GHARAMA:- ‘Tozo za huduma za simu hazizuiliki’ - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, February 20, 2015

GHARAMA:- ‘Tozo za huduma za simu hazizuiliki’

Wakati Watanzania wakizidi ‘kutoboa’ mifuko yao kununua vifurushi vya kupiga simu na kutuma ujumbe wa mfupi, baada ya mabadiliko ya viwango vya huduma hizo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo imesema mabadiliko hayo hayazuiliki kutokana na changamoto za uwekezaji.

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Tigo, Cecile Tiano alisema jana Februari 19,2015, kuwa Tanzania ni nchi yenye bei za chini za huduma za simu Afrika Mashariki, huku kodi zake zikiwa juu, jambo linalowapa ugumu kibiashara.

Tuna mipango yetu ya kuwekeza Sh221 bilioni mwaka huu 2015, lakini hatuwezi kuendeleza uwekezaji huo kwa mazingira magumu yaliyopo,” alisema Tiano.

Tigo ambao waliongeza wateja wao kwa asilimia 20 hadi kufikia wateja milioni tisa mwaka jana, wanatarajia kuongeza minara 787 ya intaneti ya 3G na 4G.

Mabadiliko ya huduma za vifurushi vya simu katika mitandao ya Tigo na Vodacom yamezua mjadala mzito nchini hasa kwa watumiaji wa mtandao wa intaneti.

Mwanzoni mwa wiki, Vodacom wakati ikitoa taarifa za maendeleo ya biashara yao ilibainisha kuwa walilazimika kufanya mabadiliko hayo ili kukwepa hasara.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), tayari imeziagiza kampuni zote zilizofanya mabadiliko hayo kutolea maelezo.

Tiano alisema ushindani mkubwa uliopo nchini ni miongoni mwa sababu nyingine inayozifanya kampuni za huduma za simu kufanya uamuzi na mabadiliko ya bei mara kwa mara kukabiliana na hali ya soko.

“Hivyo basi, iwapo washindani wetu wakifanya uamuzi au mabadiliko, lazima na sisi tuendane nayo haraka ili kuhakikisha hatuathiriki kibiashara. Hicho ndicho tulichafanya wiki iliyopita,” alisisitiza Tiano.

Alipoulizwa kwa nini walifanya mabadiliko hayo kwa siri tofauti na walivyokuwa wakitangaza huduma hizo awali wakati wakizianzisha, alisema suala hilo TCRA imewataka kulitolea maelezo.

Vodacom nayo imetangaza kuwekeza Sh150 bilioni ili kujitanua na kuboresha huduma zake mwaka 2015. 

Kiwango kikubwa cha fedha hizo zitatumika katika upanuzi wa mitambo ya intaneti ya 2G na 3G na kuboresha M-Pesa na ubunifu zaidi.

Sorce:-Mwananchi.


UNGANA  NASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad