Jitihada za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mzozo kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zinaelekea kugonga mwamba. |
Tanzania
Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya kutosha katika hujuma dhidi
ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani wa chama hicho kuunda mgogoro
na kukipasua.
Hata hivyo,
licha ya misukosuko na kelele kutoka kwa baadhi ya wanachama na wanaodhaniwa
kuwa ‘mapandikizi’, CHADEMA kimeweza kupuuza hujuma hizo na kujikita katika
harakati za ujenzi wa ngazi za chini za chama katika vijiji na vitongoji.
Kwa sasa
viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika majimbo 103 nchi nzima kujenga
chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu lililoketi mwishoni mwa mwaka jana,
kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko, na ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi
unaokuja.
Baadhi ya
wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali wamekuwa wanashirikiana na wana
CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya CHADEMA mtandaoni na mitaani.
Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango na kuyapeperusha katika mikutano
inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa
ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga
uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson
Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Kitila amevuliwa
wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba amevuliwa wadhifa wa Mwenyekiti wa
Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ‘usaliti’.
Katika
kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama wamekuwa wakitoa matamko, huku
wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika mikoa ya Lindi na Singida.
Huku wakitoa
shinikizo kwa chama Zitto asichukuliwe hatua zaidi, baadhi yao mkoani Kigoma
walikwenda mbali wakitaka chama kiahirishe ziara ya Dk. Slaa mkoani humo hadi
baadaye, kwa kisingizio cha usalama.
Hata hivyo,
Dk. Slaa alisisitiza kuwa masuala ya usalama yamezingatiwa barabara, na kwamba
ziara ziko pale pale, kwani hakuna mkoa au wilaya ya mtu.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa uongozi wa CCM mkoani Kigoma, chini ya Dk. Aman Walid
Kabourou, umekuwa ukiratibu vitisho na fujo katika mikutano au maeneo
anayotembelea Dk. Slaa kwa lengo la kutisha wananchi.
Dk. Kabourou
aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya CHADEMA kabla ya kukimbilia
CCM miaka kadhaa iliyopita. Alipohamia CCM akapewa ubunge wa Afrika Mashariki.
Sasa ndiye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.
Makundi ya
vijana wa CCM na wana CHADEMA wenye matatizo na chama, wamekuwa wakisambazwa
kuelekea maeneo kadhaa kwa lengo la kuhujumu mikutano ya Dk. Slaa.
Lengo ni
kutumia fursa hii kujaribu kudhoofisha uwezo wa chama kinachohatarisha utawala
wa CCM.
Miongoni mwa
mikakati ya kuivuruga CHADEMA inayofadhiliwa kwa gharama kubwa ni kuwapandikiza
vijana kufanya fujo katika mikutano ya Dk. Slaa.
Katika
mikutano hiyo vijana mbalimbali wamekuwa wakijitokeza na mabango ya kupinga
uamuzi wa kuondolewa kwa Zitto, kuzomea na kufanya vituko vyenye lengo la
kuharibu mikutano hiyo.
Miongoni mwa
matukio hayo ni lile lililotokea juzi katika Kijiji cha Mabamba wilayani
Kibondo, ambako zaidi ya vijana saba walikamatwa na kufikishwa kwenye kituo cha
polisi.
Hata hivyo,
baadhi ya watu waliokuwapo eneo la tukio waliwatambua kuwa wengi wao ni vijana
wa CCM ambao wamekuwa wakizunguka katika mikutano yote anayofanya Dk. Slaa.
Katika
mikutano yake mkoani Shinyanga na Kigoma, Dk Slaa, alisema propaganda za udini,
ukabila na ugaidi zinazopandikizwa na CCM zimezidi kuimarisha chama chake
katika safari ya kuelekea Ikulu mwaka 2015.
Dk. Slaa
alisema wanaosema CHADEMA itakufa hawajui kinachoendelea, kwa sababu ya uamuzi
wa kuwachukulia hatua au kuwaondolea nyadhifa watu wasiotaka kufuata maadili,
katiba na miongozo ni njia ya kukipa uhai chama hicho.
“Mimi
nilidhani CCM wangeshangilia chama chetu kufa, lakini hiki ninachokiona
kinanistaajabisha; yaani eti wanatuonea huruma sisi tusife? Huu ni muujiza,”
alisema.
Tanzania
Daima Jumapili, limekuwa likidokezwa kuwa viongozi wa CCM wamekuwa wakifadhili
harakati za kuidhoofisha CHADEMA ili wasipate upinzani mkali katika uchaguzi ujao.
Wiki
iliyopita kupitia ukurasa wake wa facebook, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (bara),
Mwigulu Nchemba aliandika kuwa Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa
CHADEMA, Benson Kigaila aliyekuwa Kigoma alipigwa na wafuasi wa Zitto hadi
kushindwa kusimama hadi aliposaidiwa na polisi.
Wakati
Mwigulu akituma maneno hayo kupitia ukurasa wake, Kigaila amesema kuwa yeye
yupo katika ziara ya kujenga chama mkoani Mbeya, na aliondoka Tukuyu kwenda
Njombe kwa kazi hiyo hiyo.
Wakati wana
CCM wakishangilia kile kinachoitwa mpasuko ndani ya CHADEMA, Dk. Slaa anasema
wanazidi kuimarika na watafanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo.
Katika
mazungumzo yake na Tanzania Daima, wiki iliyopita, Dk. Slaa aliwataka
Watanzania wawe makini, kwani hao wanaotoa matamko ya kulaani Kamati Kuu
wanafanya kazi ya CCM, hata kama baadhi yao wana kadi za CHADEMA.
“Wanaojitokeza
kutoa matamko kulaani Kamati Kuu ya CHADEMA hawazungumzi bei ya umeme kupanda,
hawazungumzi hali mbaya ya elimu na afya nchini, hawazungumzii suala la
mishahara ya wafanyakazi, wamejikita kumjadili Mbowe na Slaa.
“Niwahakikishie
wanachama na Watanzania wanaotaka mabadiliko kuwa tuna usalama uliokomaa
tunajua hujuma zote, ndio maana jana Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba,
aliwatangazia Watanzania kuwa Mkurugenzi wetu wa Oganaizesheni na Mafunzo
Benson Kigaila amepigwa na wafuasi wa Zitto na amesaidiwa na polisi wala
hajiwezi hata kusimama.”
Dk. Slaa
alisema wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa chama hicho wapo kwenye majimbo
103 nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa chama ngazi ya msingi, kutekeleza uamuzi
wa Baraza Kuu.
Alisisitiza kuwa ziara hizo hazina uhusiano na propaganda
zinazosambazwa sasa kuhusu hatua ya chama hicho kumvua vyeo Zitto.
ZAIDI HAPA:- http://www.freemedia.co.tz/daima/chadema-yadinda
No comments:
Post a Comment