KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015:- Watu milioni 11 wajiandikisha BVR. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, July 08, 2015

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015:- Watu milioni 11 wajiandikisha BVR.

Rais Jakaya Kikwete akiweka alama za vidole wakati akijiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapigakura (BVR) kijijini kwake Msoga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani jana. Picha na Ikulu .

Rais Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha ili watumie haki yao kuchagua viongozi wanaowataka kuanzia diwani, mbunge na hata rais na kwamba wasipofanya hivyo, wasije kulalamikia viongozi watakaokuwa madarakani ambao watakuwa wamechaguliwa na wenzao waliojiandikisha. “Napenda niwakumbushe Watanzania wenzangu, jitokezeni kujiandikisha sasa ili mtumie haki yenu ya kupiga kura kuchagua kiongozi, kama diwani, mbunge au rais mnayemtaka ninyi na siyo uache kujiandikisha halafu usipige kura kisha, uje ulaumu ‘huyu naye vipi anatuongozaje?, mbona hafai?’, huku jibu ulikuwa nalo kama ungepiga kura,” alisema Rais Kikwete.
Waziri mkuu wa Tanzania,Mizengo Pinda akiwa na kitambulisho cha mpiga kura.

Wapiga kura  11,248,198 kati ya milioni 22 waliotarajiwa kuandikishwa mwaka huu 2015 katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura nchini Tanzania, wameshaandikishwa na sasa wanamiliki vitambulisho wakisubiri kuvitumia katika uchaguzi mkuu Oktoba, 25 mwaka huu.

Kutokana na  hali hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ina uhakika wa kukamilisha uandikishaji kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) mapema mwezi ujao.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Danian Lubuva, alitoa kauli hiyo jana Julai 07,2015  huko Msoga, Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani ambako Rais Kikwete alikuwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo waliojitokeza kujiandikisha ikiwa ni siku ya kwanza kwa uandikishaji mkoani Pwani.

Jaji Lubuva alimueleza Rais Kikwete kuwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mchakato huo, hali ya uandikishaji ilipofikia nchini hadi Julai 06,2015 inaendelea vema na matumaini ni makubwa kuwa uandikishaji ujao utakamilika mapema na kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa.

“Mheshimiwa Rais, pamoja na changamoto nyingi na kelele nyingi zilizokuwa zikisikika huku na kule, tayari tumeandikisha watu 11,248,198 mpaka jana (juzi) kati ya lengo tulilojiwekea la kuwafikia watu kati ya milioni 21 mpaka 23, na mikoa iliyokuwa tayari imekamilisha ni 13, bado 11 ambayo nayo nakuhakikishia itakamilisha na mapema Agosti, kazi hii itakamilika,” Jaji Lubuva.

Baada ya kujiandikisha, Rais Kikwete aliipongeza Nec kwa hatua iliyofikiwa hadi sasa na kuwataka wasife moyo bali wachape kazi kikamifu ili uandikishaji ukamilike ndani ya muda na wananchi wawe na uhakika wa kupiga kura kwa kutumia vitambulisho hivyo.

Rais Kikwete alisema changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa zuandikishaji  zichukuliwe kama fursa ya kukamilisha kwa wakati.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad