 |
Spika wa Bunge la Muungano Bi. Anne Makinda.
|
Katika kikao cha
Bunge la Bajeti kinachoendelea hivi sasa
mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe
alilazimika kusimama na kutoa majibu kwa swali lililoulizwa na Mbunge wa Konde,Bw.
Khatibu Said Haji (CUF) aliyetaka kujua msimamo wa Tanzania kuhusu suala la
kuridhia ndoa za watu wa jinsia moja hasa baada ya shinikizo la nchi wahisani
kuwa awtasitisha misaada kwa nchi zitakazoweka vikwazo kwa watu wa kundi hilo.
Akijibu swali hilo Bw.
Membe ameelezea msimamo wa Tanzania, amesema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inatafsiri ndoa
kuwa ni muungano wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke wenye lengo la kudumu
katika maisha ya wawili hao.
Akasema suala la
msingi ni kuwa, kulingana na matakwa ya sheria ya Tanzania ili kuwepo na ndoa
inayotambulika kisheria ni lazima kuwepo na pande mbili za jinsia tofauti,
yaani mwanamume na mwanamke.
“Dini zetu zote za
hapa nchini hazikubaliani na uwepo wa ndoa za jinsia moja na viongozi wake wapo
kwenye mstari wa mbele kukemea jambo hili,” alisema Membe.
 |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard
Membe.
|
Akasema utamaduni
wetu na sheria zetu hazitambui ndoa ya jinsia moja. Akasema muungano kati ya
watu wa jinsia moja, yaani mwanamume na mwanamume mwingine au mwanamke na
mwanamke mwingine hautambuliki kama ndoa kisheria nchini Tanzania.
Katika swali la
nyongeza, Haji pia alitaka kujua ni mikakati gani Tanzania imejiwekea endapo
nchi hizo wahisani zitasitisha misaada yao kwa nchi hii, kutokana na msimamo
wake ambapo Membe alisema fursa za kiuchumi ambazo zimeendelea kuibuliwa nchini
ni moja ya mikakati ya Serikali kuhakikisha kuwa inajitegemea kiuchumi badala
ya kuzitegemea nchi wahisani.
Alitoa mfano wa gesi
iliyovumbuliwa katika mikoa ya Kusini kuwa ni moja ya nguzo ya uchumi ambayo
Tanzania itaitumia ili iweze kujiendesha kiuchumi mara nchi wahisani
waking’ang’ania sharti hilo la kuruhusu ushoga. Membe akasema rasilimali hizo
na nyingine zikitumiwa vizuri hakuna taifa ambalo litaichezea Tanzania hovyo hovyo kwa kuwapa masharti ya ajabu.
 |
Bendera ya Taifa ya
Tanzania.
|
Waziri Membe amesema
itakapotokea wahisani wanasitisha misaada kwa sababu ya msimamo wa Tanzania wa
kupinga ndoa za jinsia moja, Watanzania wako tayari kujifunga mikanda na
kujibeba wenyewe badala ya kukubali kudhalilishwa utu na utamaduni wao.
Membe ameliambia Bunge
kuwa Tanzania itaendelea kupokea misaada ile tu ambayo haina masharti ya
kubadili sera, utamaduni na sheria za nchi kuhusu ndoa za jinsia moja.
“Nchi marafiki
duniani zikiwemo zile za Magharibi, zimeendelea kutuheshimu kutokana na msimamo
wetu huo thabiti na usiotetereka kwa kuendelea kutoa misaada ya ushirikiano wa
kiuchumi kwa Serikali ya Tanzania,” alisema Membe.
No comments:
Post a Comment