa kuapishwa.

Waangalizi wa kimataifa na wa ndani pia walieleza kushangazwa kwao na hatua ya Jecha kufuta matokeo hayo wakati hawakushuhudia kasoro zozote wakati wa upigaji kura kisiwani Pemba hadi baada ya kutoa taarifa yao ya kwanza.

Mataifa kadhaa ya nje yakiwamo Uingereza, Ireland na Marekani pia yalieleza kushangazwa na uamuzi wa wao na kushauri ZEC iendelee na mchakato wa kutangaza matokeo.


Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa taarifa za kukubaliana na uamuzi wa Zec wa kufuta matokeo na kutaka uitishwe uchaguzi mpya.

Kabla Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar  hajakutana na Rais Kikwete jana, alilalamika kwamba alikuwa akiwapigia simu pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, bila kuzipokea kwa lengo la kutaka kutafuta suluhisho la mgogoro huo.

Wadau kadhaa wameshaingilia kati kusaka suluhu kwa kukutana na pande zinazohusika. Miongoni mwao mi Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, viongozi wa dini na viongozi wastaafu.


Source:-Nipashe.


Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za  Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga  na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp .
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad