TUKIO LA UCHOTWAJI MAFUTA YA PETROLI BAADA YA LORI KUPINDUKA NA KULIPUKA MOTO:- laua watatu na Kujeruhi 18 mkoani Mbeya. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, February 20, 2015

TUKIO LA UCHOTWAJI MAFUTA YA PETROLI BAADA YA LORI KUPINDUKA NA KULIPUKA MOTO:- laua watatu na Kujeruhi 18 mkoani Mbeya.

Ilikuwa ni kama marudio ya ajali ya mwaka 2002, lakini ukubwa wa athari za tukio la jana Februari 19,2015 unatofautiana baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuchota mafuta kutoka kwenye lori lililopinduka katika Kijiji cha Idweli.


Lori hilo lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Malawi, lilipinduka kwenye milima ya Mporoto, eneo ambalo ajali kama hiyo ilitokea mwaka 2002 na kuua watu 40 na wengine 100 kujeruhiwa na moto uliolipuka wakati wanakijiji wakijaribu kuiba mafuta kutoka kwenye lori hilo.

Usiku wa kuamkia jana Februari 19,2015, hali ilikuwa kama hiyo katika Kijiji cha Idweli, Rungwe wakati lori jingine lilipolipuka kwenye Barabara ya Mbeya-Malawi.

Akitoa taarifa juu ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema waliofariki na waliojeruhiwa, walikuwa katika harakati za kuiba mafuta kutoka katika gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 891 AQZ likiwa na tela lenye namba T 821 ARF.

Alisema gari hilo mali ya Ailis Sanga, lilipakia petroli yenye ujazo wa lita 41,000, likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilikuwa likiendeshwa na Zawadi Nyato (46) mkazi wa Sae jijini Mbeya akiwa na utingo wake, Frank Yohana (24) mkazi wa Mbozi.

Baada ya kufika kijijini hapo, liliacha njia na kupinduka. Dereva na utingo waliokolewa na kupelekwa kituo cha Polisi Kiwira kupata fomu namba tatu  kwa ajili ya matibabu. 

Kamanda alisema baadhi ya wakazi, walivamia lori hilo na kutoboa tangi la mafuta, hali iliyosababisha mafuta kuanza kumwagika na kusambaa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye makazi ya watu.

Kwa mujibu wa kamanda, watu hao hawakujali hatari iliyokuwa ikiwakaribia, badala yake waliendelea kukinga mafuta kwa kutumia vyombo vyao zikiwemo ndoo, madishi, karai na madumu. 

Katika tukio hilo, watu watatu walifariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa kwa moto uliowafuata hadi kwenye nyumba zao walikoficha mafuta waliyoiba kutoka kwenye lori hilo.

Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Igogwe, Alexanda Masaru alisema alipokea miili miwili ya watu na mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu na wengine 16 walilazwa baada ya kuungua sehemu mbalimbali.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Maria Pajela (18) na William Paschal (38) wote wakazi wa Kijiji cha Idweli na utingo wa gari hilo Frank Chaula.

Waliojeruhiwa ni Shukuru Kanzale (21), Nuru George (30), Asante Boniface (38), Joseph Jamson (18),  Joseph Paschal (30), Siza Kinesa (22), Alex Daud (35), Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37), Samson Mbwila (29).

Wengine ni Dora Michael (35), Veronica Elia (30), Rabsen Ayub (26), Wasiwasi Spika (32), Asia Anon (20), Bahati Kyando (23), Christopher Erasto (32) na Melisa Sanane (50) wote wakazi wa Kijiji cha Idweli.

Majeruhi azungumza.

Mmoja wa majeruhi aliyelazwa kwenye Hospitali ya Igogwe, Wasiwasi Spika alisema aliungua wakati akichota mafuta hayo.

Spika alisema chanzo cha moto ni mtu mmoja aliyeshika kibatari jirani na eneo la ajali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Idweli, Marcus Msomba alisema aliwaonya wakazi hao kukaa mbali na lilipopinduka gari hilo lakini hawakusikia.
UNGANA  NASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad