![]() |
Clement
Mabina enzi za uhai wake…ambapo baada ya kumpiga risasi raia mmoja na yeye
kuuawa katika ugomvi wa mashamba!
|
Mwenyekiti wa zamani wa
chama cha mapinduzi(CCM) mkoa wa Mwanza Clement Mabina ambaye pia ni diwani wa
kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza ameuawa na wananchi wenye hasira
katika ugomvi wa mashamba.
Tukio la kuuawa kwa
Mwenyekiti huyo wa Ccm Mkoa wa Mwanza ambaye alishindwa katika uchaguzi wa nafasi
ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza mwaka jana na Waziri wa zamani na Mbunge wa
zamani wa Ilemela Dk Antony Diallo lilitokea leo asubuhi katika eneo la kijiji
cha Kanyama wilayani Magu.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa polisi wa wilaya(OCD) ya Magu ODC
Mkapa pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu Desdery Kiswaga
zimeeleza kuwa tukio limetokea majira ya saa mbili asubuhi.
ODC Mkapa alikiri kutokea
kwa tukio la kupigwa na kuuawa kwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Ccm Mkoa na
Mwenyekiti wa zamani wa Halmashauri ya wilaya ya Magu baada ya kutokea
kutokuelewana baina yake na wananchi wa eneo la kijiji cha Kanyama alikokuwa na
shamba lake alikokuwa amekwenda kupanda miti.
Naye Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Magu Desdery Kiswaga alisema kuwa amepokea taarifa za
kuuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kutokana na ugomvi wa mashamba na
kuelezwa kuwa amesikitishwa sana na kuuawa kwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Halmashauri
ya wilaya ya Magu.
Taarifa zaidi toka eneo la
tukio la Kanyama kulikotokea mauaji hayo zimeeleza kuwa Mwenyekiti huyo wa
zamani wa Ccm alifika katika eneo hilo majira ya asubuhi kwa ajili ya kupanda
miti katika eneo la milima ya Kanyama ambalo analimiliki ambavyo hata hivyo
linadaiwa kuwa na mgogoro baina yake na wananchi.
Baada ya kufika katika eneo
hilo,wananchi nao walifika katika eneo hilo na kumhoji sababu za kupanda miti
katika eneo hilo ambalo bado lina mgogoro wa umiliki na kutokea kutokuelewana
baina yake na wananchi.
Baada ya majibishano ya muda
mrefu na kuona wananchi wameanza kumzingira Mabina aliamua kufyatua risasi
hewani kuwatawanya wananchi hao ambapo kwa bahati mbaya mojawapo ya risasi hizo
zilimpiga mtoto aliyekuwa katika eneo hilo na kupoteza maisha.
Taarifa hizo toka katika
eneo hilo la tukio zimeeleza kuwa kutokana na tukio hilo wananchi walimzingira
Mabina na kuanza kumpiga kwa silaha mbalimbali za jadi kama vile mapanga,
fimbo, mawe, mikuki na kusababisha kifo chake papo hapo.
Kabla ya kurejea chama cha
mapinduzi(ccm) na kufanikiwa kuwa diwani wa Kata ya Kisesa na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Magu, Mabina aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha
NCCR-Mageuzi na aligombea nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo mwaka 1995 na
kushindwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Malaki Lupondije.
Source:-gsengo
No comments:
Post a Comment