Serikali ya
Tanzania imewarejesha kwao kwa hiari wakimbizi wapatao 569,018 toka nchi za
Maziwa Makuu waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini kutokana na machafuko katika
nchi zao.
Kati ya hao
502,358 walitoka nchini Burundi na 66,660, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakimbizi
hawa wamerejeshwa kwao kufuatia zoezi lililoanzishwa rasmi mwaka 2002 kwa
wakimbizi toka Burundi na mwaka 2005 kwa wakimbizi toka Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo (DRS), baada ya usalama katika nchi zao kuimarika.
Sambamba na
mafanikio haya, pia kambi 12 kati ya 13 zilizokuwa zikitumika kuwahifadhi
wakimbizi hawa zimefungwa, na hadi sasa ni kambi moja tu ya wakimbizi ya
Nyurugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma ndiyo iliyobakia ikiwahifadhi
wakimbizi kutoka DRC (63,728), Burundi (4,153) na nchi nyingine mchanganyiko za
Kiafrika (212).
Tanzania
inajulikana kimataifa kama nchi mojawapo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa
kutoa hifadhi kwa wakimbizi wanaokimbia nchi zao kutokana na machafuko ya
kiaiasa ambapo mwaka 1995 idadi yao ilifikia zaidi ya milioni moja.
Lengo la
Serikali ni kuona kuwa suala la kuhifadhi wakimbizi hapa nchini linafikia ukomo
na juhudi zinaendelea kuona kuwa hata Kambi ya Nyarugusu ambayo ndiyo kambi
pekee iliyobakia inafungwa baada ya wakimbizi walio katika kambi hiyo
kurejeshwa kwao, pale hali ya usalama nchini DRC itakapokuwa imeimarika.
Kuondoka kwa
wakimbizi hawa sasa kunatoa nafasi kwa Serikali na wananchi kutumia kwa
shughuli nyingine za kimaendeleo maeneo makubwa yaliyokuwa yanatumika kuhifadhi
wakimbizi, lakini pia kunatoa nafasi nzuri ya kuweza kukabiliana na changamoto
za kiusalama katika maeneo hayo ambayo yapo katika mikoa ya mpakani mwa
nchi.
Serikali inapenda kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja
wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa misaada ya hali na mali
waliyotoa na wanayoendelea kutoa kusaidia hifadhi ya wakimbizi hapa nchini.
Pia
Watanzani wote na hasa wale wa mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera kwa
ushirikiano waliotoa kwa wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa katika maeneo yao,
na nchi za Burundi, Congo kwa ushirikiano wao uliowezesha kuwarejesha raia wao
waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini.
Mashirika
mengine ambayo pia yalihusika na yanaendelea kutoa huduma za kibinadamu kwa
wakimbizi ni pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP), Mfuko wa Umoja wa
Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kamati ya Kimataifa ya Uokozi (IRC), na
Shirila la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS).
Imeandaliwa
na
Felix Mwagara
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment