NIPASHE
Zikiwa
zimebakia siku sita kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kura ya maoni iliyoendeshwa na
Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inamweka kileleni
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa changuo la kwanza la wengi
kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho.
Wakati
Lowassa akiwafunika watia nia wenzake ndani ya CCM, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk. Wilbroad Slaa, anawafunika wenzake kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akiwa
changuo la wengi kwa asilimia 23.1.
REDET
wamesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama
maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika
kipindi cha utafiti.
“Sampuli iliyotumika katika utafiti huu kwa kiwango cha kutosha ni
wakilishi na ina akisi hali halisi ya Watanzania,” imesisitiza
ripoti hiyo iliyojatwa kuwa ni maoni ya wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa
Oktoba 2015, mwaka huu.
Katika
utitiri wa watia nia ndani ya CCM, kati ya wahojiwa 1,250 waliohojiwa, Lowassa
alipigiwa kura na watu 338, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, akipata asilimia 8.2 akichaguliwa na watu 103.
Utafiti
wa REDET ulifanyika katika wilaya moja moja kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara
baada ya wahojaji kukataliwa ruhusa ya kufanya utafiti wao katika mikoa mitano
ya Zanzibar.
Utafiti
huo uliokuwa umedhaminiwa na kampuni ya Business Times Limited, ulifanyika kati
ya Juni 23-26, mwaka huu na kila wilaya ilikuwa na wahojiwa 50.
Kwa
upande wa CCM watia nia wengine ni Mizengo Pinda nafasi ya tatu akiwa na
asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; John Magufuli nafasi ya nne
akipata asilimia 6.6 akipigiwa kura na watu 83 na Charles Makongoro Nyerere
nafasi ya tano akipigiwa kura na watu 54.
Wengine
ni Mark Mwandosya nafasi ya sita akipata asilimia 3.1 akichaguliwa na
watu 39; Dk. Harrison Mwakyembe nafasi ya saba akiwa na asilimia 1.4
akichanguliwa na watu 18; Frederick Sumaye nafasi ya nane akipata
asilimia 1.4 akichaguliwa na watu 17; nafasi ya tisa imekamatwa na Jaji
Augustino Ramadhani akiwa na asilimia 1.2 akichaguliwa na watu 15 na nafasi
ya 10 amekamata Mwigulu Nchemba akiwa na asilimia 1.0 akichaguliwa na
watu 13.
Wengine
na idadi ya waliowachagua na asilimia zao kwenye mabano ni January Makamba
nafasi ya 11 (asilimia 0.8, watu 10); Dk. Asha-Rose Migiro nafasi ya 12
(asilimia 0.7, watu tisa); Samuel Sitta nafasi 13 (asilimia 0.6. watu
wanane); Lazaro Nyalandu nafasi ya 14 (asilimia 0.4, watu watano).
Pia
wamo Prof. Sospeter Muhongo nafasi ya 15 (asilimia 0.4, watu watano); Balozi
Amina Salum Ali nafasi ya 16 (asilimia 0.2, watu wawili); Dk. Mohammed
Gharib Bilal nafasi ya 17 (asilimia 0.2, watu watatu); Stephen Wasira
nafasi ya 18 (asilimia 0.2, watu 3) na William Ngeleja nafasi ya 19
(asilimia 0.2, watu wawili).
Wengine
ni Balozi Ally Karume nafasi ya 20 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Amos
Siyantemi nafasi ya 21 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Joseph Chagama
nafasi ya 22 (asilimia 0.1, mtu mmoja); na Mwele Malecela nafasi ya 23
(asilimia 0.1, mtu mmoja).
Katika
kura hiyo, watia nia 14 ambao wamejitosa kwenye urais kupitia CCM hawakutajwa
kabisa na watoa maoni ambao ni Balozi Augustine
Mahiga; Boniphace Ndengo; Eldophonce Bihelo; Godwin Mwaipopo; Dk. Hamis
Kigwangalla; Dk. Hans Kitine; Joseph Chagana; Leons Mulenda; Luaga Mpina;
Maliki Marupu; Mathias Chikawe; Monica Mbega; Titus Kamani na Balozi Patrick Chokala.
Kwenye
kundi la Ukawa, namba mbili amechukua Prof. Ibrahim Lipumba akiwa na
asilimia 13.6 akichaguliwa na watu 170; Freeman Mbowe ameshika nafasi ya
tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; James Mbatia
amekamata nafasi ya nne akiwa na asilimia 3.2 akichaguliwa na watu 40; Emmanuel
Makaidi akishikilia nafasi ya tano kwa asilimia 0.6 akichaguliwa na watu 8,
huku George Kahangwa akishika nafasi ya sita kwa asilimia 0.2
akichaguliwa na watu wawili.
Swali
la msingi lililokuwa linaulizwa lilisema: “Kama wewe
leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya
CCM, kati ya wanachama wake 37 waliokwishajitokeza, ungemchagua nani apeperushe
bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Oktoba 2015?”
Pia
swali kwa Ukawa lilikuwa: “Kama wewe leo
ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kati ya wanachama wake
waliokwishakutangaza nia na wanaotarajia kutangaza nia ungemchagua nani
apeperushe bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Oktoba 2015?”
Ripoti
ya REDET imesema kuwa kwa maswali yote, mhoji alitakiwa kutomtajia majina
mhojiwa, bali mhojiwa aliombwa ataje jina alilonalo kichwani mwake.
NIPASHE
Mbunge
wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-
Mageuzi, James Mbatia, amesema hakuna Spika aliyewahi
kuonyesha udhaifu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
alivyoonyesha Anna Makinda.
Amesema Makinda ameligawa vipande
vipande Bunge la 10 na kutumiwa na mhimili wa utawala.
Mbatia alisema badala ya Bunge kuisimamia
serikali, lakini Makinda ameshindwa kuliongoza Bunge hilo kutokana na shinikizo
la mhimili wa utawala na kulazimika kufuata matakwa ya CCM na hivyo kuliongoza
kwa ubabe.
Alisema tofauti na ilivyokuwa katika
kipindi cha Samuel Sitta na
Pius Msekwa ambao walionyesha weledi na kuliongezea heshima Bunge, lakini
Makinda ameriharibu kutokana na kuacha kusimamia Katiba ya nchi katika
kuliongoza Bunge hilo.
“Siku zote mwanamke ndiye
huwa ni mtu wa mwisho kuligawa Taifa, lakini limekuwa ni jambo la ajabu sana
kuona mwanamke huyo ambaye angekuwa mstari wa mbele katika kuitetea nchi hii,
lakini ameamua lifie mikononi mwake, hata bila kuficha ameonyesha wazi kwamba
anatumika na serikali na CCM, Makinda yeye siyo kiranja wa bunge ni
mratibu tu,” Mbatia.
Aliongeza: “ Badala ya Bunge kusimamia serikali kama Mhimili unaojitegemea,
limejivua kazi yake na kuwa kiungo cha serikali na inalisimamia, na ndiyo
maana hata juzi mlisikia Serikali inasema imeoliongezea Bunge siku,
badala ya Bunge lijiongezee lenyewe, hii ni fedheha.”
Mbatia alisema suala la kupelekwa
bungeni kwa hati ya dharura na kujadiliwa miswaada mitatu ya mafuta na gesi ni
ajenda ya siri ya kutaka kuiweka gesi kama dhamana ya CCM ya kupata fedha ya
uchaguzi na kwamba hicho ni kiashiria cha kuanza kuiuza nchi rejareja.
“Raslimali hizi badala ya
kuwa neema kwa Watanzania, sasa inakuwa balaa, watu wachache wanataka kuwaibia
Watanzania, hivi unawezaje kuwekaje miswaada hii muhimu kujadiliwa kwa pamoja
na kuipeleka harakaharaka
hivyo, sisi tumesema hatukubali kuona hujuma hizi zinafanyika dhidi ya
rasilimali na Taifa,”Mbatia.
Mbatia alisema msimamo wa Wabunge wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uko wazi, kwamba hawako tayari kujadiliwa
miswaada hiyo kwa hati ya dharura na pia hawatashiriki wakati wa kuvunjwa bunge
hilo Julai 9, mwaka huu.
Pia aliongeza kuwa hata wakiitwa
katika meza ya maridhiano na Makinda hawatakuwa tayari kushiriki.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kwamba chama hicho kina
ajenga ya siri ya kuifanya gesi kusaidia kuwa dhamana katika
uchaguzi, alijibu kwa kifupi kwamba ni uzushi.
HABARILEO
Mlinzi
wa usiku katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kalambo mkoani Rukwa, Florence Kazonde amejinyonga baada ya
kumuua kikatili kwa kumkaba koo mkewe aliyekuwa na ujauzito wa miezi tisa,
Emilia Mzui.
Chanzo
cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi. Tukio hilo
limethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, majirani na ndugu wa karibu wa
familia ya marehemu hao waliokuwa wanaishi katika Kitongoji cha Namlangwa mjini
Matai yalipo makao makuu ya wilaya ya Kalambo.
Kwa
mujibu wa Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Ramadhan Juma, alikiri kuwa
Kazonde alikuwa mlinzi wa ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo zilizopo
nje kidogo ya Mji wa Matai, lakini hakuwa mwajiriwa wa halmashauri hiyo.
“Kazonde alikuwa anatoka katika kampuni moja ya ulinzi…hakuajiriwa
na Halmashauri hii,“ alisisitiza Juma.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kutokuwa na taarifa
za mkasa huo kwamba akizipata atazitolea taarifa.
Hata
hivyo taarifa kutoka Jeshi hilo la Polisi mkoani humo limethibitisha kutokea
kwa tukio hilo. “Kweli kuna hilo tukio limetokea
wilayani Kalambo … taarifa zipo tayari lakini kwa kuwa mie si msemaji wa Jeshi
hili siwezi kutoa maelezo zaidi ya kina lakini nikiri kuwa tukio hilo limetokea
…Kwa utaratibu wa Jeshi letu ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ndiye msemaji na si
vinginevyo.
Baadhi
ya majirani na ndugu wa karibu kwa masharti ya kutoandikwa gazetini walieleza
kuwa walibaini vifo hivyo baada ya kufika nyumbani kwa wanandoa hao ili
kuwasabahi lakini walikuta milango ya nyumba hiyo imefungwa kwa ndani.
“..Tulihisi labda walikuwa bado wamelala lakini kila tukibisha hodi
ni watoto tu waliokuwa wakiitikia …… “Mazingira hayo yalitutia mashaka makubwa
tukahisi kuwa kwa kuwa mke wake siku zake za kujifungua zilikuwa zimekaribia
tuliamini kuwa walikuwa wamekwenda hospitali na kuwaacha watoto wakiwa
wamejifungia ndani na kushindwa kufungua milango hiyo, “ alisema
mtoa taarifa.
Ilielezwa
kuwa ndugu na majirani hao waliamua kufungua mlango kwa nguvu ili wawatoe
watoto hao wadogo nje ambao walikuwa wawili.
Kwa
mujibu wa mtoa taarifa baada ya kufungua mlango wa nyumba hiyo kwa nguvu mmoja
wa watoto hao aliwaonesha ishara kuwa chumbani kwa wazazi wao kuna kitu cha
kutisha ndipo walipolazimika kuingia chumbani humo na kuona mwili wa Kazonde
ukiwa umening’inia darini ukiwa na kamba ya katani shingoni ambapo mwili wa
marehemu mkewe ulikuwa kitandani.
“Inatisha na kusikitisha sana ….tuligundua kuwa wote wawili walikuwa
wafu tukatoa taarifa mara moja katika Kituo cha Polisi hapa mjini Matai ……
askari Polisi walifika na waganga ambao walifanyia uchunguzi miili hiyo na
kuthibitisha kuwa Kazonde alikuwa amejinyonga baada ya kumuua mke wake kikatili
kwa kumkaba koo,” aliongeza mmoja wa ndugu wa karibu.
Taarifa
kutoka eneo hilo la tukio zinaeleza kuwa kwa muda mrefu wanandoa hao walikuwa
wakigombana mara kwa mara ambapo mume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine na kwamba kati ya watoto wao wawili
mmoja sio wake ni wa mwanamume mwingine.
HABARILEO
Mahakama
ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende,
Alei Charles (CHADEMA) kifungo cha miaka
miwili jela baada ya kukiri kumlinda mshtakiwa Wenceslaus Namwanda “Pepea”
anayemiliki shamba la bangi.
Mshitakiwa
Namawanda ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Mbende anakabiliwa na kosa la
kumiliki shamba la bangi.
Hakimu
wa mahakama hiyo, Adam Mwanjokolo alitoa adhabu hiyo baada ya mshtakiwa huyo
mwenye miaka 30 kukiri kutenda kosa hilo mahamakani hapo .
“Nimelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi
wengine wenye tabia kama yako (Alei)… hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili
jela,“ Hakimu Mwanjokolo.
Awali
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa
mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 14 , mwaka huu katika kijiji cha Mbende , saa
3 usiku.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa usiku huo wa tukio Alei aliwadanganya maofisa wa polisi
kuwa mshtakiwa Namwanda hakuwa mkazi wa kijiji hicho hivyo aliwaelekeza kwa
Mwenyekiti wa kijiji cha jirani.
Kwa
mujibu wa Mwendesha Mashtaka, maofisa hao walithibitishiwa na Mwenyekiti wa
kijiji cha jirani kuwa mshitakiwa wanayemtafuta anaishi katika kijiji cha
Mbende ambapo aliongozana nao hadi nyumbani kwake.
“Maofisa wa Polisi walipofika nyumbani kwa mshtakiwa Namwanda
walipobisha hodi ghafla alitoka mtu baada ya kuona askari alitimua mbio, askari
walifanikiwa kumkamata na ikagundulika kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende
ambapo alikiri kuwa alifika nyumbani kwa mshtakiwa na kumtaarifu atoroke kwa
kuwa alikuwa akitafutwa na Polisi,”
alieleza Mwendesha Mashtaka.
Akijitetea
mshitakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza. Pia
ana watoto wategemezi wawili wa marehemu dada yake ambapo mama mzazi anaishi
naye baada ya mumewe kufariki dunia.
|
No comments:
Post a Comment