UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:-Mchakato urais Chadema waanza. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, June 24, 2015

UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:-Mchakato urais Chadema waanza.

Wakati makada wa vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF wakiwa wametangaza kugombea urais, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza mchakato wa kumpata mgombea wake wa nafasi hiyo.


Chama cha NCCR-Mageuzi tayari kimemtangaza Dk. Joseph Kahangwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba akijitokeza kuwania kiti hicho kwa mara ya tano.

Kutokana na hali hiyo, Chadema kimesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea urais unaanza Julai 20 hadi 25, mwaka huu, na uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge ulianza Mei 18 hadi Juni 25, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene aliliambia gazeti hili Dar es Salaam jana kuwa uchukuaji wa fomu hizo za ubunge unalenga majimbo ambayo chama hakina wabunge kwa sasa, pamoja na fomu za ubunge wa viti maalumu.

Makene alisema mchakato wa uchukuaji na urudishaji fomu kwa ngazi ya ubunge na udiwani unaendelea vizuri na kwamba mwisho wa wagombea kuchukua na kurudisha fomu hizo ni kesho na baadaye michakato mingine itafuata.

Alisema kwa sasa hana majina ya wabunge au madiwani waliorejesha fomu kwa sababu mchakato huo unafanyika nchi nzima. Alisema wabunge wanarudisha katika majimbo yao na madiwani katika kata zao.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa huenda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa akagombea nafasi hiyo na ndiye anayepewa nafasi kubwa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Dk. Slaa alipeperusha vyema bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa rais baada ya kuibuka mshindi wa pili nyuma ya Rais Jakaya Kikwete.

Mwaka 2005, Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe aligombea kiti cha urais na kwamba mwaka huu, mwenyekiti huyo hajaweka bayana kama atarejea kugombea ubunge katika Jimbo lake la Hai mkoani Kilimanjaro.

Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Salum Mwalimu ameshachukua fomu za kuwania ubunge Jimbo la Mkwajuni Zanzibar. Jimbo hilo ndilo pekee ambalo liliachwa kwa Chadema baada ya majimbo mengine kuachiwa CUF chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa unaunganisha vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, vimepanga kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi wa mwaka huu, na kwamba baada ya kila chama kumpata mgombea wake watakaa kumchagua mmoja kati yao kupeperusha bendera ya upinzani.

Tayari Chama Cha Mpinduzi (CCM), kimeanza mchakato wa kumpata mgombea wake wa urais kwa makada wake kuchukua fomu kutafuta saini za wadhamini 450 kutoka mikoa 15. Mpaka sasa makada ambao wamejitokeza kuchukua fomu ni 40.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad